![]() |
JKT OLJORO |
Na Baraka Mpenja Dar
es Salaam
Maafande wa Jeshi la kujenga taifa,
JKT Oljoro kutoka jijini Arusha wanaendelea kupanga silaha za kuwaangamiza
vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara, vijana wa mitaa ya Jangwani, Dar Young
Africans, katika mchezo wa ligi kuu utakaopigwa uwanja wa taifa jumatano aprili
10.
Akizungumza kwa njia ya simu kutoka
jijini Arusha, Kocha msaidizi wa klabu hiyo, Riziki Shawa, amesema kuwa,
wanajua ugumu wa wapinzani wao , lakini wanaandaa mashine za uhakika ili
kuwaadhibi wakiwa mbele ya umati mkubwa wa mashabiki wao.
“Yanga inasifiwa kwa kuwa na nyota wa
kimataifa, lakini mwaka huu kinachowabeba ni bahati tu, mwaka ni wao na ndio
maana wanaweza kupata ushindi hata kama hawajacheza kandanda, sisi tutapambana
nao kufa na kupona ili kupata ushindi”. Alijigamba Kocha Shawa.
Kocha huyo anayeonekana kujiamni
zaidi aliongeza kuwa msimu huu Oljoro kushuka
daraja ni sawa na ndoto za mchana, wamejipanga kushinda mechi zilizosalia
wakianza na mechi ya jumatano.
Wakati huo huo wenyeji wa Oljoro siku
ya jumatano, klabu ya Yanga, inaendelea na mazoezi ya mchezo huo jijini Dar es
salaam huku wachezaji wote wakiwa salama.
Akizungumza leo hii, afisa habari wa
Yanga, Baraka Kizuguto, amesema wanajiandaa kupata ushindi muhimu mbele ya
Oljoro na kuimarisha zaidi harakati zao za kutwaa taji la ligi kuu msimu huu.
“Sisi tunaendelea vizuri na tuna uhakika
wa kufika siku hiyo salama, kikubwa wana Yanga wote tushikamane wakati huu
muhimu wa kulitwaa taji linaloshikiliwa na watani wetu Simba, muhimu kwa kila
shabiki wetu ni kufika uwanja wa taifa jumatano”. Alisema Kizuguto.
Yanga wapo nafasi ya kwanza ya
msimamo wa ligi kuu wakiwa na pointi 49 kibindoni, wakati wapinzani wao JKT
Oljoro wapo nafasi ya nane wakijikusanyia pointi 28.
0 comments:
Post a Comment