MAKAMU Mwenyekiti wa klabu ya Yanga Clement Sanga amemtambulisha kocha mkuu wa timu hiyo Mzambia George Lwandamina pamoja Mkurugenzi wa ufundi Hans Pluijm mbele ya Waandishi wa Habari mapema asubuhi ya leo makao makuu ya klabu ya Yanga SC.
Lwandamina anachukua nafasi ya Mholanzi Hans aliyebadilishiwa majukumu na kuwa mkurugenzi wa ufundi ili kumsaidia Mzambia huyo katika masuala mbali mbali ya maendeleo ya klabu hiyo.
Sanga alisema kuwa baada ya tetesi za muda mrefu kuhusu ujio wa kocha huyo, sasa ni rasmi baada ya Lwandamina kusaini mkataba wa miaka miwili na vijana hao wa Jangwani ambapo mzunguko wa pili ataongoza kikosi cha Yanga SC kwenye harakati za kutetea Ubingwa wa ligi.
"Uongozi wa Yanga unayo furaha kuwatambulisha kocha mkuu (Lwandamina) na mkurugenzi wa ufundi (Hans) ambao tunaamini kwa pamoja wataweza kuipa mafanikio zaidi timu yetu kutoka hapa ilipo na kusonga mbele zaidi" alisema makamu mwenyekiti Sanga.
Kwa upande wake Lwandamina alisema: "Ni changamoto mpya kwangu najua Yanga ni klabu kubwa nitahakikisha natumia kila kinachowezekana kuhakikisha tunafanya vizuri kuanzia kwenye ligi ya nyumbani hadi klabu Bingwa Afrika.
Naye Mkurugenzi wa Ufundi mpya wa klabu hiyo Hans van der Plujin alisema:" Sina shida na majukumu yangu mapya kikubwa nipo Yanga na nitaendelea kutimiza majukumu yangu kwa mujibu wa mkataba wangu na nitapambana na kushirikiana vyema na Mwalimu George pamoja na wachezaji na benchi zima la ufundi kuhakikisha tunatetea ubingwa wetu na kufika mbali kimataifa"
0 comments:
Post a Comment