
Kocha mkuu wa Yanga sc, Marcio Maximo (kushoto) akimuelekeza jambo mshambuliaji wa klabu hiyo, Jeryson John Tegete
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
KATIKATI ya wiki hii, Yanga sc ilishuka dimbani
kucheza mechi ya kimataifa ya kirafiki dhidi ya Thika United kutoka nchini
Kenya katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam na kushinda bao 1-0.
Bao pekee la Mbrazil, Geilson Santos Santana
‘Jaja’ katika dakika ya 60 lilitosha kumpa kocha wa Yanga, Marcio Maximo
ushindi wa nne mfululizo katika mechi nne za kirafiki ilizocheza mpaka sasa.
Katika mchezo huo kuna mapungufu kadhaa
yalijitokeza katika kikosi cha Yanga hususani kipindi cha kwanza, lakini
nadhani ilichangiwa na ubora wa Thika United ambayo ilionekana kucheza kitimu
zaidi kwasababu ipo katika ligi inayoendelea wakati wanajangwani wanatengeneza
timu.
Kuna mambo matatu Maximo huwa anapenda kusema kila
baada ya mchezo.
Moja ni kutokuwa tayari kumzungumzia mchezaji
mmoja mmoja katika kikosi chake.
Pili ni kuepuka kuzungumza mapungufu ya timu
hadharani, akiamini njia nzuri ni kuzungumza nao katika kikao cha ndani baada
ya mechi.
Tatu ni kutokuwa na wachezaji wenye namba za uhakika
badala yake kuwa na kundi la wachezaji wenye utayari wa kutumika muda wowote.
Ninavyomfahamu Maximo ni kocha anayependa kuongoza
timu yenye morali kubwa na hapendi kuona kuna mpasuko miongoni mwa wachezaji.
Zipo sababu nyingi zinazochangia timu kuwa na
morali, mojawapo ni kuzungumza na wachezaji kama timu na sio kushusha lawama
kwa baadhi ya wanandinga wanaofanya vizuri.

Marcio Maximo (katikati) akiwa na wachezaji wake kisiwani Pemba walipoweka kambi ya siku tano na tano nyingine kisiwani Unguja
Kuna baadhi ya makocha wa ndani na kimataifa huwa
wanazungumza na mchezaji mmoja mmoja pale yanapotokea makosa binafsi na
anamuagiza cha kufanya bila wenzake kujua.
Hii inatokea pale ambapo kocha anagundua kuna
sababu binafsi zilimfanya mchezaji wake acheze chini ya kiwango au kufanya
makosa binafsi uwanjani.
Maximo kwa upande wake anasema hataki kumzungumzia
mchezaji mmoja mmoja kwasababu timu inaundwa na wachezaji 11 uwanjani.
Makosa ni sehemu ya mpira na ili ufunge goli
lazima mpinzani akosee na ili ufungwe goli lazima wachezaji wa timu yako
wakosee.
Mapungufu uwanjani ni jambo la kawaida na
linatokea duniani kote, lakini baadhi ya makocha wanashindwa kutatua matatizo
hayo kwa busara badala yake wanawabebesha lawama baadhi ya wachezaji.
Jambo hilo huwafanya wachezaji waingiwe na uoga na
kujikuta wakishindwa kucheza mpira vile wanavyofikiria wakihofia lawama kutoka
kwa kocha.
Ili kuepusha hilo, Maximo anapenda kuzungumzia
‘kufeli’ kwa timu kama timu na sio makosa binafsi ya Nadir Haroub au Kelvin
Yondani.
Kosa la Mrisho Ngasa linajadiliwa kama timu na sio
kumzungumzia Ngasa kwa makosa yake binafsi.

Marcio Maximo anasema hakuna mchezaji mwenye namba ya uhakika
Hili ni jambo zuri na litazidi kuipa nguvu Yanga
kama timu na wachezaji watakuwa huru kucheza mpira kwa maelekezo ya Maximo.
Jambo la pili ni Maximo kutumia vikao vya ndani
kuzungumza mapungufu ya wachezaji na kuwaagiza nini cha kufanya mechi zilizopo
mbeleni.
Ni jambo la busara zaidi kuliko kuanika kila kitu
hadharani. Kuna baadhi ya makocha wanashindwa kuvumilia na kujibu kila
wanaloulizwa.
Ni kawaida kumsikia kocha akizungumzia mapungufu
ya timu, lakini waliowengi wanatumia zaidi nafasi husika na sio kutaja moja kwa
moja mchezaji aliyechemsha.
Kocha anaweza kusema timu yangu ilikuwa na
matatizo safu ya ulinzi au kiungo, lakini ni mara chache kumzungumzia mchezaji
mmoja mmoja tu.
Kila mtu ana mtazamo wake kuhusu soka na kwa
bahati mbaya waliowengi tunajifanya tunajua zaidi ya makocha, lakini ukweli
unabakia palepale kuwa mashabiki wengi wa soka huwa hawana utaalamu wa kiufundi
na kimbinu katika soka.
Ni rahisi kumsikia shabiki akishusha lawama kwa
mchezaji mmoja anapofanya makosa na kupiga kelele atolewe, lakini ni ngumu
kujua kwanini kocha anaendelea kumtumia uwanjani licha ya wengi kuona hafai.
Mwalimu anapanga wachezaji kutokana na aina ya
mpinzani wake, na ndio maana unaweza kuona mchezaji fulani hachezi mara kwa
mara, lakini kuna mechi anapangwa kwa dakika zote 90.

Kocha anaelewa kuwa atasaidia kupata matokeo
kuliko mnayemtaka ninyi, lakini linapotekea kosa, mwalimu ana namna ya
kuzungumza na mchezaji huyo.
Ndio maana Maximo anatambua kuwa mapungufu ya
wachezaji lazima waambiwe wao. Kuna maana gani kuzungumzia kila kitu kwenye
vyombo vya habari.
Kuna faida gani umma wa wapenda michezo kujua kila
kitu kuhusu mapungufu ya timu? Kwani wao wana nafasi gani?
Kazi ya shabiki ni kushangilia mpira tu unaochezwa
na wachezaji kwa kuzingatia falsafa ya mwalimu wao.
Mambo ya kimbinu na kiufundi ni kocha na wachezaji
wake, hivyo hakuna haja sana kumwambia shabiki mapungufu ya wachezaji badala ya
kuwaambia wao wenyewe.
Ni jambo nzuri kukosolewa katika kikao cha ndani
kuliko kukosolewa hadharani. Kuna watu hawana uvumilivu, ukikosolewa hadharani
nao huongezea kwa kuponda zaidi.
Kupondwa pia huwapunguzia ufanisi wachezaji, hivyo
njia bora ni kukaa nao kwa busara bila watu kujua nini mmezungumza.
Kwa hili Marcio Maximo nadhani yuko sahihi na
itamsaidia sana kujenga morali ya wachezaji wake.
Kitu kingine muhimu alichofanya Maximo ni
kuwafanya wachezaji wote wajitume kwasababu hakuna mwenye uhakika wa namba.
Maximo anapenda kuwa na kundi la wachezaji wenye
uwezo wa kutumika muda wowote, hivyo anawajenga wachezaji wote katika utayari
wa kucheza.
Moja ya matatizo ya timu za kibongo ni kuwa na
idadi ya wachezaji Fulani wenye uhakika wa namba, lakini wengine wanakamilisha
idadi tu ya wachezaji wa timu.

Mchezaji anakaa msimu mzuri bila kucheza mechi
yoyote, siku akiingia uwanjani kutokana na kukosekana kwa mchezaji muhimu,
unamuona kabisa akitetemeka.
Madhara ya kuwa na wachezaji wenye namba za
uhakika na wengi kutokuwa na uhakika wa kucheza ni pale inapotokea majeruhi,
kocha anashindwa cha kufanya kwasababu waliopo benchi hawajiamini.
Maximo kuwaaminisha wachezaji wote kuwa wana
nafasi ya kucheza, ni jambo muhimu na litafanya wote wajiamini na kujituma
zaidi.
Lakini ukweli ni kwamba kuna nafasi huwa zina watu
wake na si rahisi kumchomoa mchezaji.
Timu lazima iwe na wachezaji wa kikosi cha kwanza,
ndivyo ilivyo duniani kote, lakini ni jambo zuri kuwa na timu yenye kundi kubwa
la wachezaji wenye utayari wa kucheza.
Kwa hili pia, Maximo anaendelea hisia nzuri kwa
wachezaji wa Yanga na itamsaidia kufanikiwa malengo yake.
Wakati huo huo,timu ya Young Africans
itashuka dimba la Uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam siku ya jumapili kucheza
mchezo wake wa mwisho wa kirafiki wa kimataifa dhidi ya timu ya Big Bullets FC
(zamani Bata Bullets) inayoshiriki Ligi Kuu ya TNM nchini Malawi.
Siku ya jumapili mechi inatarijiwa
kuanza majira ya saa 10 kwa saa za Afrika Mashariki na viingilio vya mchezo ni
kama ifuatavyo:
VIP A Tshs 30,000/=
VIP B & C Tshs 20,000/=
Orange Tshs 10,000/=
Blue & Green Tshs 5,000/=

0 comments:
Post a Comment