Kocha Mkuu wa Simba, Muingereza, Dylan Kerr, amesema
anahitaji wachezaji wake kucheza soka la pasi za harakaharaka wanapokuwa na
mpira wakati wanashambulia lango la timu pinzani.
Kauli hiyo aliitoa mara baada ya kumalizika kwa mechi ya
kirafiki ya kimataifa dhidi ya SC Villa iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa
jijini Dar es Salaam wikiendi iliyopita na Simba kushinda kwa bao
1-0.
Hiyo ni mechi ya sita kocha huyo kukaa kwenye benchi la Simba tangu apewa
kibarua cha kukinoa kikosi hicho kinachojiandaa na Ligi Kuu Bara.
Soka hilo la pasi za haraka haraka wakati timu ikiwa na
mpira, linatumiwa sana na klabu ya Barcelona ya nchini Hispania.
Kerr amesema bado kikosi chake kinahitaji marekebisho kabla
ya kuanza kwa ligi kuu, yakiwemo ya kucheza soka la kupiga pasi za haraka wanapomiliki
mpira.
Kerr alisema tatizo hilo la timu yake kutocheza soka la pasi
za haraka, ameliona kwenye mechi tano za kirafiki walizozicheza ikiwemo dhidi
ya KMKM, Polisi Zanzibar na Taifa Jang’ombe, zote za kirafiki.
“Bado wachezaji wangu hawajaushika mfumo ninaoutaka wa
kucheza soka la pasi za haraka wakati tukiwa na mpira sisi tukishambulia kwenye
goli la timu pinzani.
“Hivyo nimepanga kulifanyia kazi hilo kuhakikisha timu
inacheza soka lile ninalolihitaji ambalo ninaamini kama wachezaji wangu wakilizoea,
basi timu yangu itapata ushindi.
“Kwa mfano mechi hii dhidi ya SC Villa ya Uganda
tulivyocheza utaona wachezaji wangu walikuwa wanakaa na mpira muda mrefu bila
ya kupigiana pasi kwa wakati, hivyo ninataka kuona timu yangu inacheza soka la
aina hiyo,” alisema Kerr.
Source: Salehjembe

0 comments:
Post a Comment