
By Israel Saria on March 16, 2014
JK ACHANGIA UWANJA WA SIMBA
MWENYEKITI
wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage, jana ametangaza rasmi kwamba
hatagombea tena nafasi hiyo katika uchaguzi mkuu wa klabu hiyo
unaotarajiwa kufanyika Mei 4 mwaka huu.
Hata hivyo Rage kabla ya
kutangaza maamuzi yake ya kutotetea cheo hicho katika uchaguzi mkuu
ujao, wanachama wa klabu hiyo walianzisha vurugu katika mkutano mkuu huo
uliotishwa maalumu kwa ajili ya kufanya marekebisho wa katiba kutokana
na kiongozi wao huyo kuwaita ‘mbumbumbu’.
Kufuatia kauli hiyo,
Rage, alilazimika kuwaomba radhi wanachama hao zaidi ya 571
waliohudhuria mkutano huyo uliofanyika kwenye Ukumbi wa Bwalo la Polisi,
Oysterbay jijini Dar es Salaam.
“Napenda kuwaomba radhi
wanachama wenzangu kutokana na nilivyosema tuache umbumbumbu, lakini
sikuwa namaanisha kama wengi wenu mlivyoelewa,” alisema Rage.
Licha
ya kusema hatagombea tena uongozi, Rage, alisema ataendelea kuwa
mwanachama mwaminifu wa Simba na atatoa mchango wake ili kufanikisha
maendeleo.
“Nitatoa mchango wangu wa hali na mali, sina ugomvi na mtu yoyote na bado nina mapenzi na Simba,” aliongeza.
JK ACHANGIA UWANJA
RAIS
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk. Jakaya Kikwete, jana alitangaza
kuipa Simba Sh. milioni 30 kwa ajili ya kusaidia ujenzi wa Uwanja wake
unaotarajiwa kujengwa katika eneo la Bunju, nje kidogo ya jiji la Dar es
Salaa.
Rage alisema kwamba Rais Kikwete alimueleza ahadi hiyo
leo Jumapili asubuhi muda mfupi kabla ya kuelekea katika mkutano wa
marekebisho ya katiba.
Rage alisema kuwa Rais huyo pia aliwatakia wanachama wa Simba heri na majadiliano ya amani.
Alisema
kuwa alitumia nafasi hiyo kumuomba awasaidie kupata hati ya eneo la
Uwanja wao lililoko Bunju ambalo tayari uongozi umeshalipia gharama ya
Sh. milioni 50.

“Na alikubali
kutusaidia na katika kuonyesha yeye (Kikwete) kuwa ni mwanamichezo,
ameahidi kutupatia Sh. milioni 30 ili kufanikisha ujenzi wa uwanja,”
Rage alisema.
Aliongeza kuwa uongozi wa Simba unatarajia kuanza
kuufyeka uwanja huo kwa gari maalumu la kulimia ili waweze kutimiza
ahadi ya kuanza kuutumia uwanja huo kwa mazoezi kabla ya siku 100
walizotangaza hazijamalizika.
“Kwa niaba ya Klabu ya Simba
tunamshukuru Rais kwa msaada huo, kweli ameendelea kudhihirisha yeye ni
mpenzi wa michezo nchini,” Rage alisema.
Vile vile alisema Kamati
ya Utendaji ya Simba juzi iliingia mkataba na Benki ya Posta Tanzania
(TPB) kwa ajili ya kutoa kadi maalumu kwa mashabiki wa klabu hiyo na
awamu ya kwanza wanatarajia kuingia Sh. milioni 300.
Alisema
shabiki anayetaka kujiunga na mfumo huo ambao pia atakuwa amefungua
akaunti kwenye benki hiyo atalazimika kulipia Sh. 5,000 na Sh. 3,000
zitaingizwa kwenye mfuko wa klabu, Sh. 1,000 itakuwa ni gharama za benki
na kiasi kilichobakia ndiyo itakuwa kianzio chake kilichobaki.
…………………………………..
FEDHA ZA OKWI
Mwenyekiti
huyo aliyeingia madarakani aliwaambia wanachama wa Simba kwamba bado
uongozi wake haujapokea malipo ya Dola za Marekani 300,000 kwa ajili ya
kumuuza mshambuliaji wao, Emmanuel Okwi.
Alisema fedha hizo zikiingia
pamoja na nyingine zaidi ya Sh. milioni 216 (hakusema ni za nini)
watazikabidhi kwa uongozi mpya utakaoingia madarakani.
Aliwataka wanachama wa Simba kuwa watulivu na wasisikilize maneno yanayozungumzwa pembeni kuhusiana na fedha hizo.
SOURCE: http://www.tanzaniasports.com
0 comments:
Post a Comment