KATIBU
Mkuu wa Wizara ya Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga
akiongea na Maafisa Mawasilino Serikalini (hawamo pichani) wakati
akifungua mkutano wa tathmini wa awamu ya kwanza ya utaratibu wa Maafisa
Mawasiliano kuzungumza na waandishi wa habari, ambapo aliwataka
kutekeleza utaratibu huu kama ulivyopangwa ili kuweza kutoa taarifa
mbalimbali za utekelezaji wa Sera na Miradi inayoratibiwa na Ofisi zao
kwa wananchi kupitia waandishi wa habari, katika mkutano uliofanyika
jana Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania(TCRA) Jijini Dar es
Salaam. Kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi.
Zamaradi Kawawa.
Baadhi
ya Maafisa Mawasilino Serikalini waliohudhuria mkutano huo wa tathmini
uliofanyika jana katika Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania
(TCRA) Jijini Dar es Salaam.
MKURUGENZI
Msaidizi wa Idara ya Habari (MAELEZO) Bi. Zamaradi Kawawa Akiwasilisha
ripoti ya utekelezaji Mikutano ya awamu ya kwanza ya utaratibu wa
maafisa mawasiliano kuzungumza na waandishi wa habari kuhusu Sera na
Mipango pamoja na ujibuji wa hoja mbalimbali zinazohusu Ofisi zao,
kwenye katika mkutano uliofanyika jana Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano
Tanzania (TCRA) Jijini Dar es Salaam.
Meneja
Mawasiliano wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Innocent Mungy
Akiwasilisha kwa Maafisa Mawasilino Serikalini juu ya namna bora ya
kuandaa na kuboresha taarifa kwa vyombo vya habari, katika mkutano
uliofanyika jana Ukumbi wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) Jijini
Dar es Salaam.
MKURUGENZI
wa Idara ya Habari na Msemaji wa Serikali Assah Mwambene akiongea na
Maafisa Mawasilino Serikalini (hawamo pichani) jana wakati mkutano wa
tathmini wa awamu ya kwanza ya utaratibu wa maafisa mawasiliano
kuzungumza na waandishi wa habari, ambapo alisisitiza utoaji wa taarifa
za utekelezaji wa Sera na Mipango pamoja na kujibu hoja mbalimbali
zinazohusu Ofisi zao. Kulia ni Katibu Mkuu wa Wizara ya
Habari,Vijana,Utamaduni na Michezo Bi. Sihaba Nkinga na katikati ni
Mkurugenzi Msaidizi wa Idara ya Habari Bi. Zamaradi Kawawa.




………………
HOTUBA
YA BI SIHABA NKINGA, KATIBU MKUU, WIZARA YA HABARI VIJANA,UTAMADUNI NA
MICHEZO KUFUNGUA KIKAO CHA TATHMINI YA MZUNGUKO WA KWANZA WA MIKUTANO YA
WASEMAJI SERIKALINI NA WAANDISHI WA HABARI, DAR ES SALAAM, SEPTEMBA 13,
2013
Ndugu Mkurugenzi wa Idara ya Habari –MAELEZO,
Wakurugenzi, Wakurugenzi Wasaidizi na Mameneja mliopo hapa,
Maafisa Mawasiliano,
Waandishi wa Habari,
Wageni Waalikwa,
Mabibi na Mabwana Habari za Asubuhi!!!
Awali
ya yote napenda kuchukua fursa hii kumshukuru mungu kuweza
kunikutanisha nanyi siku hii ya leo tukiwa na afya njema. napenda kutoa
shukrani zangu za dhati kwenu kwa kuhudhuria mkutano huu muhimu kwa
ajili ya kufanya tathmini ya utekelezaji wa ratiba ya mzunguko wa kwanza
wa mikutano ya Waandishi wa Habari na Wasemaji Serikalini.
Ndugu Washiriki,
Kama mnavyofahamu Wizara ambayo ina jukumu la kusimamia masuala ya Habari na Uratibu wa Mawasiliano ya Serikali, iliandaa ratiba kwa ajili ya Ofisi za Serikali kujitangaza kwa umma kupitia vyombo mbalimbali vya mawasiliano nchini.
Ratiba
hiyo ilianza rasmi Tarehe 4, Julai,2013 na kumalizika Septemba 3,2013
ambapo Wasemaji wa Taasisi/Wakuu wa Idara/Vitengo vya Mawasiliano
Serikalini walitakiwa kuzungumza na vyombo vya Habari katika siku na
muda uliopangwa . Mikutano 75 ilifanyika katika Ukumbi wa Mikutano wa
Idara ya Habari-MAELEZO na mkutano mmoja wa Hospitali ya Taifa Muhimbili
ulifanyika katika ukumbi wa mikutano wa Kitengo kipya cha magonjwa ya
moyo cha Hospitali hiyo iliyopo Upanga, Dar es Salaam.
Nimeambiwa kuwa Jumla
ya Taasisi za Serikali 88 zilitakiwa kushiriki katika mikutano hiyo,
kati ya Taasisi hizo, Taasisi 75 sawa na asilimia 85 zilishiriki katika
mikutano hiyo na Taasisi 14 sawa na asilimia 15 hazikushiriki.
Kwa
mara nyingine tena natoa pongezi kwa Taasisi zote zilizoshiriki katika
mikutano hiyo. Mikutano hii ni muhimu na imeleta tija kwa kuwa wananchi
kupitia Vyombo vya Habari nchini walipata fursa ya kuelewa masuala mengi
ya msingi yanayotekelezwa na Serikali kwa lengo la kupunguza umaskini
na kukuza uchumi wa wananchi. Ni ukweli usiopingika kuwa maswali
yaliyoulizwa na wananchi kupitia Waandishi wa Habari wakati wa mikutano
hiyo kunaonesha shauku kubwa iliyokuwepo ya kutaka kujua Serikali
inafanya nini kwa ajili ya wananchi wake.
Aidha,
napenda kutoa wito kwa Taasisi ambazo hazikuhudhuria mzunguko wa
kwanza wa mikutano hii wajiandae kwa ajili ya kushiriki mzunguko wa
Pili.
Ndugu Washiriki,
Kama
mnavyofahamu, jukumu kubwa mlilopewa ni kuwezesha Serikali kupitia
Ofisi zenu kufanya mawasiliano na umma kupitia Vyombo vya Habari kuhusu
masuala mbali mbali yanayohusu Sera na Miradi inayotekelezwa na Serikali
yenye lengo la kustawisha maendeleo ya watanzania. Kwa kufanya hivyo,
Serikali inatimiza wajibu wake wa kutoa haki ya msingi ya wananchi ya
kupata habari hususan zinazohusu utekelezaji wa shughuli mbali mbali za
Serikali.
Kumekuwa
na malalamiko ya kutokuridhika na namna ambavyo Serikali haitoi taarifa
kwa umma ili kuweza kutosheleza kiu ya wananchi ya kupata habari
zinazohusu utekelezaji wa shughuli za maendeleo ambazo kwa kiasi fulani
huchangiwa na fedha za walipa kodi.
Ndugu Washiriki,
Nitumie
nafasi hii kuwaasa kuwa tumieni fursa za ratiba za mikutano
zinazoandaliwa na Idara ya Habari-MAELEZO ili kukidhi kiu ya jamii ya
kuhabarishwa na kuelimishwa shughuli za Serikali.
Pamoja
na mikutano hiyo inayoratibiwa na Wizara, napenda pia kuwakumbusha kuwa
Taasisi kupitia Ofisi zenu kuandaa Mkakati wa Mawasiliano Serikalini
kwa wale ambao hawana na wale ambao tayari wameshaandaa Mkakati huo
utekelezeni kwa dhati ili kufanikisha malengo yaliyokusudiwa.
Aidha,
natoa wito kwenu kama daraja la mawasiliano ya Serikali kwa umma
kuelewa Sera na shughuli zote zinazotekelezwa na Taasisi zenu ili muweze
siyo tu kuwa wasemaji wazuri wa Serikali lakini pia kuwa washauri
wazuri wa viongozi katika ngazi mbali mbali kuhusiana na masuala ya
mawasiliano ya Serikali kwa umma.
Nasisitiza
kuwa toeni ushauri ulio sahihi, kwa haraka na wakati ili kutoa majibu
mwafaka kwa umma pale ambapo Vyombo vya Habari vinakuwa vimetoa taarifa
zisizo sahihi. Hili lifanyike kwa vyombo vyote vya Habari vikiwemo
Radio, Televisheni, Magazeti na Mitandao ya Kijamii pale inapolazimu ili
kuondoa upotoshaji wa taarifa za Serikali unaosababishwa na ukuaji wa
teknolojia ya Habari na Mawasiliano ambapo kila mtu anaandika kile
anachokijua bila kufuata weledi wa taaluma ya uandishi wa habari. na
utangazaji. Taarifa zisizosahihi zikiachwa bila kujibiwa zinaweza
kuleta uchonganishi kati ya Serikali na umma na hivyo kusababisha
sintofahamu isiyokuwa na ulazima.
Aidha,
napenda kuchukua fursa hii kuwashukuru Waandishi wa Habari
walioshiriki katika zoezi hili kwa mchango mkubwa wa kutoa taarifa kwa
umma kuhusu utekelezaji wa shughuli mbali mbali za Serikali hususan kwa
kazi kubwa mliyoifanya wakati wa mikutano ya Waandishi wa Habari na
Wasemaji wa Taasisi za Serikali iliyoanza Julai 4,2013 na kumalizika
Septemba 3, 2013.
Ndugu Washiriki ,
Wizara
sasa imeandaa ratiba ya awamu ya Pili ya Mikutano ya Waandishi wa
Habari na Wasemaji wa Taasisi ambayo inaanza Septemba 16, 2013. Naomba
mshiriki kwa kikamilifu na mjiandae vizuri zaidi kama mlivyofanya awali.
Aidha, mkitumie vizuri kikao cha tathmini kwa kufahamu mafanikio na
upungufu uliokuwepo wakati wa utekelezaji wa awamu ya Kwanza ya Mikutano
hiyo ili muweze kujirekebisha na kuboresha zaidi mikutano hii ya Awamu
ya Pili.
Ni
matumaini yangu kuwa wenzetu Waandishi wa Habari wataendelea kutoa
Ushirikiano kwa Serikali katika kutoa taarifa wakati wa mikutano hii.
Ndugu Washiriki ,
Mwisho
niwatakie maandalizi mema, mfanye kazi vizuri kwa kuhabarisha jamii
yale yote yanayofanywa na Serikali yetu. Wizara itaendelea kushirikiana
nanyi ili kufanikisha majukumu yetu sote.
Naomba
sasa nitamke kuwa mkutano wenu umefunguliwa rasmi. Nawatakia kila la
heri na mafanikio katika tathmini ya kazi kubwa mliyoifanya katika Awamu
ya Kwanza ya kukutana na waandishi wa Habari pamoja na kujibu maswali
yote kwa usahihi na kwa kutumia takwimu sahihi.
Ahsanteni.
0 comments:
Post a Comment