MATOKEO ya Sensa ya Watu na Makazi iliyofanyika nchini Agosti 26
hadi Septemba 8 mwaka jana, yameonyesha kuwa idadi ya Watanzania
imefikia milioni 44,929,002.
Rais Jakaya Kikwete ndiye alitangaza matokeo hayo jana jijini Dar es
Salaam na kuwataka Watanzania kupunguza kasi ya kuzaliana.
Akizungumza katika viwanja vya Mnazi Mmoja wakati wa uzinduzi huo,
Rais Kikwete ambaye aliambatana na viongozi mbalimbali wa kitaifa,
alisema kuwa matokeo ya awali yameonyesha kuwa Tanzania Bara ina idadi
ya watu milioni 43,625,434 huku Zanzibar wakiwa 1,303,568.
Alisema kuwa matokeo hayo ni ishara kwamba ifikapo mwaka 2016 kuna
uwezekano wa idadi hiyo kufikia milioni 51 jambo ambalo linaweza kuwa ni
mzigo kwa taifa, jamii na hata katika masuala ya uchumi.
Rais alifafanua kuwa jamii inapaswa kuyachukulia kwa uzito matokeo
hayo hasa katika masuala ya kupanga uzazi pamoja na kuongeza bidii ya
kufanya kazi.
“Mikakati lazima ifanyike sasa kuna umuhimu wa kupanga uzazi;
Watanzania wanapaswa kutambua hilo vinginevyo hali ya maisha itashuka,”
alisema. | DR.KIKWETE |
Rais Kikwete alisema kuwa Watanzania wanapaswa kuongeza nguvu ya
kufanya kazi zaidi kwa kuwa idadi imekuwa kubwa na inaongezeka kwa kasi
kubwa.
“Kupanga uzazi ni jambo la msingi sana na tuzingatie hayo ili kuweza
kupiga hatua maana matokeo hayo yanaashiria idadi ya watu milioni 10
imeongezeka tangu sensa ya mwaka 2002 kufanyika,” alisema.
Alisema kuwa matokeo yatakayofuata yatatangazwa Februari ambapo
yatatoa idadi ya wanaume na wanawake na matokeo mengine kutolewa Aprili
2013.
Rais aliongeza kuwa zoezi hilo linagharimu fedha nyingi lakini
serikali inalazimika kufanya kutokana na kutakiwa kupanga sera na
mikakati ya maendeleo ambapo kwa sensa ya mwaka 2012 imegharimu kiasi
cha sh bilioni 140 na zilizotumika hadi sasa ni sh bilioni 124.
“Hata hivyo ninapongeza kukamilika kwa zoezi hili la awali kwani
kulikuwa na purukushani nyingi na maneno mengi ya kutaka kuvuruga…wapo
walioendesha na kuhamasisha wengine wasusie, wapo waliotaka kuendesha
maandamano wakati wakijua ni wakati wa sensa lakini pamoja na mitihani
yote tumeweza kupata matokeo,” alisema.
Alisema sensa hiyo ni ya tano kufanyika tangu Muungano ambapo ya
kwanza ilifanyika mwaka 1967 na idadi ya watu ilikuwa milioni
12,313,469, bara wakiwa milioni 11,958,654 na visiwani 354,400.
Alisema kuwa sensa ya kwanza ilifanyika mwaka 1910. Sensa nne za
mwisho zilifanyika baada ya Uhuru katika miaka ya 1967, 1978, 1988 na
2002.
Kulingana na sensa ya mwisho iliyofanyika Agosti 2002, idadi ya watu nchini ilikuwa 34,443,603.
Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya
sensa, alisema kuwa mchakato huo ulikabiliwa na changamoto nyingi ikiwa
ni pamoja na watu wanne kupoteza maisha huku wengine wakijeruhiwa.
Alisema kuwa zaidi ya sh bilioni 90 zilitumika kuwalipa vijana
walioajiriwa wakati wa sensa ambapo vijana 200,000 waliajiriwa katika
kuhesabu na 400 wakati wa uchambuzi. | MH. MIZENGO PINDI, WAZIRI MKUU TANZANIA |
Naye Mwenyekiti wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahimu Lipumba,
alisema kuwa hoja aliyoitoa Rais Kikwete ni ya msingi hasa katika suala
zima la kupanga uzazi.
 | prof. IBRAHIM LIPUMBA |
Profesa Lipumba alisema kuwa matokeo hayo pia yanatoa fursa kwa
serikali kuhakikisha inajipanga ili kuhakikisha Watanzania wanapata
ajira.
|
|
0 comments:
Post a Comment