Asha
Baraka akizungumza jambo katika kutambulisha onyesho maalum la Gurumo
53 litakalofanyika Oktoba 11 katika Ukumbi wa Diamond Jubilee, jijini
Dar es Salaam. Anayefuata upande wa kushoto wa Asha ni mzee Muhdini
Gurumo, Juma Mbizo, Cosmas Chidumule na Said Kibiriti.

Juma
Mbizo, mratibu wa shoo hiyo, akionyesha mfano wa cd itakayouzwa ikiwa
ni juhudi za kumuwekea mazingira mazuri mwanamuziki Muhdini Gurumo,
baada ya kutangaza kustaafu muziki.
Picha zote na Kambi Mbwana
Na Mwandishi Wetu, Dar es Salaam
MWANAMUZIKI
mkongwe aliyestaafu kujiuzuru kuimba akiwa na bendi ya Msondo Ngoma,
Muhdini Gurumo, ameandaliwa shoo mbili za kumuaga, moja wapo ikipangwa
kufanyika Oktoba 11, ikiwa ni VIP, huku ikifanyika katika Ukumbi wa
Diamond Jubilee.
Nyingine
itafanyika Novemba Mosi mwaka huu katika Ukumbi wa TCC Sigara
Chang’ombe, jijini Dar es Salaam, zote zikiwa na lengo la kumuaga kwa
heshima mwanamuziki huyo na kumpa nafasi ya kuyamudu maisha yake baada
ya kuachana na muziki.
Akizungumza
leo na waandishi wa habari, Mwenyekiti wa shoo hiyo iliyopewa jina la
(Gurumo 53), Asha Baraka, alisema kuwa ni heshima kuwa na mwanamuziki
kama Gurumo, hivyo wadau wameamua kuandaa shoo hizo za kumtafutia fedha
mkali huyo.
Alisema
wazo hilo limefanyiwa kazi kwa pamoja, akiwa na wadau kadhaa, akiwamo
Said Mdoe Katibu wa Kamati hiyo, Richard Sakala mjumbe, Cosmas
Chidumule, Waziri Ally, Said Kibiriti na Juma Mbizo, ambaye ndio mratibu
wa Kamati hiyo.
”Lengo
si kumpa karatasi za kuthamini mchango wake katika tasnia ya muziki wa
dansi Tanzania, ila kuhakikisha kuwa anapata mwangaza wa maisha yake
baada ya kuachana na muziki.
”Huyu
ni mwanamuziki mwenye uwezo wa juu wakati huo, hivyo kwa sasa lazima
sisi wadau tuhakikishe anajiweka katika ramani nzuri, ikiwa ni kutambua
ataishi vipi nje ya muziki,” alisema.
Naye
Gurumo aliwaambia waandishi wa habari kuwa ameamua kuachana na muziki
kwasababu umri na afya yake hairuhusu kufanya kazi hiyo, hivyo asitokee
mtu wa kupotosha ukweli wake huo.
”Nasikia
watu wanasema naachana na muziki Msondo nikiwa na lengo la kurudi tena
Sikinde, jambo ambalo si kweli kwakuwa sioni nitamuimbia nani wakati
nimechoka.
”Naomba
kwa sasa kuwapa nafasi watu waliojitolea kunisaidia hasa kwa kuunda
kamati hii ambayo nitapanda jukwaani kuimba mara ya mwisho, ukizingatia
kuwa kazi yangu inahitaji kuagana na mashabiki wangu jukwaani na si
mahali pengine,” alisema.
Katika
hatua nyingine, mwanamuziki Cosmas Chidumule, alisema kuwa licha ya
kuwa ameokoka, ila atapanda jukwaani kuimba na mzee Gurumo kama sehemu
ya kutambua mchango wake.
”Nimeokoka
lakini si sababu ya kunifanya nishindwe kumheshimu mwanamuziki ambaye
nina uhakika mchango wake ulinifanya niwe juu katika muziki wa dansi
Tanzania,” alisema.
Kwa
mujibu wa Kamati hiyo ambayo Mdoe ndio Katibu wake, taratibu zote
zinaendelea ikiwa ni kuandaa nyimbo alizowahi kuimba na kuziweka katika
mfumo wa kibiashara, ikiwamo mpango wa kuuda nyimbo zake katika
makampuni ya simu za mikononi.
0 comments:
Post a Comment