Manchester United leo wanawakaribisha Bournemouth kwenye dimba la Old Trafford katika mchezo wa funga dimba wa Ligi Kuu England msimu wa 2015-16.
Mashetani hao wekundu kwa sasa wana uwezekano mkubwa wa kukosa nafasi ya kushiriki michuano ya Mabingwa Ulaya kwa mara ya pili ndani ya misimu mitatu mara baada ya kukubali kipigo cha mabao 3-2 dhidi ya West Ham katikati ya wiki.
Endapo Manchester City leo atapata japo sare tu basi atakuwa amekata tiketi ya kufuzu hata kama United atashinda kutokana na kuwa na mtaji mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa.
Ripoti mbalimbali zinaeleza kuwa, Manchester United watapoteza kiasi cha Yuro milioni 30, pesa inayotokana na matangazo endapo watashindwa kufuzu kwenda Ligi ya Mabingwa msimu ujao.
Vijana hao wa Louis Van Gaal kwa sasa wanashika nafasi ya tano, alama mbili nyuma ya mahasimu wao Manchester City.
Kwa upande wao Bournemouth maarufu kama 'The Cherries' wako salama kabisa na janga la kushuka daraja huku wakiwa na pointi nane juu ya wahanga wa kushuka daraja.
The Cherries, ambao wameshinda mchezo mmoja tu kati ya saba iliyopita ya ligi, waliifunga Manchester United 2-1 wakati walipokutana kwa mara ya kwanza mwezi desemba mwaka jana.
Kauli za makocha kueleka mchezo wa leo
Meneja wa Bournemouth Eddie Howe anasema: “Ni jambo zuri sana kuona tunacheza mchezo ambao kwa kiasi fulani unaamua mustakabali wa timu mojawapo.
“Michezo kadhaa iliyopita ilikuwa migumu sana kwetu kwa sababu tumekuwa sio timu ambayo imekuwa na mechi nyingi za ushindani
“Kwenye misimu kadhaa iliyopita tulikuwa na umakini wa hali ya juu kwa sababu kila mchezo kwetu ulikuwa na maana kubwa sana na ndiyo maana tuliweza kuendana na presha ya ya mashindano.”
Meneja wa Manchester United Louis van Gaal: “Kwa sasa tumebaki na tegemeo moja tu, si lingine bali ni kuangalia matokeo ya Manchester City kwa siku ya leo,”
“Hilo ni jambo la kusikitisha sana kwa sababu tulikuwa na nafasi wakati tukiwa bado tuna michezo miwili kabla ya ligi kumalizika, lakini tulishindwa kuitumia vyema. Mpaka zikiwa zimebaki dakika 15 kabla mpira kumalizika dhidi ya West Ham, tulikuwa tukiongoza mabao 2-1, lakini tuliishia kupoteza mchezo huo kwa mabao 3-2, si jambo zuri kwetu kutegemea matokeo ya timu nyingine lakini hatuna jinsi lazima tufanye hivyo.”
Taarifa muhimu za kila timu.

Matteo Darmian anatarajia kukosekana kwenye mchezo wa leo kwa upande wa United, kutokana na kusumbuliwa na maumivu ya kifundo cha mguu (ankle injury), wakati Luke Shaw anatarajiwa kurudi msimu ujao.
“Bahati mbaya Januzaj amepata majeraha wakati wa mazoezi, hivyo atakosekana katika mchezo wa leo.’’Van Gaal amesema.
‘’Ashley Young anaweza kuwepo, tumefanya naye mazoezi leo (jana) na maendeleo yake ni mazuri.”
Bournemouth kwa upande wao hawana majeruhi yeyote mpya lakini meneja Eddie Howe amesema kwamba anaweza kufanya 'rotation' ya kikosi chake leo.
Mlinzi Sylvain Distin na Adam Smith wote kwa pamoja watakuwa nje wakiuguza majeraha yao ya mgongo na henia, wakati Tokelo Rantie (anayesumbuliwa na misuli) and Tyrone Mings (goti) pia watakosekana kwenye mchezo wa leo.
Utabiri wa vikosi vyote.

Bournemouth: Boruc, Cook, Daniels, Francis, Elphick, Surman, Stanislas, Ritchie, Gosling, Gradel, King, Federici, Wiggins, O’Kane, MacDonald, Pugh, Grabban, Wilson.
Manchester United: De Gea, Romero, Valencia, Jones, Smalling, Blind, Rojo, Borthwick-Jackson, Fosu-Mensah, McNair, Herrera, Schneiderlin, Carrick, Depay, Pereira, Lingard, Mata, Rashford, Rooney, Martial.

Manchester United wameshinda michezo sita kati ya saba ya mwisho ya ligi waliyocheza kunako dimba la Old Trafford,na kutoka sare mmoja.
Bournemouth wamejiwekea kibindoni pointi nne tu kati ya 21 na wameshinda mechi nyingi zaidi za ugenini ambazo ni sita dhidi ya tano walizoshinda wakiwa katika dimba la nyumbani.
United wameruhusu magoli machache zaidi zaidi ya timu yoyote kwenye ligi ya England msimu huu kwenye uwanja wa nyumbani (magoli 8) wakati Bournemouth wakiruhusu magoli 64 msimu huu – ni Aston Villa pekee ndio wamewazidi ambao wameruhusu magoli 72.
Ni Leicester City pekee ndio wamejikusanyia pointi nyingi zaidi katika uwanja wa nyumbani msimu huu zaidi ya United. Wamejinyakulia pointi 42 huku United wakipata pointi 38.
0 comments:
Post a Comment