
Na Baraka Mbolembole
REJEA kutoka katika makala niliyoandika wiki
iliyopita ambayo ilikuwa na kichwa cha habari; ‘ NAFASI YA MAKAMU WA RAIS SIMBA
SC HAINA MTU SAHIHI’. Mmoja wa wagombea wanaowania kiti hicho katika uchaguzi
ujao wa klabu ya Simba Geofrey Nyange Kaburu, juzi alitoa ufafanuzi kuhusiana
na yale ambayo nilikuwa nimeandika dhidi yake. Katika makala hiyo niliandika
kuwa, Kaburu anarudi Simba kufanya nini wakati nyuma yake ni mmoja wa viongozi
ambao wachezaji wengi walikuwa wakimlaumu kwa kutowathamini, kuwajali nap
engine kushindwa kuwalipa pesa zao.
Sehemu ya makala ile niliandika kwamba; ‘Kwa, mfano, mimi ningewaambia, Itangare na
Kaburu wakajifunze kwanza jinsi ya kuunganisha mahusiano ya kiutawala kati ya
kiongozi wa chini na yule wa nafasi ya juu. Wote hawa walishindwa kwenda
sambamba na mwenyekiti anayemaliza muda wake, Mh. Aden Rage. Nakumbuka kuna
wachezaji wengi waliwahi kuniambia kuhusu kutothaminiwa, kunyanyaswa katika
malipo, na kudharauliwa na makamu huyo mwenyekiti wa zamani aliyejiuzulu katika
utawala unaomaliza muda wake’
Akizungumza kwa utulivu na kujiamini, makamu huyo
mwenyekiti wa zamani aliyejiuluzu baada ya kuitumikia klabu hiyo kwa miaka
isiyozidi miwili, amefunguka mengi. Ni kwanini aliamua kujiuzulu katika nafasi
hiyo huku akitumia muda mwingi kuwazungumzia wachezaji wa klabu hiyo katika
mambo mbalimbali ambayo wa,ekuwa wakilalamikia nje ya klabu.
KABURU; Siwagawi wachezaji, umeniandika kwa nia ya
kunichafua. Hukuwahi kuniuliza kwa nini nilijiuzulu katika nafasi yangu ndani
ya Simba. Nimeongoza pale kwa miaka miwili tena kwa mafanikio makubwa. Makala
yako haikunitendea haki hasa mimi. Kwa sababu umesema kuwa uliongea na
wachezaji na wamekuambi vitu fulani. Ndiyo, inawezekana ni kweli hayo
wanayokuwa wakisema, au yasiwe mambo ya kweli, ama pengine inawezekana ikawa ni
katika utaratibu wa klabu. Ungepaswa kuniuliza kwanza kabla ya kuandika ili
kuwe na mizani katika makala yako, ila hukufanya hivyo. Umeandika kwa nia ya
kunichafua hasa kipindi hiki kuelekea uchaguzi mkuu wa klabu.
SWALI; Kama
kuna kitu kibaya nimekiandika, naomba samahani, ila huo ndiyo ukweli kutoka kwa
wachezaji wenu. Si mchezaji mmoja anayelalamika kuhusu hayo, watu wanne hadi
watano nafikiri wanatosha kunipatia hali halisi.
KABURU;
Inawezekana wakati mimi nikiwa kiongozi kuna mchezaji akawa anadai, ila hapa
ieleweke kuwa hakuwa anamdai, Kaburu, anaidai klabu. Mchezaji anaweza kuwa na mikataba yake lakini akishindwa
kuendana na mahitaji ya Mwalimu hivyo hapo ni lazima ufanye mabadiliko. Kama,
Mwalimu anakuambia ' fulani simuhitaji'. Kama viongozi ni kuchukua uamua wa
kumuondoa na kuleta mwingine ambayo anahitajika.
Tuna muandalia utaratibu wa kumlipa, na anaweza
kulipwa wakati huo kidogo au akaambiwa atalipwa nyingine baadae. Mfano,
wachezaji wengi wa Simba ukisoma mikataba yao inasema kabisa, labda mchezaji
anasajiliwa kwa millioni kumi, hupewa millioni tano wakati akisaini na katika
mwaka wa pili anapewa tena millioni tano. Kwa hiyo mtu anaweza kusema anadai pesa ila kuna vitu
vingi katikati mchezaji akawa havijui vizuri, au anaongea kwa nia tofauti.
SWALI, Je hakuna hali hiyo?
KABURU; Uongozi ni ' jalala', mimi wakati naingia
pale kweli nilikuta utaratibu wa wachezaji kulipwa pesa mkononi. Niliondoa hali
hiyo na hadi sasa wachezaji wanalipwa moja kwa moja kwa kuingiziwa pesa katika
akaunti zao.
SWALI, Pesa ya mishahara inatoka wapi na nani
anayehusika na kuwalipa wachezaji?
KABURU;
Pesa ya mishahara inatoka kwa mdhamini, na anayefanya kazi hiyo ni Mtendaji
mkuu wa klabu.
SWALI; Kwa nini baadhi ya wachezaji wanakunyoshea
wewe vidole vya lawama?
KABURU;
Hakuna mchezaji aliyotoka chini ambaye sikumsaidia, ila msaada wangu wote
unakuwa na maana mchezaji anatakiwa naye kuisaidia klabu. Kama mchezaji
anasaidiwa naye hatoi msaada kwa klabu utafanya nini? Mwalimu akisema fulani
simuhitaji, mimi nifanyaje?.Ripoti ya Mwalimu inakuja katika kamati ya
utendaji, maamuzi yakifanyika baada ya kuijadili tunakuwa wazi, mchezaji husika
anaambiwa wazi kuwa ameshindwa kufikia malengo ya Mwalimu.
Mfano,
ripoti ya Z. Logarusic inaoneshawachezaji wengi wanatakiwa kuvunjiwa mikataba
yao kwa sababu hawajafikia malengo. Si
mchezaji mmoja au wawili ni wengi. Hii ni inshu' serious', itabidi wengine
tuwapunguze kwa kuwapeleka kwa mikopo katika timu nyingine kwa kuwa hatuwezi
kuvunja mikataba ya wachezaji wote. Uamuzi huo unapofika kwa mchezaji anaona
anawekewa zengwe na Kaburu. Mpira ni ugaidi. Unamfahamu vizuri, Ferguson ( Sir
Alex)?. Hacheki na mtu anapoamua kufanya mabadiliko, ni mtu mwenye roho mbaya.
Kwenye soka kila mtu anatakiwa kufanya kazi yake ipasavyo, ndiyo utaratibu
uliopo kila mahali.
Kwa vile mchezaji hajui atalalamika. Tazama,
mchezaji gani ambaye Mwalimu, Loga hakumpatia nafasi?. Wote amewapatia nafasi
ila wameshindwa. Leo hii, ukiwaambia wachezaji kama, Mwombeki ( Betram), Pazzi
( Zahoro) au Christophe ( Edward) waende mahali kwa mkopo ili wapate nafasi ya
kucheza watakataa, ila ni nafasi nzuri ya wao kujiimarisha kimpira. Hawa ni
mfano tu, lakini wapo wengi ambao ukichukua maamuzi kama hayo wanajenga chuki
na kuona wanaonewa au hawatendewi haki.
SWALI; Kumekuwa na madai kuwa viongozi kuwajali
zaidi wachezaji fulani wanaotajwa ni nyota katika timu na kuwapuuza wale
wengine ambao ukitazama kwa umakini utaona mchago wao pia ni mkubwa. Wewe ni
mmoja wa viongozi ambao wanalalamikiwa sana kuhusu hilo, unasemaje?
KABURU;
Nataka nikupe mfano mmoja, Emmanuel Okwi, ni watu wangapi ambao walikuwa
wakimzunguka mara baada ya kumalizika kwa mchezo?. Ni wengi, je, ni kwanini
wamfuate yeye?. Kiwango chake cha uwanjani kinawavutia wengi hivyo wengine
wanaamua kumpa asante kwa kazi yake nzuri, hivyo mchezaji mwingine akiona hivyo
roho inamuuma. Ukimwambia naye afanye jitahada mazoezi ili awe bora zaidi
hataki.
Wewe ndiye ungekuwa kiongozi utafanya nini?.
Kwenye mpira kila mchezaji atakula kutokana na urefu wa kamba yake, ili ni
lazima Watanzania walijue. Mwanzo kila mchezaji alikuwa akipewa kiasi sawa na
mwenzake katika kila mgao, lakini, Mwalimu
akasema, hapana mchezaji atakaye fanya vizuri apewe kiasi cha juu zaidi
na yule ambaye atashindwa apewe kidogo ama huenda asipewe kabisa. Anayefanya
kazi zaidi, ndiye atakayekula zaidi.
SWALI; Kwa nini ulijiuzulu katika nafasi yako ya
umakamu mwenyekiti?.
KABURU; Nilijiuzulu Simba kwa sababu nyingi,
lakini kubwa ni suala la katiba. Nilijiuzulu kwa kuwa sikufurahishwa na jinsi
ambavyo sisi kama uongozi tulivyokuwa na mtazamo tofauti kuhusu mambo ya
usajili wa wachezaji. Niliwaambia wenzangu mpango wa kuwaondoa wachezaji wote
wakongwe haukuwa sahihi.
Wao walitaka tuwapandishe vijana wote wa timu B,
ili kuchukua nafasi za wachezaji wazoefu. Nilikataa kuhusu hilo na nikasisitiza
kuwa tutafanya kosa, kwa kuwa timu ilikuwa ikihitaji matokeo zaidi kwa sasa.
Nikapendekeza tuwe tunapandisha kijana mmoja mmoja kila msimu katika kikosi cha
kwanza. Mfano, Shomari Kapombe aliingia moja kwa moja katika kikosi cha kwanza
mwaka juzi, wakafuata kina, Ramadhani Singano, Haruna Chanongo, Jonas Mkude.
Kuwapandisha wote kwa pamoja ilikuwa na maana
ya kujitoa katika ushindani. Mimi ndiye niliyeitengeza timu ya U20, hakuna
kiongozi aliyekuwa na mpango na timu hiyo. Niliamua kumsomesha, Suleimani
Matolaili aweze kunisaidia katika hilo. Nimemsomesha, Singano tangu kitado cha
kwanza hadi cha nne, nimewasaidia vijana wengi, hatukuwa na mishahara lakini
nilikuwa na mawazo kuwa baada ya miaka minne nitagombea uongozi na vijana hao
watanibeba.
SWALI; Kwa nini ulipingana mpango huo wa
kuwapandisha wachezaji vijana?
KABURU;
Lengo letu kubwa ilikuwa ni kusajili wachezaji wazawa, huku tukilenga kuwasaini
vijana wa timu B, ili klabu isiwe na wasiwasi wa kuhujumiwa kwani mara nyingi
wachezaji wa ndani husemwa kuwa wanajihusisha na uuzwaji wa mechi hivyo mpango
wa timu B, ulitakiwa kutazamwa lakini si
haraka vile. Wakati naingia katika uongozi wale vijana walikuwa pamoja kwa
miaka mitatu, na mawazo yangu ilikuwa ni kuwaingiza kikosini mmoja mmoja. Mimi
sikukubaliana na wenzangu timu yote ipandishwe kwa sababu hawakuwa na uzoefu wa
ligi.
Huwezi
kumpandisha mchezaji kinda anayecheza mechi nne kwa mwaka. Nikatoa mawazo kuwa
baadhi yao tuwapeleke kwa mkopo katika timu nyingine ili wapate uzoefu. Kamati
ya utendaji yote ilikataa, lakini wamefeli. Kuuza mchezaji bila kufikiria ni
mchezaji gani utamsajili kama mbadala wake lazima utafeli.
SWALI; Unamaanisha nini?
KABURU; Mimi nilikataa, Okwi asiuzwe. Nakumbuka
nilimwambia ' mwenyekiti usimuuze mchezaji huyo', akalazimisha na wenzake
wakamuuza bila pesa. Kama msaidizi wa mwenyekiti maana yake nigombane na
mwenyekiti ili timu iende katika mgogoro. Kipi bora?.Cha kufanya nikaamua
kujiuzulu.
SWALI; Simba haikufanikiwa sana katika michezo ya
kimataifa, tatizo lilikuwa ni nini?
KABURU; Mtu
aliyetuangusha ni Rage, mwaka juzi tulifika hadi hatua ya 16 bora ya kombe la
Shirikisho. Alienda Sudan bila kuwa na wachezaji muhimu. Nilimwambia ni
lazimatwende kule na plan tofauti akakataa. Akaichukua timu akaenda nayo,
nikamwambia nenda. Hivi katika mchezo wa kimataifa unaweza kwenda uwanjani bila
kuwa na mshambuliaji? Alimuacha, Okwi nyumbani kwa sababu tu ya mchezaji kutaka
mkataba mzuri zaidi baada ya ule wa awali kumalizika. Ilikuwa kosa lake. (
kumbuka Simba il)
SWALIL Nini kinafuata sasa?
Kaburu; Hakuna kiongozi ambaye amefanya mambo
ambayo mimi nimefanya, napenda sana kukosolewa, lakini napokuwa naonewa huwa
sijisikii vizuri kwa sababu nimejitoa sana kwa klabu hii. Nimeingia TFF, katika
kamati ya LIgi ili kuzisadia klabu kuboresha timu zao za vijana ambazo ndiyo
msingi mkubwa. Kuanzia msimu ujao tuna mpango kuwa timu zote za vijana zicheze
katika ligi ya mkoa na zikiweza
zinapanda daraja la pili, hadi la kwanza hazitaruhusiwa kucheza ligi kuu kwa
kuwa huwezi kuzichezesha timu mbili
katika daraja moja. Hivyo ndivyo wanavyofanya, Hispania, Ujerumani na
kwingineko duniani.
Mimi ni mtu wa vitendo, mimi ni mtu wa watu. Tangu
nimeondoka katika uongozi Simba haijashinda taji lolote. Kwa nini> Sababu
kubwa ni kwamba Simba inahitaji pesa kwanza, usajili mzuri, kufanya maandalizi
ya uhakika ya ligi. Timu inaposhinda watu watakuja uwanjani, na klabu itapata
pesa . Kuuza wachezaji ilikuwa ni moja kati ya mipango yangu. Kwamba kila mwaka
tunauza mchezaji mmoja na kutumia pesa hiyo kusajili wachezaji wengine, watatu
hadi wanne wenye uwezo pia .Kwa nini? Ili timu ipate pesa na iweze kujiendesha.
Sijisifii, ila nilikuwa na maarifa , Kwanza, nilikuwa nikiwasaini wachezaji
wazuri na kutengeneza timu bora kwa kufuata maagizo ya Mwalimu.
SWALI; Umejifunza wapi?
KABURU; Mwaka 2005 nilikwenda na Simba nchini
Nigeria wakati tukienda kucheza na timu ya Enyimba, nilipofika kule nilikutana na rais wa timu hiyo naye
akaniambia kuwa ‘ hatua wachezaji’ kwa maana kuwa wachezaji wetu hawakuwa
wameandaliwa katika misingi ya uchezaji. Akanielekeza jinsi ya kuandaa timu,
nan i huko ndipo nilikopatia wazo la kuja kuanzisha timu B ya Simba. Nakumbuka
nilijenga mahusiano mazuri na rais wa Enyimba na kuna wakati akatupatia bure
wachezaji Emeh Ezechukwu na Orgi Obinna. Nimetembea, Ujerumani, Hispania,
Ufaransa nan chi nyingine za Ulaya na Afrika kote huko nilienda kwa nia ya
kujifunza kuhusu uendeshaji wa mambo ya mpira.
Nashukuru, sana kiongozi kwa kutoa ufafanuzi mzuri
kuhusu hoja yangu.
KABURU; Asante pia, ila wakati mwingine ni lazima
utafute wahusika kwanza na kuandika. Sina tatizo na wewe ila makala yako
ilikuwa na lengo la kunichafua .
0714 08 43 08
0 comments:
Post a Comment