
Kikosi cha JKT Ruvu Stars msimu uliopita
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 16, 2014, saa 6:49 mchana
MAAFANDE wa JKT Ruvu Stars kutoka mkoani Pwani
wanashuka dimbani jioni ya leo kukipiga dhidi ya wakata miwa wa Mtibwa Sugar
katika mechi ya kirafiki itakayocheza uwanja wa Bandari Tandika jijini Dar es
salaam majira ya saa 10:00 jioni.
Waandaaji wa mechi hiyo wamesema kiingilio katika
mtanange huo unaozikutanisha timu mbili za ligi kuu Tanzania bara ni buku tu
(1,000/=)
Kocha wa JKT Ruvu, Fredy Felix Minziro amesema
maandalizi kwa ajili ya mechi hiyo yanakwenda vizuri na wanatarajia kupata
kipimo kizuri kutoka kwa Mtibwa Sugar.
“Maandilizi yamekwenda vizuri kwa maana ya kwamba,
tumepata kikosi kizuri. Juzi tulicheza
mechi ya kirafiki na Polisi Morgoro na kushinda mabao 3-1”. Alisema Minziro.
“Kupata timu ya ligi kuu ni nafasi nzuri ya
kuwaona vijana wangu, nadhani mechi dhidi ya Mtibwa Sugar itakuwa kipimo kizuri
na tutapata mazoezi mazuri’
Kuelekea msimu ujao wa ligi kuu, Minziro alisema
kikosi chake kitafanya vizuri kutokana na maandalizi ya muda mrefu
wanayoendelea nayo mpaka sasa.
“Ninaamini wachezaji watafanya vizuri msimu ujao
kwasababu wanaonesha kuimarika. Nina mpango wa kucheza mechi za kirafiki dhidi
Ruvu Shooting, Simba na Yanga kama watakuwa tayari”.
Kwa upande wake kocha wa Mtibwa Sugar, Mecky
Mexime alisema mechi ya leo ni kipimo kizuri kwake kwasababu JKT Ruvu ni timu
bora.
“Sisi tunaendelea vizuri na maandalizi na
tunacheza na JKT Ruvu.Tunaamini itakuwa mechi nzuri”. Alisema Mexime.
“Ruvu tunawaheshimu, lakini tumesajili vizuri na
tutaonesha burudani nzuri. Niwaombe mashabiki wafike kwa wingi kuona mpira wa
kiwango cha juu”

0 comments:
Post a Comment