![]() |
Uganda The Cranes wana kibarua cha kufuta kipigo cha mabao 2-1 katika mechi ya kwanza |
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Mei 31, 2014, saa 5: 02 asubuhi
MATAIFA mbalimbali barani
Afrika leo yanashuka dimbani kusaka nafasi ya kupangwa katika hatua ya makundi
kuwania kufuzu fainali za kombe la mataifa ya Afrika, AFCON 2015 nchini
Morocco.
Jana mechi mbili zilipigwa
ambapo Kenya walilazimisha sare ya bao 1-1 ugenini dhidi ya Comoros na
kufanikiwa kusonga mbele kutokana na ushindi wa bao 1-0 walioupata mjini
Nairobi.
Sudan kusini waliofungwa
mabao 5-0 na Msumbiji mjini Maputo, jana waliwakaribisha wapinzani wao nyumbani
na kutoka suluhu ya bila kufungana.
Kwa matokeo hayo, Msumbiji
wamesonga mbele na wanasubiri mshindi wa mechi ya Taifa stars na Zimbabwe ili
kuumana naye katika hatua ya mwisho kuwania kupangwa hatua ya makundi.
Mechi nyingine zinatarajia
kuendelea leo katika nchi mbalimbali barani Afrika.
Timu ya Taifa ya Rwanda
iliyotoka suluhu ya bila kufungana nyumbani mjini Kigali dhidi ya Libya, leo
wanacheza mechi ya marudiano ugenini mjini
Tripoli na wenyeji wao.
Uganda The Cranes
wanawakaribisha Madagascar mjini Kampala. Mechi ya kwanza Uganda walifungwa
mabao 2-1.
Guinea Bissau wanachuana na
Jamhuri ya Afrika ya Kati. Mechi ya kwanza timu hizo zilitoka suluhu pacha ya
bila kufungana.
Sierra Leone wakiwa na kumbukumbu ya kutoka sare ya bao 1-1 ugenini ,
wanaikaribisha katika mechi ya marudiano, Jamhuri ya Swaziland.
Mechi nyingine zitapigwa
kesho juni 1 ambapo timu taifa ya Tanzania, Taifa stars itakabiliana na wenyeji
wao, Zimbabwe, mjini Harare.

Taifa Stars walioripotiwa
kufanyiwa hujuma hapo jana kwa kufungiwa Hoteli wanayoishi mjini Harare,
wanahitaji sare ya aina yoyote au ushindi ili kusonga mbele. Hii inatokana na
ushindi wa bao 1-0 walioupata uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Lesotho waliofungwa bao 1-0
ugenini, watawakaribisha wapinzani wao Liberia katika mechi ya marudiano.
Nao Botswana waliotoka
suluhu mjini Bujumbura, kesho watawakaribisha Burundi nyumbani kwao.
Congo yenye kumbukumbu ya
kuchapwa bao 1-0 na Namibia, kesho itakuwa nyumbani kulipa kisasi.
Katika mechi nyingine,
Benin waliotoka suluhu mechi ya kwanza, watakuwa nyumbani kuvaana na Sao Tome.
Chadi waliofungwa mabao 2-0
na Malawi, kesho watakuwa kwenye kibarua kigumu nyumbani kuhitaji kufuta
matokoe hayo.
Guinea ya Ikweta
iliyofungwa bao 1-0 ugenini, kesho itahitaji ushindi nyumbani katika mechi ya
marudiano na Mauritania.
0 comments:
Post a Comment