
Katibu mkuu wa CECAFA, Nicholas Musonye akizungumza katika
moja ya semina ya FIFA iliyofanyika jijini Dar es salaam hivi karibuni.
Na Baraka Mpenja, Dar es
salaam
Imechapishwa Mei 27, 2014, saa 2: 17 asubuhi
BARAZA la vyama vya soka ukanda wa Afrika mashariki na kati,
CECAFA limeungana na nchi ya Somalia kuomboleza
kifo cha mtoto mmoja mcheza mpira na wengine wawili kujeruhiwa kutokana na mlipuko wa bomu lililotegwa
katika uwanja wa wazi mjini Balanbale karibu na mpaka wa Ethiopia.
Mwa mujibu wa taarifa iliyotumwa katika mtandao huu na Afisa
habari wa chama cha soka nchini Somalia, Shafi’i Mohyaddin Abokar imesema ili kuungana
na Somalia katika kipindi hiki kigumu baada ya tukio hilo la kuhuzunisha,
katibu mkuu wa CECAFA Nicholas Musonye ametuma salamu za rambirambi kwa katibu
mkuu wa chama cha soka nchini Somalia Abdi Qani Said na kutoa pole kwa taifa hilo changa katika
maendeleo ya soka.
“Nimesoma habari za
kuhuzunisha juu ya kifo cha mchezaji kijana na wawili kujeruhiwa wakati
wakicheza mpira nchini Somalia. Naungana na wewe na familia ya mtoto
aliyefariki katika kipindi hiki cha huzuni”. Alisema katibu wa CECAFA katika
barua yake ya salamu za rambirambi kwa katibu mkuu wa chama cha Somalia jana
jioni.
Bwana Musonye alisema
CECAFA siku zote inaamini kuwa ipo siku itatokea Somalia yenye utulivu ambapo
maendeleo ya mpira yatapatikana na wachezaji wake watajitangaza kimataifa.
“Tunaamini wachezaji
wawili waliojeruhiwa wataendelea vizuri na tunawaomba wazazi wawe wavumilivu wakati huu wa huzuni” . Musonye
aliendelea katika barua yake ya Salamu za rambirambi.
0 comments:
Post a Comment