

……………………
Na Baraka Mpenja wa Fullshangwe Dar es salaam
Wakati homa ya pambano la kuwania kucheza fainali za mwakani nchini Afrika kusini za mataifa ya Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani (CHAN) baina ya vijana wa timu ya taifa ya Tanzania Taifa Stars dhidi ya Uganda “The Cranes” julai 13 mwaka huu uwanja wa Taifa, kocha wa Stars, Mdernimark Kim Paulsen ameweka wazi kuwa pambano hilo litakuwa gumu sana, lakini haina jinsi ila ni kuhakikisha anapata ushindi wa nyumbani.
Akizungumza katika mazoezi ya timu hiyo jana jioni katika dimba la Taifa jijini Dar es salaam, Kim alisema kwa sasa anafanya kazi ya kunoa safu yake ya ushambuliaji ili wawe na uwezo wa kufumania nyavu kadri wawezavyo.
“Uganda wana timu bora, na ndio maana mara nyingi wamekuwa wakijitahidi kufuzu kwa fainali za mataifa ya Afrika na kombe la dunia mwakani, lakini hii haimaanishi tunawaogopa bali tunawaheshimu sana , tutapambana katika uwanja wa nyumbani ili kuibuka na ushindi mnono”. Alisema Kim.
Stars ambao leo saa tisa alasiri wataendelea na mazoezi uwanja wa Taifa wamehamishia nguvu zote kutafuta tiketi ya kucheza CHAN baada ya kushindwa kufuzu fainali za kombe la dunia mwakani nchini Afrika kusini huku wakiburuzwa na mabao 4-0 na akina Yaya Toure.
Kim amewataka watanzania kujenga imani na timu yao kwani wachezaji wana morali kubwa ya kucheza mechi hiyo muhimu dhidi ya Waganda.
Wakati huo huo naye kocha wa Uganda Milutin Sredojovic (Micho) amekaririwa na vyombo vya habari akisema anatarajia ushindani mkubwa kutoka kwa stars huku akidai timu ya Tanzania kwa asilimia kubwa ina kikosi cha wachezaji wale wale kasoro wawili, Mbwana Samata na Thomas Ulimwengu wanaocheza soka la kulipwa TP Mazembe ya Kongo DRC.
Micho Alisema pamoja na kuiheshimu Tanzania bado ana imani ya kuibuka na ushindi katika uwanja wao mzuri wa Taifa jijini Dar es salaam.
Tusubiri kuona nani ataibuka na ushindi katika mchezo huo, na tayari hapo jana shirikisho la soka Tanzania TFF liliweka wazi viingilio vya kuitazama mechi hiyo.
Kiingilio cha chini katika mechi ya mchujo ya Kombe la Afrika kwa Wachezaji wa Ligi za Ndani (CHAN) kati ya Tanzania (Taifa Stars) na Uganda (The Cranes) itakayochezwa Jumamosi (Julai 13 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam ni sh. 5,000 kwa viti vya rangi ya kijani.
Viti vya kijani katika uwanja huo wenye uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000 viko 19,648. Kwa upande wa viti vya rangi ya bluu ambavyo viko 17,045 kiingilio ni sh. 7,000. Kiingilio kwa viti vya rangi ya chungwa ambavyo viko 11,897 ni sh. 10,000.
Viingilio vya daraja la juu ni kama ifuatavyo; VIP C yenye watazamaji 4,060 ni sh. 15,000 wakati sh. 20,000 ni kwa VIP B yenye watazamaji 4,160. VIP A yenye watazamaji 748 kiingilio chake ni sh. 30,000.
Mechi hiyo ya kwanza ya raundi ya mwisho kuwania tiketi ya kucheza fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Afrika itachezeshwa na mwamuzi Thierry Nkurunziza kutoka Burundi. Mechi ya marudiano itachezwa jijini Kampala kati ya Julai 26 na 28 mwaka huu.
Tiketi kwa ajili ya mechi hiyo itakayoanza saa 9 kamili alasiri zitaanza kuuzwa siku moja kabla ya mchezo (Ijumaa) katika vituo vifuatavyo; Shule ya Sekondari Benjamin Mkapa, Sokoni Kariakoo, mgahawa wa Steers ulioko mtaa wa Ohio/Samora, Oilcom Ubungo, Kituo cha Mafuta Buguruni, Dar Live Mbagala na BMM Barbershop iliyoko Sinza Madukani.
Katika vituo hivyo tiketi zitauzwa katika magari maalumu. Magari hayo pia yatafanya mauzo ya tiketi uwanjani siku ya mechi.
Tunapenda kuwakumbusha watazamaji kutonunua tiketi mikononi mwa watu au katika maeneo yasiyohusika ili kuepuka kununua tiketi bandia, hivyo kukosa fursa ya kushuhudia mechi hiyo.
0 comments:
Post a Comment