Na Baraka Mpenja , Dar es salaam
0712461976 au 0764302956
KUELEKEA katika mechi ya keshokutwa ndani ya dimba
la Taifa, jijini Dar es salaam baina ya mabingwa watetezi wa ligi kuu soka
Tanzania bara, Young Africans dhidi ya makamu bingwa kwa misimu miwili
mfululizo, Azam fc wana Lambalamba mashabiki, viongozi na mabenchi ya ufundi
yamepandwa na homa kali.
Azam fc waliopo kileleni wakiwa na pointi 43 wapo
katika mipango kabambe ya kuhakikisha wanapata ushindi mbele ya Yanga
inayotajwa kuwa na kikosi bora zaidi msimu huu.
Ni kweli Yanga msimu huu imesheheni majina ya
wachezaji wenye mvuto zaidi nje ya uwanja, japokuwa ndani ya uwanja bado kuna
matatizo ndani ya kikosi chao.
Ukitaja majina kama vile Emmanuel Anord Okwi, Hamis Friday
Kiiza `Diego`, Didier Kavumbagu `Kavu`, Mrisho Khalfan Ngasa `Anko`, Simon
Msuva , Said Bahanuzi, Jeryson John Tegete ambao huongoza safu ya ushambuliaji,
hakika utahofia unapoingiza uwanjani kikosi chako cha bei `chee` .
Pia ukija dimba la kati, unakutana na mafundi,
Haruna Niyonzima `Fabregas`, Frank Domayo `Chumvi`, Athuman Idd `Chuji` ,
Hassan Dilunga na wengineo ambao hawana namba za kudumu katika kikosi cha
kwanza.
Nayo safu ya ulinzi imesukwa kwa mabeki visiki
wakiwemo Kelvin Patrick Yondan, Nadir Haroub `Canavaro`, Mbuyu Twite, Oscar Samwel
Joshua, David Luhende na wengineo.
Ukiangalia tofauti ya majina baina ya Yanga na Azam
fc, Wanajangwani ni chama kubwa zaidi kwa maana ya kuwa na mtaji mkubwa wa
wanachama, mashabiki na hata ukongwe wa ligi kuu soka Tanzania bara.
Ukija katika mipango, uwekezaji, hapo unaleta habari
nyingine. Azam fc wameipiga bao Yanga kwa asilimia kubwa.
Wakati mashabiki wakisubiri mechi hiyo kwa hamu
kubwa, tayari kikosi cha Yanga kimeingia chimbo maeneo ya Bagamoyo, Mkoani Pwani kujiwinda na mechi hiyo ya kesho
kutwa.
Taarifa za uhakika kutoka ndani ya Yanga zinasema
kuwa kipa namba moja wa klabu hiyo aliyekosa mchezo wa jumamosi dhidi ya Mtibwa
Sugar ulioishia kwa suluhu ya bila kufungana, Deogratius Munich `Dida` anaweza
kurejea uwanjani kufuatia kuendelea vizuri baada ya kuumia katika mazoezi wiki
iliyopita.
Naye Mrisho Ngasa aliyeumia katika mchezo wa machi 9
mjini Alexndria dhidi ya Al Ahly ambapo
Yanga walitolewa kwa penati 4-3 anaendelea vizuri ingawa bado hakuna uhakika
kama anaweza kutumika mechi ijayo.
Hata kama `Dida` hatakuwepo katika mchezo wa kesho
kutwa, bado nafasi yake itaweza kuzibwa na makipa waliopo, Juma Kaseja na Ally
Mustapha `Bartez`.
Kaseja aliyesajiliwa maalum kwa mechi za kimataifa,
alikosa mechi tatu za ligi ya mabingwa barani Afrika.
Alikosa mechi ya marudiano dhidi ya Komorozine mjini
Moroni, na akakosa mechi mbili dhidi ya Al Ahly.
Lakini jumamosi kwenye mchezo wa Mtibwa Sugar,
Kaseja alitumika na alionesha umahiri langoni, hivyo kama `Dida` hatocheza,
lango la Yanga litakuwa katika mikono salama.
Nao vinara Azam fc wameshaingia kambini katika
Hosteli zao zilizopo Azam Complex, Chamazi, nje kidogo ya jiji la Dar es
salaam.
Ni mandhari nzuri kwao na masikani kwao, hivyo bila
shaka wapo katika mipango madhubuti kuwaliza Yanga kwa mara nyingine tena ligi
kuu soka Tanzania bara.
Yanga wanahitaji ushindi kwa nguvu zote ili
wapunguze pengo la pointi dhidi ya Azam fc.
Mpaka sasa Yanga wapo nafasi ya pili kwa pointi 39
baada ya kucheza mechi 18.
Nyuma yao wapo Mbeya City wenye pointi 39 sawa na
Wanjangwani, lakini utofauti wa mabao ya kufunga na kufungwa ndio unawafanya wagonga
nyundo wa Mbeya kuwa nyuma.
Endapo Yanga watashinda mchezo wa jumatano,
watafikisha pointi 42 nyuma ya Azam fc wenye pointi 43, hivyo pengo la pointi
moja litawapa unafuu mkubwa.
Kama Azam fc watashinda, basi Yanga watazidi kuisoma
namba. Endapo watatoka sare, basi Azam fc wataendelea kubarizi kileleni kwa
raha zao.
Matokeo yoyote katika mchezo huo, hayatabadili
nafasi mbili za juu. Azam fc watabaki wa
kwanza na Yanga watabaki wa pili, huku mechi za wikiendi zikisubiriwa ambapo
Mbeya City watakupambana na JKT Ruvu, uwanja wa Chamazi.
Ugumu wa mchezo wa keshokutwa unachangiwa na
mazingira mengi;
Moja; ubora wa Azam fc ambao mpaka sasa chini ya
kocha wake Joseph Marius Omog hawajafungwa katika mechi 19 walizocheza.
Kutofungwa kwa mechi 19, kunakupa picha kuwa Azam fc
wapo katika mikakati mizito ya kuchukua ubingwa.
Hawakufanya vizuri kombe la shirikisho mwaka huu,
lakini mechi za mwisho za ligi kuu wamepata ushindi mkubwa sana katika uwanja
wa Chamazi.
Wikiendi iliyopita waliwafunga Coastal Union 4-0,
lakini kabla ya hapo nao Ashanti walikula 4-0.
Pia urejeo wa nahodha wao na mwenye bahati ya
kuwatungua Yanga, John Bocco `Adebayor`
kumewaongezea nguvu zaidi Azam fc katika safu ya ushambuliaji ambayo kwa muda
mrefu imekuwa ikiongozwa na Kipre Herman Tchetche na Mganda Brian Umony.
Siku za karibuni, Azam fc walionekana kuwa na tatizo
nafasi ya beki wa kushoto kufuatia nyota wake, Samih Hajji Nuhu na Waziri Salum
kuwa majeruhi kwa muda mrefu, lakini kwasasa pengo hilo linaonekana kuzibwa vyema na beki
aliyepandishwa kutoka kikosi cha pili, Gadiel Michael.
Mechi ya mzunguko wa kwanza Azam fc iliifunga Yanga SC mabao 3-2 uwanja wa
Taifa jijini Dar es salaam.
Kabla ya mechi hiyo, timu hizo zilikutana katika
mechi ya Ngao ya jamii ambapo Yanga waliilaza Azam fc bao 1-0.
Timu hizo zimekutana mara mbili msimu huu na kila
moja kushinda na kufungwa, hivyo kwa haraka hakuna mbabe msimu huu, na Jumatano
kila klabu itataka kuonesha kuwa ni bora zaidi.
Pili; Azam fc wanataka ubingwa wao wa kwanza msimu
huu, huku Yanga wakihitaji pointi muhimu ili kupunguza pengo. Hivyo kutakuwa na
upinzani mkubwa zaidi.
Tatu; ubora wa vikosi vyote. Yanga wana wachezaji wa
gharama kubwa zaidi, lakini hawajafanikiwa kucheza kwa mafanikio ligi kuu soka
Tanzania bara kama Azam fc.
Wao waliwahi kufungwa, Azam fc hawajafungwa mpaka sasa. Hivyo
utagundua kuwa timu hizi ni bora.
Kufungwa kwa Yanga hakumaanisha hawana timu bora,
bado kikosi chao kinaonekana kuwa na makali. Mechi itakuwa ngumu zaidi.
Joto la mechi hii linazidi kupanda na ukipita
mitaani unawasikia mashabiki wakizungumzia kipute hiki.
Nao viongozi wamesikika wakisema wapo katika
mikakati mizito ya kuibuka na ushindi.
Sina shaka kuwa mikakati hiyo inalenga kuziandaa
timu zao kucheza mpira uwanjani.
Kama mikakati inayosemwa ni nje ya uwanja, sasa hapo
kunakuwa na shaka juu ya ubora wa mechi yenyewe.
Makocha wa timu zote, Joseph Marius Omog wa Azam fc
na Hans Van Der Pluijm wa Yanga wanaonekana kutuliza akili zao kuhakikisha wanawapa
raha mashabiki wao.
Pluijm ana kazi kubwa ya kuhakikisha anapata ushindi
ili kuwapa raha mashabiki wa Yanga ambao walifurika uwanja wa Jamhuri Morogoro,
lakini waliambulia kuona timu yao inatoka suluhu.
Inafurahisha sana kuona mechi ya Azam fc dhidi ya
Yanga inagusa hisia za mashabiki kwa kiasi kikubwa.
Miaka ya nyuma, mechi ya watani wa jadi pekee ndio
ilionekana kuwa na mvuto kwa mashabiki.
Kila mtaa ukipita unasikia wakitambiana mno. Lakini
sasa mambo yamebadilika kabisa.
Mechi ya Azam fc na Yanga inazungumzwa kila mtaa, pia
mechi ya Yanga dhidi ya Mbeya City inaliteka jiji.
Pia ukija upande wa pili, Simba vs Azam fc, Simba vs
Mbeya City, Simba vs Yanga zimekuwa mechi zenye mvuto mkubwa zaidi kwa
mashabiki.
Hali hii imechangiwa na ujio wa Mbeya City na Azam
fc kuzipatia changamoto Simba na Yanga.
Kimpira ni hatua nzuri. Unapokuwa na timu nyingi zenye
ushindani na mvuto kwa mashabiki, unapata ligi bora kabisa.
Angalia mashabiki wa Mbeya City wanaokuja
kuishangilia timu yao inapocheza uwanja wa Taifa, hakika unagundua kuwa kuna
hatua soka la Tanzania linapiga.
Asante sana Azam fc na Mbeya City kwa kubadilisha
utawala wa Simba na Yanga. Sasa wakongwe hawa huwa hawalali mnapokutana.
Ingekuwa vizuri zaidi ifike wakati tuwe na timu nyingi
zaidi zenye mvuto kama Azam fc na Mbeya City ili tabia ya kutabiri matokeo na kuamini
Simba na Yanga wanashinda ife kabisa.
Yanga na Azam fc onesheni ubora uwanjani ili muwape
raha mashabiki wenu.
Mpira unachezwa hadharani, na hauchezwi kwa siri.
Tafuteni matokeo ndani ya uwanja na si nje ya uwanja.
Waamuzi chezesheni mpira kwa weledi. Sheria 17 zipo
wazi, zifuateni bila kuwa na unazi wa timu.
Mkifanya kazi yenu kwa ufanisi, mtasababisha mpira
bora kuonekana baina ya miamba hii miwili.
0 comments:
Post a Comment