Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
MATOKEO ya 0-0 waliyoyapata Mbeya City leo hii
kwenye mchezo mgumu wa ligi kuu soka Tanzania bara dhidi ya Ashanti United
katika uwanja wa Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es salaam
yamewagharimu na kuwakosha rasmi ubingwa msimu huu.
Ashanti United waliokuwa na lengo la kupata ushindi
leo hii mbele ya Mbeya City wameambulia pointi moja muhimu kuliko kupoteza
mchezo huo.
City wamefikisha pointi 46 katika nafasi ya tatu
sawa na Yanga waliopo nafasi ya pili kwa pointi 46, lakini kikosi cha Pluijm
kina wastani mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Hii ilikuwa mechi ya 24 kwa Mbeya City, hivyo wamebakiza
mechi mbili nyumbani dhidi ya Azam fc na
Mgambo JKT.
Kama watashinda mechi zote watafikisha pointi 52
ambazo tayari Azam wameshafikisha kileleni.
Kwa maana hiyo, Mbeya City rasmi wamejitoa kuwania
ubingwa na kuwaacha wanaume wawili, Yanga sc na Azam fc kuendelea na vita hiyo.
Kilichobaki kwao ni kuisaka nafasi ya pili, kwani
wanaweza kuipata kutegemeana na matokeo watakayopata Yanga SC.
Yanga wamebakiza mechi nne kuanzia ya kesho dhidi ya
JKT Ruvu ndani ya dimba la Taifa jijini Dar es salaam.
Kama Mbeya City wanataka kuchukua nafasi ya pili wanatakiwa kuwaombea
Yanga mabaya ili wapoteze mchezo mmoja, washinde mmoja na kutoa sare miwili.
Kikosi cha Kager Sugar leo. Picha na www.bukobasports.com
Kama matokeo hayo yatatokea, maana yake Yanga
atavuna pointi tano pekee na ukijumlisha na pointi 46 walizonazo sasa
watafikisha pointi 5I ambazo Mbeya City atazivuka endapo atashinda mechi zote.
Yanga ataanza kazi kesho dhidi ya JKT Ruvu, baada ya
hapo atavaana na Kagera Sugar mechi ya kiporo aprili 9, na hatimaye atasafiri
kwenda Arusha aprili 13 kuwavaa JKT Oljoro na kurejea Dar es salaam kufunga
msimu dhidi ya Simba uwanja wa Taifa aprili 19 mwaka huu.
Kwa mechi alizosaliwa nazo Yanga si rahisi kutabiri
matokeo, lolote linaweza kutokeo, lakini kwa Mbeya City biashara imewakata
kwasababu mambo ya kusubiri mwenzako apoteze inaweza kutokea au isitokee.
Hata hivo mtandao huu umezungumza na kocha msaidizi
wa Mbeya City, Maka Mwalwisyi ambaye amekiri wazi kuwa mchezo wa leo ulikuwa
mgumu sana kwa upande wao.
‘Tunamshukuru Mungu mechi imeisha salama na
tumeambulia suluhu. Ni matokeo mabaya kwetu, lakini huwezi jua waliopo juu yetu
watapata matokeo ya aina gani huko mbeleni. Kimsingi yametuharibia sana, lakini
hatukati tamaa kupambana mpaka dakika ya mwisho”.
“Hata kama itakuwa tofauti na malengo yetu sio
mbaya. Huu ni msimu wetu wa kwanza. Tumejitahidi kadri ya uwezo wetu na haya
ndio mavuno yetu. Tunarudi kujiandaa na mchezo ujao dhidi ya Azam fc”. Alisema
Kocha Maka.
Kocha wa Ashanti United, Abdallah Kibadeni
aliwahofia Mbeya City kwasababu ya ubora wao, lakini amemaliza mechi kwa kupata
pointi moja muhimu.
Kwa matokeo hayo, Ashanti wanafikisha pointi 22
katika nafasi ya 12 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Mchezo ujao watashuka dimbani kukabiliana na Simba
uwanja wa Taifa na watahitimisha kibarua chao msimu huu dhidi ya Tanzania
Prisons uwanja wa sokoine jijini Mbeya.
Kama Ashanti United watashinda michezo hiyo mitatu
watafikisha pointi 31 na pengine kujiweka mazingira mazuri ya kubakia ligi kuu.
Kikosi cha Simba kilichoanza leo. Picha na www.bukobasports.com
Wakati huo huo Mgambo JKT wapo nafasi ya 11kwa
pointi 22 kama Ashanti, na wamebakiwa na michezo mitatu.
Kama Mgambo watashinda mechi zijazo dhidi ya Coastal
Union, Kagera Sugar na Mbeya City watafikisha pointi 31 kama Ashanti, na hapo
timu moja italazimika kushuka kwa kuangalia tofauti ya mabao ya kufunga na
kufungwa.
Rhino wapo mkiani kwa pointi 13 na wamebakiza mechi
tatu. Kama watashinda zote watafikisha pointi 22 ambazo zimefikiwa na Ashanti,
Tanzania Prisons na Mgambo, huku timu hizi zikiwa na mechi tatu mkononi.
Oljoro JKT wapo nafasi ya 13 kwa pointi 15 na wakishinda
mechi zao tatu zilizosalia watafikisha pointi 24 ambazo zinaweza kupitwa na
Ashanti United, Prisons na Mgambo JKT.
Hivyo kwa mazingira haya, Rhino Rangers na JKT
Oljoro zina asilimia kubwa ya kushuka daraja, huku Ashanti, Mgambo na Prisons
zikipambana kwa nguvu kukwepa kuungana na timu hizi mbili za mwisho.
Mchezo mwingine umepigwa katika dimba la Kaitaba ambapo
wenyeji wa uwanja huo wamewakaribisha wekundu wa Msimbazi Simba sc.
Mechi hiyo imemalizika kwa sare ya bao 1-1.
Simba walikuwa wa kwanza kuandika bao la kuongoza
katika dakika ya 45 kipindi cha kwanza kupitia kwa Zahor Idd Pazzi akipokea krosi kutoka
kwa nahodha wao, Nassor Masoud Cholo.
Kagera walisawazisha
bao hilo dakika ya 51 kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji wao hatari,
Them Felix `Mnyama`.
Kwa matokeo hayo, Simba sc wamefikisha pointi 37
katika nafasi ya 4 baada ya kushuka dimbani mara 24.
Kagera Sugar wamefikisha pointi 34 katika nafasi ya
5 baada ya kushuka dimbani mara 23.
Mechi ya Kaitaba haikuwa na ushindani mkubwa kwani
timu zote hazikuwa na cha kupoteza, kwa maana ya kutotafuta ubingwa wala nafasi
ya pili.
Timu zote zilikuwa zinashambuliana kwa zamu, lakini
Kagera Sugar walipata nafasi nyingi zaidi ya Simba.
Hata hivyo ubutu wa safu za ushambuliaji kwa timu
zote ,kumeamuru matokeo yawe 1-1 mpaka dakika 90 zinamalizika.
Ligi hiyo itaendelea kesho kwa mechi kadhaa kupigwa
katika miji tafouti.
Jijini Dar es salaam, Yanga watakabiliana na JKT
Ruvu na ushindi ni muhimu kwa timu zote.
JKT Oljoro watawakaribisha maafande wa Tanzania
Prisons katika dimba la Shk. Amri Amri Abeid Kaluta jijini Dar es salaam.
Rhino Rangers watakuwa dimba la Ali Hassan Mwinyi
kuumana na Mtibwa Sugar kutoka Morogoro.
Nao wagosi wa Kaya watawakaribisha ndugu zao, Mgambo
JKT katika dimba la CCM Mkwakwani, Jijini Tanga.
0 comments:
Post a Comment