MABINGWA wa Kandanda Tanzania bara, Young Africans wanatarajia kuanza mazoezi ya ufukweni mwishoni mwa juma hili ikiwa ni maandalizi ya kombe la Kagame linalotarajia kuanza Julai 11 mwaka huu jijini Dar es salaam.
Mkuu wa kitengo cha habari na Mawasiliano wa Yanga, Jerry Muro amesema kwamba kikosi chao kinaendelea na mazoezi uwanja wa Karume tangu mwanzoni mwa wiki hii chini ya kocha, Hans van der Pluijm, lakini bado wachezaji wengi wapo na timu zao za Taifa wakicheza mechi muhimu za kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika, AFCON 2017.
Hata hivyo, Muro amezungumzia suala la wachezaji wa Kigeni ambapo amebainisha kwamba wameshawapata, lakini wanashindwa kuwasainisha kwasasa kwani bado mapendekezo ya kuongezea idadi ya wachezaji wa kigeni hayajajibiwa na TFF.
"Wachezaji wengi tuliozungumza nao wanaonekana kuipenda Yanga na wanatamani kuja Yanga, tunasubiri majibu ya mapendekezo yaliyotumwa na klabu TFF kuomba kuongezewa idadi ya wachezaji wa kigeni kutoka watano mpaka angalau 10. Kwasasa tuna wachezaji watano wa kigeni, tunapata kigugumizi tumuache nani".
Pia Muro amesema safari hii wanaangalia wachezaji kutoka mataifa yaliyopiga hatua kisoka na ikiwezekana watakwenda mpaka ulaya.
"Tumetoa kipaumbele kwenye mataifa yale ambayo yanaonekana yamekaa vizuri kisoka, tunaangalia Zimbabwe, Afrika Magharibi, Afrika kaskazini, ikiwezekana tutaangalia na Ulaya pia kwasababu nia tunayo, sababu tunayo na uwezo tunao. Hatushindwi kufanya hivyo pale ambapo maelekezo ya benchi la ufundi yatataka tufanye hivyo".
0 comments:
Post a Comment