Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Mei 23, 2014 saa 11: 00 jioni
NAHODHA wa zamani wa klabu ya Yanga na timu ya
taifa ya Tanzania, Taifa Stars, Shadrack John Nsajigwa Mwandemele amewataka
wachezaji wa Taifa Stars kufuata maelekezo ya mwalimu wao na kuzingatia nidhamu
ya mchezo katika mechi ya marudiano dhidi ya Zimbabwe, mjini Harare, juni 1
mwaka huu.
Taifa Stars iliyopata ushindi mwembamba wa bao 1-0
kwenye uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam katika mechi ya kwanza kuwania
kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza fainali za AFCON mwakani
nchini Morocco, inahitaji sare ya aina yoyote ile au ushindi ili kusonga hatua
inayofuata.
Mshindi wa jumla baina ya Taifa Stars na Zimbabwe atachuana
na mshindi kati ya Msumbiji dhidi ya Sudan ya kusin, lakini mechi ya kwanza
iliyopigwa mjini Maputo, Msumbiji walishinda kwa mabao 5-0, hivyo kuweka mguu
nje-ndani.
Akizungumza na MPENJA
BLOG, Nsajigwa alisema mechi za ugenini huwa ni ngumu kwasababu
wenyeji wanashambulia sana, hivyo ni
jukumu la wachezaji wa Stars kujipanga na kuwa na nidhamu ya mchezo ili kupata
matokeo mazuri.
“Kwasababu ni mechi ya ugenini, mwalimu aweke
mkazo sana sehemu ya ulinzi. Lakini ushambuliaji pia ni muhimu kwasababu
tunahitaji kushinda”. Alisema Nsajigwa.
“Mabeki wanaonekana kuzoeana kiasi, najua ni
changamoto kwasababu mwalimu naye ni mgeni. Kila mchezaji awe na juhudi binafsi
kwasababu mchezo utakuwa na presha kubwa”.
“Tuna goli moja, tunahitaji kulilinda. Nadhani
wachezaji na mwalimu wao wanajua hilo”. Alisema Nsajigwa.
Beki huyo wa kulia wa zamani wa Taifa stars aliyekuwa miongoni mwa walinzi
waliokuwa wanaunda ngome bora ya Mbrazil Marcio Maximo na Jan Poulsen kwa
nyakati tofauti aliongeza kuwa enzi zao walicheza kwa mafanikio sehemu ya
ulinzi kwasababu walikaa kwa pamoja kwa muda mrefu.
“Kipindi chetu tulicheza pamoja kwa muda mrefu. Tulizoeana sana na ndio
maana tulikuwa hatufungwi. Pia tulikuwa na jitihada binafsi za kuisaidia timu”.
“Tulikuwa tunaelewana kwa kufuata mfumo wa
mwalimu. Maximo alikuwa anatufundisha kulinda zaidi hasa mechi za ugenini.”
“ Stars ya sasa kuna mabadiliko ya mara kwa mara
kwa wachezaji”. Alisema Nsajigwa.
Akizungumzia nafasi ya Stars kufuzu hatua ya
makundi, Nsajigwa alisema bado safari ni ndefu na kama ikitokea tukafuzu basi
itakuwa ni bahati.
Aidha, alisema ugeni wa mwalimu itaigharimu Stars
kwa sasa, lakini ni muhimu kuanzia kwa kocha huyu ili timu iwe ya kudumu.
“Wachezaji wa timu ya taifa wanatakiwa kuondoka
taratibu taratibu na sio kubadilishwa ghafla”.
‘Wawaache wazoeane. Wapewe muda. Wacheze mechi
nyingi za kirafiki ili kuzoeana. Mara huyo kaingia mara katoka, hii haina tija
kwa taifa”. Alifafanua Nsajigwa.
0 comments:
Post a Comment