TIMU
 ya soka ya taifa ya Tanzania, Taifa Stars usiku huu imefanyiwa 
kilichoonekana kuwa hujuma baada ya kufanyiwa vurugu na kuzimiwa taa 
ishindwe kufanya mazoezi kwenye Uwanja huo siku moja kabla ya mchezo wao
 na wenyeji wao Morocco kesho, kuwania tiketi ya kucheza Fainali za 
Kombe la Dunia. 
Sheria
 za FIFA zinasema timu mgeni, itapewa fursa ya kufanya mazoezi katika 
Uwanja utakaotumika kwa mechi dhidi ya wenyeji katika muda ambao mechi 
itachezwa, lakini leo msafara wa Stars ulipofika Uwanja wa Marakech 
ulizuiwa kuingia ndani na askari wa uwanjani hapo. 
Juhudi
 za Kocha mkuu wa Stars, Kim Poulsen kuwaelewesha askari wa Uwanja huo 
sheria ili wairuhusu timu kuingia uwanjani hazikuzaa matunda na ikabidi 
viongozi wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) waingilie kati, nao pia 
wakachemsha.
Ikawadia
 zamu ya viongozi wa Kamati ya Ushindi ya Stars, inayodhaminiwa na 
Kilimanjaro Premum Lager, ambao nao walichemsha- ndipo baadhi wa 
Watanzania waishio hapa na wachache waliosafiri kutoka Dar es Salaam 
walipoongeza nguvu.
Walikwenda kufungua geti kwa nguvu, wakawaweka kando askari waliokuwa wanawazuia na kuiingiza timu uwanjani kufanya mazoezi. 
Hata hivyo, Stars ilipofika uwanjani ililazimika kusubiri tena, kwani wenyeji Simba wa Atlasi walikuwa wakiendelea na mazoezi.
Baada
 ya nusu saa, Morocco walimaliza awamu yao na Stars wakaanza kupasha 
misuli moto. Hata hivyo, baada ya dakika 34, taa za Uwanja huo zilizimwa
 na uwanjani kuwa giza totoro, lakini viongozi wa TFF wakaenda kuomba, 
zikawashwa na timu ikafanya mazoezi kwa dakika 10 zaidi. 
Naibu
 Waziri wa Habari Utamaduni na Michezo, Mh. Amos Makalla aliyekuwapo 
wakati wa vurumai zote hizo, alisikitishwa mno na kitendo hicho akisema 
si cha kiungwana na si cha kiunamichezo.
Makamu
 wa Rais wa TFF, Athumani Nyamlani alisema Morocco walikuja kucheza Dar 
es Salaam walipokewa vizuri na wakahudumiwa vizuri hadi wanaondoka, 
ajabu leo wanaifanyia ‘unyama’ Tanzania.
Mkuu
 wa Msafara wa Stars hapa, Crescentius John Magori alisema watapeleka 
malalamiko FIFA, waandaji wa michuano ya kufuzu kwa Kombe la Dunia na 
kwa kuwa ushahidi upo, anaamini Morocco watachukuliwa hatua.
Mwenyekiti
 wa Kamati ya Usajili ya Simba SC, Zacharia Hans Poppe alishauri Stars 
icheze chini ya angalizo kwa kuwasilisha barua FIFA mapema ili wakae 
wanajua kuhusu hali halisi Morocco.
Kwa
 ujumla kilichotokea leo kimewatia woga Watanzania wengi waliopo hapa 
kuelekea mchezo wa kesho, ambao Stars inahitaji ushindi ili kujiimarisha
 katika mbio za kuelekea Brazil 2014. 
Hata
 ulinzi wa msafara wa Stars kutoka hotelini hadi uwanjani hakuwa wa 
kutosha na ilishuhuidiwa mara kadhaa ukiingiliwa na magari mengine 
barabarani wakati timu ikienda uwanjani kwa mazoezi.
Wenyeji nchini Morocco wanasema inapowadia mechi, huwa wanaogopa kwa sababu mara nyingi hutokea vurugu ya damu kumwagika.
Kwa ujumla Stars inaingia katika mchezo wa kesho katika hali ya wasiwasi na woga mkubwa. 
Stars itashuka dimbani saa 3:00 usiku kesho kwa saa za hapa sawa na saa 5:00 za Tanzania kucheza na Morocco.
Stars
 inashika nafasi ya pili katika Kundi C, ikiwa na pointi sita nyuma ya 
Ivory Coast yenye pointi saba, ambayo kesho itakuwa ugenini ikimenyana 
na Gambia katika mchezo mwingine wa kundi hilo.
Stars
 ilitua hapa Jumatatu ikitokea Ethiopia ambako iliweka kambi ya wiki 
moja na kucheza mchezo wa kirafiki dhidi ya Sudan, ulioisha kwa sare ya 
bila mabao.
Kabla
 ya kuja hapa, Stars iliweka kambi ya wiki moja katika hoteli ya 
Tansoma, Dar es Salaam ikijifua Uwanja wa Karume na siku chache kabla ya
 kuondoka ilialikwa Ikulu na Rais Jakaya Kikwete, aliyewapa hamasa kwa 
hotuba nzuri. 



0 comments:
Post a Comment