SIMBA YAPATA NAFASI YA TATU KOMBE LA UHAI
Simba imetwaa nafasi ya tatu katika michuano ya Kombe
la Uhai inayoshirikisha timu zenye umri chini ya miaka 20 za klabu za Ligi Kuu
ya Vodacom baada ya kuitandika Mtibwa Sugar ya Morogoro mabao 3-0.

Hadi mapumziko katika mechi hiyo iliyochezwa leo
asubuhi (Desemba 23 mwaka huu) kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume, Dar es
Salaam, Simba ilikuwa mbele kwa bao 1-0.


Mabao yote ya washindi katika mechi hiyo yalifungwa na
Ramadhan Mkipalamoto. Mfungaji alifunga bao la kwanza dakika ya 43 wakati
mengine alipachika dakika za 57 na 70. Kwa kunyakua nafasi ya tatu, Simba
imeondoka na kitita cha sh. 500,000.
Mechi ya fainali ya michuano hiyo kati ya Azam ya Dar
es Salaam na Coastal Union ya Tanga itachezwa leo (Desemba 23 mwaka huu)
saa 10 jioni kwenye Uwanja wa Kumbukumbu ya Karume.
Mbali ya kombe, bingwa wa michuano hiyo inayodhaminiwa
na kampuni ya Said Salim Bakhresa kupitia maji Uhai atapata sh. milioni 1.5
wakati makamu bingwa atazawadiwa sh. milioni 1.
Timu iliyoonesha zaidi mchezo wa kiungwana (fair play)
itapata sh. 400,000, mchezaji bora wa mashindano sh. 350,000, mfungaji bora sh.
300,000 na kipa bora sh. 300,000. Naye kocha bora katika mashindano hayo
atazawadiwa sh. 300,000 kama itakavyokuwa kwa refa bora.
0 comments:
Post a Comment