Kesho Jumapili Yanga inacheza mechi ya kirafiki na Mbeya
City kwenye Uwanja wa Sokoine, Mbeya katika kujiandaa na msimu ujao wa Ligi Kuu
Bara na Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika kikosi cha Yanga, yumo kiungo
mshambuliaji Deus Kaseke aliyesajiliwa hivi karibuni kutoka Mbeya City, ambaye
angeweza kuutumia mchezo huo kuwaaga wachezaji wenzake.
Pengine Kaseke angecheza kipindi cha kwanza akiwa Mbeya City
kisha kipindi cha pili akacheza Yanga kama alivyofanya Geoffrey Mwashiuya pindi
timu yake ya zamani ya Kimondo ilipocheza na mabingwa hao watetezi wa ligi kuu.
Kaseke amesema kuwa, haoni sababu ya kuichezea Mbeya City
kwani tayari yeye ni mchezaji wa Yanga na hawezi kuichezea timu nyingine.
“Nicheze Mbeya City? Hapana, nitacheza Yanga kwa dakika zote
tena kwa kiwango changu kilekile, watu wasitarajie kwamba nitazitumikia timu
zote kwa vipindi tofauti. Waelewe tu kuwa mimi ni mchezaji wa Yanga.
“Wachezaji wengi hasa wa kimataifa wamekuwa wakifanya hivyo,
lakini kwangu sijafikiria,” alisema Kaseke ambaye amejihakikishia namba kwenye
kikosi cha Yanga.
Akizungumzia mchezo huo, Kocha wa Mbeya City, Juma Mwambusi,
alisema: “Nilikuwa Dar es Salaam, ndiyo narudi Mbeya sasa (jana), nitaiandaa
timu kesho (leo Jumamosi) kwa mechi hiyo.”
Katika mchezo huo, Yanga inatarajiwa kuwatumia nyota wake
wengine wapya akiwemo Donald Ngoma, Thabani Kamusoko, Malimi Busungu, Simon
Matheo, Benedict Tinocco na Haji Mwinyi.
Chanzo: Championi
0 comments:
Post a Comment