Sunday, August 18, 2013


Na Baraka Mpenja 
Wakati mashabiki wakifurika kwa wingi kwenda kuutazama mchezo wa ngao ya jamii hapo jana baina ya mabingwa wa ligi kuu Tanzania bara, klabu ya Yanga dhidi ya Makamu bingwa, Wana Lambalamba Azam fc katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, binafsi sikwenda kushangilia timu yoyote bali nilienda kushuhudia mambo makubwa mawili.
Mechi ya jana kwa upande wangu ilikuwa burudani kubwa sana kwani nilishuhudia soka safi la ushindani, kwani timu zote “zimefundwa” kiukweli.
Maarifa ya makocha wawili wa kizungu, Ernie Brandts kwa Yanga na Sterwart John Hall wa Azam, yanaonekana kuwakolea vijana wa Kitanzania na nje ya Tanzania wanaozichezea timu hizo mbili.
Ukihusianisha majina ya “Yanga na Azam fc” hayana ushindani, na hii inatokana na Yanga kuwa klabu kongwe zaidi hapa Tanzania na imejiimarisha kwa kuwa na mashabiki lukuki zaidi ya Azam ambao ndio kwanza wameanza safari yao, lakini kwa kuangalia aina ya mpira unaochezwa na timu hii yenye makazi yake Chamazi, najiridhisha kuwa ni timu bora iliyojipanga na itafika mbali.
Inafahamika kuwa mechi ya jana hiyo ilimazika kwa Yanga kushinda kwa bao 1-0, bao likifungwa na Salum Abdul Telela katika dakika ya pili tu, watoto wa mjini huita “Dakika za Asubuhi”, kwangu mimi matokea hayana maana sana, lakini  nilijivuta kwenda uwanja wa Taifa kwa  mambo mawili kama nilivyosema hapo juu.
Ngao
Nahodha wa Yanga, Nadir Haroub “Canavaro” akipokea ngao ya jamii kutoka kwa mgeni Rasmi, mkuu wa Mkoa wa Dar es salaam, Mhe. Said Meck Sadick
Kwanza, nilienda kumuangalia bwana mdogo aliyeshutumiwa na mashabiki wengi wa soka nchini kwa kusababisha penati na kuwa uchochoro wakati  Taifa Stars ilipofungwa na Uganda mabao 3-1 jijini Kampala kuwania kucheza fainali za CHAN,  huyu si mwingine bali ni kinda David Luhende.
Watu walizungumza sana juu ya uwezo wake,wengine walisema kocha Kim alikosea kumpanga mechi yake ya kwanza Taifa Stars  dhidi ya Uganda, mechi kubwa ya mashindano na alikuwa uchochoro, lakini wakasahau kuwa hata “Mbuyu ulianza kama mchicha”. Binafsi nilijiridhisha kuwa atakuwa bora zaidi kwa uwezo alioonesha kwa siku ya kwanza, licha ya kuwa na mapungufu.
LUHENDE & MSUVA
DAVID LUHENDE
Naupenda sana msemo wa kocha wa klabu ya Mbeya City ya jijini Mbeya, Juma Mwambusi, huwa anasema “Mchezaji yeyote mwenye uzoefu alianza kutokuwa na uzoefu, akapewa nafasi akacheza na baadaye kupata uzoefu, hivyo lazima wachezaji wote wapate nafasi ya kucheza ndipo wajenge uzoefu, usipompa nafasi kijana atatoa wapi uzoefu”?.
Nina uhakika hata kocha wa Stars, Kim Poulsen ana falsafa hiyo ya kuwaamini wachezaji vijana na kuwapa majukumu mazito kama alivyofanya kwa David Luhende ambaye aliitwa kwa mara ya kwanza Taifa stars mwezi uliopita na kucheza mechi ngumu ya mashindano dhidi ya Uganda.
Ukitaja jina la Luhende, wapenda michezo wengi waliokuwa na malengo ya kwenda Afrika kusini kushuhudia fainali za kombe la mataifa ya Afrika kwa wachezaji wa Ligi za ndani, CHAN nywele zinawasisimka kutokana na madudu aliyofanya nyota huyo kinda baada ya kuitwa kuziba pengo la Shomary Kapombe aliyekwenda Ulaya kujaribu bahati yake ya kucheza soka la Mataifa.
Luhende alikuwa uchochoro vibaya sana kwani alipitisha mipira mingi ya hatari na kuunawa mpira katika eneo la hatari na mwamuzi kuwazawadia mkwaju wa penati Uganda na kufunga bao la pili kupitia kwa nyota wao Brian Majwega na kuwachanganya stars waliolala kwa mabao 3-1.
Jana bila kuwa na roho ya kinyongo,  bila kujali unazi wa timu, Luhende alipiga mpira mkubwa sana na ilikuwa burudani kubwa wanapokutana na Khamis Mcha “Vialli” wa Azam, ufundi mkubwa ulioneshwa na hii inaashiria hatari kwa beki wa kushoto wa Yanga, Oscar Samwel Joshua.
Wakati nimekaa na rafiki zangu kumtazama nyota huyo anayechipukia katika soka, nilijiridhisha kwa kusema kuwa Luhende amebadilika na anaonesha uwezo mkubwa na hivyo kuwa na neno moja kwake kuwa “Akizingatia nidhamu ya mpira na mazoezi, akiachana na sifa za kupambwa na vyombo vya habari na kujitambua, basi atafika mbali kwa kipaji kikubwa alichopewa na Mungu”.
YANGANAAZAMNOV420122Jambo la pili katika mchezo wa jana, nilienda kuchunguza mabadiliko ya washambuliaji wa timu zote mbili.
Binafsi bado nimejiridhisha kuwa kuna shida kubwa, kwani nafasi nyingi zilipatikana kwa timu zote, lakini washambuliaji walishindwa kuzibadili kuwa mabao.
Kwa upande wa Azam fc,  John Bocco na Kipre Tchetche walipata nafasi za kufunga, lakini walikosa umakini na pengine walikumbana na mabeki wenye akili akiwemo Kelvin Yondan, Nadir Haroub “Canavaro”, David Luhende, na Mbuyu Twitwe. Lakini kwa mshambuliaji lazima awe na akili ya kufunga kwani ndio kazi yake akiwa uwanjani.
7b85277ad0L
JOHN RAPHAEL BOCCO “ADEBAYOR”
Hata kwa upande wa Yanga, Telela , Msuva, Kavumbagu,  Haruna Niyonzima  na wengine walishindwa kufunga kwa nyakati tofauti baada ya kupata nafasi nzuri.
kavumbagu
DIDIER KAVUMBAGU
Kukosa ni kawaida katika mchezo wa soka, tunashuhudia wanasoka bora wa dunia kama akina Cristiano Dos Santos Aveiro Ronaldo na Lionel Andrew Jorge Messi wakikosa nafasi za kufunga, lakini kwa wao imekuwa mara chache sana kukosa nafasi zote.
Kwa Tanzania mshambuliaji anaweza kupata nafasi tatu za wazi akashindwa kuzitumia, lakini wenzetu akipata nafasi tatu angalau moja inazaa bao au mbili na kama ameamka vizuri anaweza kufunga zote.
Kwa namna ambavyo washambuliaji wa jana walikosa nafasi za kufunga ambapo mashambulizi ya kushitukiza yalitawala kwa pande zote, najiridhisha na kuunga mkono maneno ya kocha Charles Boniface Mkwasa “Master” ambaye kwa wakati wote anasisitiza kuwa soka la Tanzania linaumwa zaidi kwa upande wa washambuliaji na unahitaji mwarobaini wa nguvu kuponya.
Mkwasa amekuwa akisema washambuliaji wengi wa soka la Tanzania wanakosa umakini na kushindwa kufunga licha ya makocha kutumia muda mwingi kuwafanyisha mazoezi ya kufunga, na hii anaitaja kuwa moja ya sababu ya Taifa Stars kushindwa kupata ushindi katika mechi mbalimbali.
Mbali na hayo, mechi ya jana, binafsi nimejiridhisha kuwa Azam fc ni wazuri sana kwani walionesha ushindani mkubwa sana mbele ya Yanga.
Ni klabu ambayo inaonekana ni timu, wamekaa chini wakajifunza mpira na wanajua nini wanataka kufanya wanapokuwa uwanjani.
Licha ya kufugwa bao 1-0, lakini soka walilocheza lilikuwa zuri sana, ingawa changamoto ilikuwa ubora wa Yanga na wachezaji wake.
Hakuna asiyejua kwa sasa kuwa kikosi cha Yanga ni bora zaidi, kimesheheni nyota wa uhakika na huwa kinachagizwa na jina la Bingwa mtetezi, hivyo jana walicheza vizuri na kuwafunga Azam kwa makosa madogo waliyoyafanya, lakini endapo wachezaji wote wangekuwa makini, timu yoyote ingepata ushindi katika mechi ya jana.
Kikubwa ambacho nimegundua, kama mechi ya jana itabeba taswira ya ligi kuu ijayo, kwa maana ya ushindani iliokuwepo jana ukaonekana kwa timu zote zinapokutana, najiridhisha kuwa ligi itakuwa tamu kuliko misimu uliyopita.
Lazima niwapongeze Yanga kwa kuifunga Azam yenye kikosi kizuri na kutwaa ngao ya jamii, pia walicheza vizuri hasa safu ya kiungo na ulinzi. Lakini kwa Azam fc sina wasiwasi, kwa mara zote wamekuwa wakijitahidi sana kucheza soka safi.
Tunahitaji ligi yetu kupiga hatua kubwa, na kama ushindani wa jana utaendelea katika mechi zote, basi naamini tutakuwa tumesogea kiasi fulani.
Nazitakia timu zote maandalizi mema ya ligi kuu Soka Tanzania bara.

0 comments:

 
https://www.sexmutant.com/ https://www.sexindrag.com/ porn movies sex videos hd porno video