Na Baraka Mpenja, Dar Es Salaam
0712461976
SIMBA SC watakabiliana na Yanga katika mechi ya
kufunga pazia la ligi kuu soka Tanzania bara jumamosi ya wiki hii kwenye uwanja
wa Taifa jijini Dar es salaam.
Timu hizi zitakutana zikiwa na mafanikio tofauti
msimu huu ambapo Yanga wameambulia nafasi ya pili, huku Mnyama akijikongoja
katika nafasi ya nne.
Simba na Yanga zinapokutana katika mechi za ligi
au mashindano mengine, wachezaji, mabenchi ya ufundi, viongozi na mashabiki wa
klabu hizi kongwe nchini wanakuwa katika presha kubwa.
Unapozungumzia historia ya soka la Tanzania, ni
dhambi kubwa kutozitaji klabu hizi mbili zenye mashabiki kila kona ya nchi hii.
Mengi yanatokea kila mechi zao zinapokaribia.
Wachezaji mara nyingi wanasakiziwa kuuza mechi pale timu moja inapofungwa.
Wakati mwingine inasemekana viongozi wa timu hizi
huenda kwa waganga wa kienyeji kwenda kuroga timu pinzani.
Suala la ushirikiana linazungumzwa sana katika
klabu hizi, lakini ni jambo gumu kulithibitisha kisayansi kama kweli linafanya
kazi.
Simba na Yanga zinakutana jumamosi, huku Yanga
wakiwazidi wenzao kwa kila kitu.
Yanga wamecheza mechi 25 sawa na Simba sc, lakini
wameweza kushinda mechi 16, kutoa sare 7 na kufungwa mechi 2 tu, hivyo
kufikisha pointi 55 katika nafasi ya pili.
Pia Yanga ndio klabu iliyofunga mabao mengi zaidi
mpaka sasa ambapo imetikisa nyavu za timu pinzani mara 60, lakini wamefungwa
mabao 18 na kuwa timu ya pili kufungwa mabao machache.
Mabingwa watetezi Azam fc wamefunga mabao 50 na
kufungwa mabao 15 tu, hivyo kuwa timu yenye rekodi ya kufungwa mabao machache
zaidi msimu huu.
Ukirejea kwa upande wa Simba sc, msimu huu upepo
mbaya umevuma kwa upande wao kwasababu mpaka sasa wamecheza mechi 25 na
kushinda mechi 9, sare 10 na kufungwa mechi 6.
Pia Mnyama Simba amefanikiwa kufunga mabao 40 na kuruhusu nyavu zake kuguswa mara 26.
Kwa takwimu hizi utagundua kuwa Yanga wamekuwa
bora kwa kila kitu dhidi ya Simba sc.
Safu ya Ulinzi ya Yanga inayoongozwa na Mbuyu
Twite, Oscar Joshua, Nadri Haroub Canavaro, Kelvin Yondani na wengineo imekuwa
bora zaidi ya Simba inayoongozwa akina William Lucian ‘Gallas’, Issa Rashid
‘Baba Ubaya’ Joseph Owino, Donald Mosoti, Nassor Masoud ‘Chollo’ na wengineo.
Kigezo cha pekee ni idadi ya mabao ambayo mabeki
wa timu zote wameruhusu kutikisa nyavu.
Yanga wamefungwa mara 15 na Simba mara 26, hivyo
Yanga wamekuwa na beki imara zaidi ya watani zao.
Ukija safu ya ushambuliaji baina ya timu hizi,
kuna utofauti mkubwa.
Yanga wamekuwa na makali zaidi baada ya kufunga
mabao 60 mpaka sasa dhidi ya mabao 40 ya Simba sc.
Safu ya ushambuliaji ya Yanga haimtegemei mchezaji
mmoja kwasababu wote Saimon Msuva, Mrisho Ngassa, Didier Kavumbagu, Jeryson
Tegete, Hussein Javu, Emmanuel Okwi na Hamis Kiiza wanaweza kufunga pale
wanapopewa nafasi ya kucheza.
Washambuliaji wa Yanga ndio wanaoongoza kufunga
mabao mengi zaidi na kuweka rekodi ya kufunga mabao mengi kuliko klabu yoyote
katika mechi moja msimu huu.
Rekodi hii waliweka baada ya kuwafunga mabao 7-0
Ruvu Shooting ndani ya uwanja wa Taifa.
Ukija upande wa Simba, mabao mengi yametengenezwa
kupitia kwa nyota wao, Mrundi Amis Tambwe, japokuwa kuna wachezaji wengine kama
akina Zahor Pazzi, Ramadhani Singano, Haruna Chanongo ambao wamekuwa wakifunga
mara kadhaa.
Hata rekodi ya kushinda na kufungwa, Yanga
wanawazidi Simba kwasasa wamefungwa mechi mbili tu wakati Simba wamechezea
kichapo mara sita.
Kwa kuangalia takwimu hizi, unaweza kusema Yanga
wana uwezo mkubwa wa kuwafunga Simba sc jumamosi, lakini mechi ya watani wa
jadi ni kitu kingine.
Mzunguko wa kwanza, Yanga walikuwa bora zaidi ya
Simba iliyosheheni wachezaji wengi vijana chini ya aliyekuwa kocha mkuu Abdallah
Kibadeni `King Mputa`.
Kipindi cha kwanza Yanga walifunga mabao 3-0 na
kujiamini kuwa wangeweka rekodi ya kuwafunga mabao mengi Simba na kulipa kisasi
cha kuwahi kufungwa mabao 5-0.
Hata hivyo mambo yalikuwa tofauti kipindi cha pili
ambapo Simba walikuja juu na kusawazisha mabao yote matatu na kutoa sare ya
3-3.
Haya yalikuwa moja ya matokeo ya ajabu baina ya
klabu hizi.
Baada ya mechi hiyo, timu hizi zilikutana tena desemba mwaka jana
kwenye mechi ya `Nani Mtani Jembe` na kushuhudia Yanga iliyokuwa bora ikifungwa
mabao 3-1.
Matokeo hayo yaliondoka na kocha mkuu Ernie
Brandts na msaidizi wake Fredy Minziro waliofungashiwa virago.
Kuelekea katika mechi ya jumamosi, bado Yanga
wanaonekana kuwa bora zaidi ya Simba.
Lakini Simba wameenda kuweka kambi Zanzibar na
bila shaka watarejea na nguvu ya kuwavaa watani zao wa jadi.
Mpira wa miguu huwa ni mchezo wa hesabu, ukikosea
kuzifanya basi unafungwa.
Ni kawaida kuona timu bora inafungwa na timu ya
kawaida kama ilivyotokea kwa Yanga na Mgambo au Simba na Ashanti United.
Ukiangalia vikosi vya timu zote mbili, Yanga wana
wachezaji wakali kuliko Simba, lakini si sababu ya kusema watashinda mechi.
Simba uliowaona katika mchezo uliopita na Ashanti
si wale utakaowaona siku ya jumamosi.
Bila shaka wataingia kwa morali kubwa ya kutaka
kushinda, na viongozi wao wamewataka wachezaji kuwafunga mahasimu wao ili
kujipunguzia maumivu.
Usije kushangaa yanatokea matokeo ambayo watu wengi
hawatarajii.
Mechi ya watani ina mambo mengi na si rahisi
kutabiri kwa kuangalia vikosi vya vyao.
Usije ukaliwa nyumba yako, Mke wako, pesa zako kwa
kuweka mzigo mezani na kutabiri matokea.
Usilete mchezo na mechi ya watani wa jadi, huwa
timu zinacheza kwa kujituma mno.
Kila la kheri Simba na Yanga katika mechi yenu ya
jumamosi.


0 comments:
Post a Comment