Na Baraka Mpenja
WAKATI Timu mbalimbali za ligi kuu soka Tanzania bara zikiendelea na zoezi la usajili wa wachezaji wapya kwa ajili ya msimu mpya wa ligi kuu unaotarajiwa kuanza Agosti 24 mwaka huu, viongozi wa klabu hizo wametakiwa kuwaachia makocha kuendesha usajili badala ya kuingilia mambo ya kiufundi.
Akizungumza na FULLSHANGWE kocha wa mpira wa miguu aliyekuwa akikinoa kikosi cha mabingwa wa zamani wa Tanzania, African Sports ya Tanga, na sasa mjumbe wa kamati kuu ya ufundi ya wekundu wa Msimbazi Simba, John Wiliam “Del Piero” amesema kumekuwepo na tabia ya viongozi wa klabu ambao sio makocha wa kandanda kitaaluma kujihusisha na zoezi la kutafuta wachezaji wapya bila kupitia ripoti za waalimu wao.
“Kitaalamu kocha ndio mtu wa kwanza kupendekeza majina ya wachezaji anaowahitaji, viongozi wanakabidhi majina hayo kwa kamati ya usajili na kuanza kutekeleza matakwa ya waalimu wao na si vinginevyo, lakini hapa nchini unakuta viongozi wanazungumza na wachezaji na kuwasajili kwa matakwa yao binasi na si makocha, hizi ni siasa za soka na hazipaswi kuendelezwa”. Alisema Piero.
Kocha huyo aliongeza kuwa siasa nyepesi zinazoendesha soka la Tanzania, zinalifanya taifa lishindwe kusogea mbele katika mchezo wa soka, hivyo lazima mabadiliko makubwa yafanyike katika fikra za viongozi waliopewa dhamana ya kuongoza soka katika klabu za Tanzania.
Piero alisisitiza kuwa yeye si muamini wa siasa za soka, bali anapenda klabu ziendeshwe kitaalamu kwa maana ya kila mtu kutekeleza majukumu yake bila kuingiliwa na mwingine.
“Kocha afanye kazi yake ya kutafuta wachezaji wa kuwasajili, viongozi watekeleze mipango ya kocha bila kumuingilia yeye, lakini huo mpango wa kumchagulia wachezaji ambao hawaendani na mfumo wake ni udhaifu mkubwa wa kuendesha soka”. Alisema Piero.
Mjumbe huyo wa kamati ya ufundi ya Simba, aliongeza kuwa timu kubwa za Tanzania kwa maana ya Simba na Yanga, ni mara nyingi zimekuwa zikihusishwa na muungiliano wa madaraka baina ya viongozi dhidi ya makocha katika masuala ya usajili, lakini ameonya kuwa tabia hiyo ni mbaya na ndio maana kumekuwepo na matatizo yasiyo ya lazima kati ya waalimu na viongozi.
“Watu wanaendesha soka kifitina, unakuta mchezajif fulani ni mzuri, lakini kutokana na chuki binafsi, viongozi wanalazimisha kumuacha mchezaji ambaye yupo katika mipango ya mwalimu, sasa kocha analazimika kufuata matakwa ya waajiri wake, kikuweli hii ni tabia mbaya sana na bila kupepesa macho lazima ipigwe vita”. Alisisitiza Piero.
Wakati Piero akisema hayo, naye Rais wa Shirikisho la soka Tanzania TFF, Injinia Leogigar Tenga, hivi karibuni alizitaka klabu kuwaachia makocha wao kuendesha masuala ya ufundi hususani zoezi la kusajili wachezaji wanaowahitaji wao na sio kuingiliwa na viongozi.
Tenga alisema mpira lazima uendeshwe kwa kuiga mfano mzuri wa mataifa ya wenzetu ambapo kocha ndio mwenye mamlaka ya kutaka kumuuza mchezaji na kununua mpya, kama hajakubali yeye viongozi hawana uwezo wa kumlazimisha.
Viongozi wa klabu kubwa za Tanzania wana tabia ya kuwalazimisha baadhi ya waalimu wao kusajili wachezaji wanaowahitaji wao na kutofautiana na makocha wao.
Mbali na kusajili wao, pia wanayo tabia ya kuwapangia makocha wao vikosi vya kutumia katika mechi, huku wakiwasimamisha baadhi ya wachezaji kwa sababu zao binafsi bila kumshirikisha kocha wa timu.
Tabia hizi ni siasa za soka, na kwa mwendo huu hatutafika popote zaidi ya kupiga maki tu na kurudi pale tulipotoka.
0 comments:
Post a Comment