KOCHA Mkuu wa Yanga, Hans van der Pluijm ameanza kuwatafutia kombinesheni kali washambuliaji wa timu hiyo, Donald Ngoma na Paul Nonga, ili waweze kufunga mabao Ligi Kuu Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika mwakani.
Nonga alianza mazoezi jana kwenye Uwanja wa Boko Veterani jijini Dar es Salaam, baada ya kujiunga na klabu hiyo katika dirisha dogo la usajili wa Ligi Kuu Bara lililofungwa Desemba 15 mwaka huu akitokea Mwadui.
Mazoezi hayo yaliyofanyika asubuhi kwa saa tatu kujiandaa dhidi ya Mbeya City ambao watacheza Jumamosi kwenye Uwanja wa Taifa jijini Dar es Salaam, Pluijm alitumia muda mwingi kusaka kombinesheni ya wachezaji wa zamani na wapya waliosajiliwa hivi karibuni.
Wachezaji hao ni Nonga na Issoufou Boubacar Garba waliosajiliwa katika dirisha dogo, ambapo Pluijm alionekana kutafuta kombenisheni ya kuwachezesha pamoja na Ngoma, Amis Tambwe na Malimi Busungu.
Pluijm alionekana kutotaka mzaha baada ya kutumia dakika 30 kuwapa somo wachezaji wake, kabla ya kuanza kwa programu kamili katika mazoezi hayo.
Kocha huyo alianza kuwakimbiza kwa kasi kutoka kuzunguka koni zilizopangwa nusu ya uwanja huo kwa lengo la kuwaweka fiti zaidi kabla ya kuvaana na Mbeya City.
Baada ya mazoezi hayo, Pluijm alitumia dakika 20 kuwapa mbinu za kiufundi zitakazowawezesha kupata ushindi katika kila mechi mbalimbali ikiwemo ya Mbeya City.
0 comments:
Post a Comment