Beki wa kushoto wa Yanga na Taifa Stars, Oscar Joshua
OSCAR Joshua kwasasa ndiye mlinzi wa kushoto chaguo la
kwanza katika klabu ya Yanga na mbadala wake ni Edward Charles.
Joshua hana kasi, hawezi kusaidia timu kushambulia, hivyo
Yanga wameamua kutafuta mlinzi wa pembeni mwenye uwezo wa kulinda, kushambulia
na kufunga magoli. Ni nani huyo? Jibu ni Mwinyi Hajji kutoka KMKM.
Mwinyi alisainishwa jana mkataba wa miaka miwili kuitumikia
Yanga na ndipo mtandao huu umeamua kumtafuta katibu mkuu wa Yanga, Dr. Jonas
Tiboroa kutaka kujua sababu za kumchukua nyota huyo.
Je, Yanga wamemsajili Mwinyi kuwa mbadala wa Oscar Joshua?
Dr. Tiboroa anajibu: “Kwa muda mrefu hatujaweza kuwa na
mchezaji namba 3 mwenye uwezo kama wa Mwinyi. Sio uwezo wa kulinda tu bali
kuweza kushambulia na kufunga magoli”.
“ Kumbuka huyu kijana licha ya kuwa mlinzi ndiye mfungaji
bora wa KMKM. Tuliona ana faida kwenye timu yetu na kuweza kumsajili”.
“Tumetumia muda mwingi sana kumchambua na kumuangalia,
tumefanya kazi hiyo kwa takribani miezi mitano, sasa tukaona ni wakati mzuri wa
kumsajili”.
Swali: Usajili wa Mwinyi unatoa ishara gani kwa Oscar
Joshua?
Dr. Tiboroa: Ni kumsukuma Oscar Joshua aweze kuwa mzuri
zaidi ya sasa, narudia tena, timu yoyote iliyopo kwenye kiwango alichopo Yanga
inahitaji kuwa na wachezaji zaidi ya wawili kwenye nafasi moja, tena wenye
kiwango kizuri, wanaoweza kucheza nafasi zaidi ya moja. Lengo letu ni kuendelea
kuimarisha timu, iwe na nguvu zaidi ya mwaka mwaka jana.
Swali: Yanga imekamilisha usajili wa Deus Kaseke, Benedictor
Tinocco na Mwinyi Hajji. Wachezaji hawa ni vijana wadogo, je, umefika wakati wa
Yanga kuamini vijana?
Dr. Tiboroa: Kilichosababisha kusajili vijana ni falsafa ya
timu na namna inavyocheza mpira. Inahitaji kuwa na wachezaji wenye kasi, hupati
mwendo kasi kutoka kwa mtu mwenye umri mkubwa, ndio maana tunachukua vijana. Kumbuka
vijana kwenye mpira unaweza kumwambia shika waya wa umeme, akashika kwasababu
ana nia ya kufanya kitu fulani. Yanga kwasasa tunachukua vijana, lakini sio
vijana tu, tunataka vijana wapambanaji watakaoifanya Yanga ishinde.
0 comments:
Post a Comment