Kocha mkuu wa timu ya taifa ya Uganda 'The Cranes', Sredojevic Milutin ‘Micho’, amesema bado ana imani kubwa na timu yake kuibuka na ushindi dhidi ya Taifa Stars, mchezo utakapoigwa usiku wa leo katika dimba la Amaan visiwani Zanzibar.
"Kucheza ugenini sio sawa na unapokuwa nyumbani. Mara nyingi mnakuwa na msukumo mkubwa sana kutoka kwa timu pinzani kutokana na kuwa na sapoti kubwa kutoka kwa mashabiki wao hasa ukizingatia wao wapo nyumbani. Lakini yote kwa yote nina uhakika wachezaji wangu watarudi nyumbani wakiwa na uso wa bashasha na tabasamu”, Micho, ambaye pia aliing'oa Tanzania katika hatua kama hii ya kufuzu CHAN alitanabaisha.
Mserbia huyo amewajumuisha wachezaji watano wenye asili halisi ya ushambuliaji katika kikosi cha wachezaji 18 ambacho tayari kipo Zanzibar tayari kwa pambano hilo. Taarifa zilizopo ni kwamba Micho atatumia mfumo wa kushambulia zaidi huku pande zote akitumia winga wenye asili ya ushambuliaji wa kati.
Hassan Wasswa Mawanda, nahodha wa timu hiyo ana uwezekano mkubwa wa kuchezeshwa kama beki wa kati huku akishirikiana bega kwa bega na ama Derrick Tekkwo au Kezironi Kizito katika eneo hilo nyeti kabisa.
Mshambulizi mwandamizi, Robert Sentongo ataongoza safu ya ushambuliaji ya 'The Cranes' huku nahodha msaidizi, Farouk Miya akisimama kama namba tisa vilevile Yasser Mugerwa au Muzamiru Mutyaba akisambaza sumu eneo la kiungo.
Mchezo wa marudiano kati ya mahasimu hawa wawili utapigwa wiki mbili zijazo katika dimba la Nelson Mandela, Namboole jijini Kampala
Mshindi atakayepatikana kati ya timu hizi, atavaana na ama Sudan au Kenya kabla ya kuelekea nchini Rwanda ambapo michuano hii ya CHAN mwaka huu ndipo itakapofanyika.
Michauno ya CHAN ni michuano ya mataifa Afrika kwa wachezaji wanaocheza ligi za ndani za nchi zao.
0 comments:
Post a Comment