Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
YANGA SC wanatarajia kukabiliana na maafande wa JKT
Ruvu katika muendelezo wa michezo ya ligi kuu soka Tanzania bara kwenye uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam kuanzia majira ya saa 10:00 jioni.
Viingilio katika mechi hiyo ni kama ifautavyo; VPA Tshs 20,000/=,
VIP B na C ni Tshs 15,000/=, huku
viti vya rangi ya Chungwa, Bluu na Kijani
ni Tshs 5,000/=
Hii ni mechi muhimu kwa Yanga kwani kushinda
kutawafanya waendeleze uhakika wa kutetea ubingwa wao msimu huu.
Mpaka sasa Yanga wao nafasi ya pili kwa pointi 46
baada ya kushuka dimbani mara 22.
Mbele yao wapo Azam fc wenye pointi 53, huku wakiwa wameitangulia
Yanga kwa mchezo mmoja.
Yanga wanaingia uwanjani wakiwa na machungu ya
kufungwa mabao 2-1 mechi iliyopita dhidi
ya Mgambo JKT katika uwanja wa Mkwakwani Jijini Tanga.
JKT Ruvu wapo nafasi ya 9 baada ya kucheza mechi 23
na kujikusanyia pointi 28 kibindoni.
Kama watashinda leo watazidi kujiweka mazingira
mazuri zaidi ya kubakika ligi kuu.
Hivyo kocha mkuu wa klabu hiyo, Fredy Felix Minziro
ataingia kwa lengo moja la kuifunga Yanga ambayo ameifundisha kwa muda mrefu
akiwa kocha msaidizi na wakati fulani kukaimu nafasi ya kocha mkuu .
Mchezo wa leo unaweza kuwa na changamoto kubwa kwa
timu zote, lakini timu itakayokuwa na mipango mizuri itaweza kushinda.
Kocha mkuu wa Yanga, Mhalonzi, Hans Van Der Pluijm
anaweza kuwaanzisha mlinda mlango Deogratius Munish `Dida`kwasababu yuko fiti baada
ya kupona majeraha yake yaliyokuwa yanamsumbua kwa takribani wiki tatu.
Beki ya kulia anaweza kuanza Juma Abdul, kushoto,
Oscar Joshua.
Mabeki wa kati bila shaka watasimama, Mbuyu Twite na
`Nadir Haroub Canavaro`.
Twite anaweza kulazimika kucheza beki ya kati kwasababu Kelvin Yondani anatumia kadi mbili za njano.
Frank Domayo `Chumvi` anaweza kuanzishwa nafasi ya
kiungo wa ulinzi, huku Saimon Msuva akianza winga ya kulia.
Kiungo namba nane anaweza kusimama kinda, Hassan
Dilunga, huku namba tisa akianza Didier Kavumbagu.
Kiungo mshambuliaji anaweza kuanza Hamisi Kiiza, wakati
winga wa kushoto leo hii anaweza kusimama Mrisho Halfan Ngasa.
Pluijm leo hii atakosa huduma ya Athuman Idd
`Chuji`, Haruna Niyonzima, Emmanuel Okwi na Kelvin Yondani wenye matatizo
tofauti.
Kikosi kilichotajwa hapo juu si rasmi, bali ni
utabiri tu kulingana na umuhimu wa mechi yenyewe na wachezaji waliopo tayari
kucheza kipute hiki.
Lakini kuna wachezaji wengi wanaoweza kuanzishwa
wakiwemo akina Jerryson Tegete na Hussein Javu kwa safu ya ushambuliaji.
Maeneo mengine pia wapo wachezaji wengine wanaoweza
kuanza kutegemeana na uchaguzi wa kocha mkuu, Hans Van Der Pluijm, kwasababu
wote wana uwezo mzuri.
Mechi nyingine za jioni ya leo ni kati ya Coastal
Union dhidi ya Mgambo uwanja wa Mkwakwani jijini Tanga.
Vibonde JKT Oljoro watakuwa na kibarua muhimu na
maafande wa jeshi la Magereza kutoka jijini Mbeya, Tanzania Prisons
`Wajelajela` katika dimba la Shk. Amri Kaluta Abeid jijini Arusha.
Rhino Ranger waliopoteza matumaini ya kubakia ligi
kuu watawakaribisha, Mtibwa Sugar kutoka Marogoro kwenye uwanja wa Ali Hassan
Mwinyi mjini Tabora.
Mechi ya Ruvu Shooting na Azam iliyotakiwa kupigwa
leo imesogezwa mbele mpaka aprili 9 mwaka huu kwasababu wachezaji wengi wa Azam
fc wameondoka na kikosi cha timu ya Taifa ya vijana chini ya miaka 20,
Ngorongoro Heroes.
0 comments:
Post a Comment