
YUSUFU MANJI |
Na Baraka Mpenja, Dar es
Salaam
Baraza la wazee wa mabingwa wa Kombe
la Kagame na vinara wa ligi kuu soka Tanzania bara msimu huu, klabu ya Yanga ya
jijini Dar es salaam, limeumwagia sifa nyingi uongozi wa sasa wa klabu hiyo
chini ya mwenyeki wake milionea Yusuf Manji.
![]() |
AKILIMALI |
Akizungumza kwa furahi nyingi, katibu
mkuu wa baraza hilo,mzee Ibrahim Akilimali, amesema baraza hilo linabariki kwa
moyo mkunjufu mambo yote mazuri
yanayofanywa na mwenyekiti Manji pamoja na baraza la udhamini hususani mpango
wa kujenga uwanja wa kisasa unaotarajia kugharimu bilioni 48 za Kitanzania.
“Tulipokuwa tunafanya Mapinduzi na
kumshinikiza mwenyekiti wa wakati ule mwanasheria Lyod Nchunga, watu walidhani
tunataka madaraka, sisi lengo letu lilikuwa kupata viongozi bora , lakini kwa
sasa tumeridhishwa sana na uongozi wa Manji, tunabariki sana”. Alisema Akilimali.
Mzee Akilimali aliongeza kuwa hali ya
klabu kwa sasa ni shwari, mipango mizuri inayofanywa na viongozi wake imesababisha
baraza la wazee, wanachama na wadau wa klabu hiyo kushikamana zaidi na kuiombea
dua njema.
Katibu huyo alisisitiza kuwa mwenendo wa Yanga kwa sasa
unatoa picha ya kuwa timu bora zaidi siku za usoni, hivyo umoja huo usivurugwe na kikundi chochote au
mtu yeyote , kama itatokea hivyo baraza la wazee litalaani vikali watu hao
wenye maslahi binafsi.
“Viongozi wetu wamerudisha amani
klabuni kwetu, kama atatokea mtu wa kuvuruga uongozi au wachezaji wetu,
tutasimama kidete kukemea ili asitie doa mambo mazuri yanayoendelea kwa sasa”.
Alisistiza Mzee Akilimali.
Akizungumzia mwenendo wa timu na
benchi la ufundi, Mzee Akilimali, alisifu uwezo wa kocha wa sasa Mholanzi Ernie
Brandts ambaye anaonekana kuibadilisha timu kwa kiasi kikubwa, huku akijenga
umoja na mshikamano miongoni mwa wachezaji”. Alisema Akilimali.
Hivi karibuni Yanga imeanika mipango
yake ya kujenga uwanja wa kisasa utakaogharimu zaidi ya biloni 48 za Kitanzania
, na tayari Kampuni ya Beijing Construction ya China imewapelekea ramani tatu
za uwanja huo, kilichobaki na kuchagua moja ili ujenzi uanze mara mambo ya
fedha yatakapokwenda vizuri.
Endapo Yanga itafanikiwa kujenga
uwanja wake, itaepukana na makato yasiyoendana na maandalizi ya mechi pamoja na
kuwapunguzia adhaa ya kuhaha huku na kule kutafuta viwanja vya kufanyia mazoezi
jijini Dar es salaam.

0 comments:
Post a Comment