
Na Boniface Wambura, Dar es salaam
Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) zimezipiga
faini ya kati ya sh. 300,000 na sh. 500,000 klabu za Mshikamano FC, Pachoto
Shooting Stars, Town Small Boys na Kiluvya United kutokana na makosa mbalimbali
ikiwemo viongozi, wachezaji na washabiki kufanya vurugu kwenye mechi za Ligi ya
Mabingwa wa Mikoa (RCL) iliyomalizika hivi karibuni.
Uamuzi huo umefanywa na Kamati ya Mashindano ya TFF
iliyokutana juzi (Juni 23 mwaka huu) jijini Dar es Salaam kupitia masuala
mbalimbali ikiwemo taarifa za mechi, na malalamiko kutoka kwa baadhi ya timu
zilizoshiriki RCL iliyochezwa katika vituo vya Mbeya, Morogoro na Shinyanga.
Town Small Boys ya Ruvuma imepigwa faini ya sh.
500,000 kwa mujibu wa kanuni ya 37(13) ya Kanuni ya RCL kutokana na udanganyifu
kwa kumtumia mchezaji Agaton Mapunda ambaye hakustahili ingawa usajili wake ulithibitishwa
na TFF, kwa kutokuwepo pingamizi kutoka klabu yoyote katika kipindi cha
pingamizi.
Licha ya usajili wake kuthibitishwa na TFF, Kamati
ilibaini mchezaji huyo hakutoka ndani ya Mkoa wa Ruvuma kama kanuni za RCL
zinavyoelekeza. Hata hivyo, matokeo ya mechi hiyo dhidi ya Njombe Mji
iliyomalizika kwa bao 1-1 yanabaki kama yalivyo kwa mujibu wa kanuni ya Kanuni ya 52
(3 na 4) na 31(11) ya RCL kwa kuwa mchezaji
Mapunda alithibitishwa na TFF (qualified player).
Vilevile mchezaji huyo amepigwa faini ya sh. 200,000
kwa mujibu wa kanuni za 48(4) na 31(11) za RCL. Nayo malalamiko ya Njombe Mji
dhidi ya mchezaji David Noel Makakala kuwa ndiye aliyecheza mechi hiyo badala
ya Carlos Mapunda yametupwa kwa kukosa vielelezo na ushahidi wa kuthibitisha
hilo.
Kiluvya United
FC ya Pwani imepigwa faini ya sh. 300,000 kwa mujibu wa kanuni ya 37(1) kutokana
na vurugu za washabiki wake kwenye mechi namba 46 dhidi ya Abajalo iliyochezwa
mjini Morogoro.
Pachoto
Shooting Stars ya Mtwara na Mshikamano FC ya Dar es Salaam zimepigwa faini ya sh.
500,000 kila moja kwa kufanya vurugu kubwa kwenye mechi yao namba 100 iliyovunjika
mjini Morogoro. Pia Mshikamano FC wamepewa pointi tatu na mabao matatu kwa
mujibu wa kanuni ya 23(1na5) na 22(d).
Wachezaji na viongozi
wa Pachoto Shooting na wachezaji wa Mshikamano FC waliofanya vurugu na kupigana,
suala lao linapelekwa kwenye Kamati ya Nidhamu ya TFF kwa uamuzi na hatua za
kinidhamu.
Nayo Tanzanite
ya Manyara imefungiwa kucheza mashindano yote rasmi kwa msimu mmoja, na
kuteremishwa daraja hadi ligi ya wilaya mara itakapomaliza kifungo chake kwa
mujibu wa kanuni ya 21(3)(a), 37(14) na 22(a). Tanzanite iliadhibiwa kwa mujibu
wa kanuni ya 23(1,5 na 6) baada ya kumpiga mwamuzi kwenye mechi dhidi ya AFC na
baadaye kugomea mchezo. Ilishindwa kulipa faini na kujitoa mashindanoni kwa
kuondoka kituoni.
Wachezaji
wanaotuhumiwa kumpiga mwamuzi mpaka kumjeruhi suala lao litapelekwa kwenye
Kamati ya Nidhamu ya TFF.
Kamati
imetupa malalamiko ya African Sports ya Tanga dhidi ya Abajalo ya Dar es Salaam,
Ujenzi FC ya Rukwa dhidi ya AFC, Panone FC ya Kilimanjaro dhidi ya Volcano FC
ya Morogoro, na Mvuvumwa FC ya Kigoma dhidi ya Mbao FC ya Mwanza kwa kukosa
vielelezo na ushahidi.
Pia
malalamiko ya Mvuvumwa FC dhidi ya Geita Veterans ya Geita juu ya kuwachezesha
Ibrahim Alphonce, Zamoyoni Magoma na John Mtobesya kwa kuwa hawakusajiliwa
yametupwa kwa vile wachezaji hao ni halali, isipokuwa orodha ya wachezaji wa
Geita Veterans FC iliyotolewa kwa ajili ya pingamizi ilikuwa na upungufu kiuchapaji
ambapo wachezaji sita hawakuorodheshwa.
Nao
makamishna Edward Hiza na Jimmy Lengwe waliokuwa kituo cha Morogoro wamepewa
onyo kutokana na ripoti zao kuwa na upungufu.
Vilevile
Kamati ya Mashindano imezitangaza rasmi timu za African Sports, Geita Veterans
na Panone FC kupanda kucheza Ligi Daraja la Kwanza (FDL) msimu wa 2014/2015
0 comments:
Post a Comment