Real Madrid na FC Barcelona ndio wanaonufaika zaidi na haki
ya matangazo ya televisheni nchini Hispania
Na Shaffih Dauda
KWA wanaofuatilia mpira wa miguu kwa ukaribu zaidi
wanafahamu stori kubwa ya mgomo wa chama cha wachezaji Hispania (Players Union),
wakipinga muswada uliopelekwa Serikalini na bodi ya ligi, LFP ( ( Liga Nacional
de Fútbol Profesional), chombo kinachoendesha soka la Hispania.
Muundo wa soka la Hispania kama wa Bongo vile, Ligi kuu (La
Liga) na ligi daraja la kwanza (Segunda division) zipo chini ya Bodi ya Ligi.
LFP na serikali wameleta muswada katika makubaliano ya haki
za matangazo ya televisheni wakitaka makubaliano yafanyike kwa pamoja kama ligi
kuu England, lengo lao ni kuongeza ufanisi kwa kuzinufaisha timu zote kuliko ilivyo
sasa ambapo klabu zinakubaliana zenyewe na makampuni yanayorusha moja kwa moja ‘Laivu’
mechi za ligi kuu na ligi daraja la kwanza.
Kinachotokea Hispania ni kwamba, FC Barcelona na Real Madrid wana ushawishi na mvuto
mkubwa, wanafuatiliwa sana, hivyo makampuni mengi hivi sasa yanavutiwa kuingia
mikataba na klabu hizo mbili, matokeo yake nusu ya pesa inayolipwa kwa ajili ya
haki za matangazo ya televisheni inachukuliwa na miamba hii ya soka nchini
humo.
Madhara yake ni kwamba klabu hizi mbili zimekuwa na msuli
mkubwa wa fedha kuliko klabu nyingine na ili kuweza kupunguza pengo lililopo,
serikali ambayo inanufaika pia na haki za matangazo ya Telesheni kwasababu
wachezaji wanalipa kodi imeona ni bora kubadilisha mfumo.
Mishahara inapoongezeka kwa wachezaji, kodi nayo inaongezeka, ili kuongeza pato,
serikali inaona ni bora kuwepo na makubaliano ya pamoja katika haki za
matangazo ya Televishei wakiamini wanaweza kuzisaidia klabu nyingine za chini
ili ziweze kupata ‘mzigo’ wa maana na kuweza kulipa mishahara ya maana kwa
wachezaji ambao wanalipa kodi serikalini.
Lakini kilichosababisha mgomo unaoendelea hivi sasa ni kutoshirikishwa
kwa chama cha soka Hispania kwenye huo mpango unaosimamiwa na serikali ya
Hispania na chombo huru kinachoendesha ligi yaani Bodi ya Ligi (LFP).
Chama kimeamua kusimamisha michezo yote mpaka pale
watakapokaa meza moja na serikali pamoja na FLP kwa lengo la kutetea maslahi
yao kwasababu katika mgao mpya uliokuja unaonesha chama cha soka kina mgao wa
asilimia 4 ya jumla ya fedha zote zinazotokana na haki za matangazo ya
televisheni na wameona ni kidogo.
Zaidi chama kinaona
kimepunjwa kwenye ule mchakato wa awali na wanaamini kama wangeshirikishwa wangekuwa
na hoja za msingi za kuwafanya waweze kupata mzigo wa maana.
Lakini upande wa pili, chama cha wachezaji (Players Union) kimeungana
na chama cha soka kupinga muswada huo wakisema kuna baadhi ya vipengele vitakavyoendelea
kuwanyonya wachezaji.
Wanapointi mbili, mosi; pamoja na gawio ambalo baadaye
watakuja kupata pamoja kwa maana ya klabu za ligi kuu na daraja la kwanza, bado
timu za Segunda division zitapata kiasi kidogo cha fedha ambazo haziwezi kusaidia.
Pili; wale wachezaji wa Ligi kuu (La Liga) wakiangalia vipengele
vya pamoja kwenye mgawanyo mpya wa haki za Matangazo, hawaoni nafasi ya klabu
za chini kupata hela ya maana na matokeo yake wachezaji wa chini hawatanufaika
na mfumo huu mpya.
Pia wachezaji hao wanaocheza ligi kuu wanasema ule mgawanyo
mpya utawaathiri wao kwasababu hauongezi pato kwa klabu zao zaidi ya
kutengeneza mazingira ya pesa nyingi kwenda serikalini.
Wanaamini kama watakubali mfumo huo itafika mahali klabu
zitapunguza mishahara yao kwasababu pato litapungua ikiwa ni matokeo ya utaratibu
mpya ambao watu wengi wanaamini ndio suluhusisho la uchumi wa soka la Hispania
katika ngazi ya klabu. Kutokana na sababu hizo wameamua kugoma kwenda kujadili
muswada huo mpaka pale ambapo baadhi ya vipengele vitakapoangaliwa upya.
Kutokana na suala hili kuna jambo muhimu la kujifunza ukija
katika mchakato wa huku kwetu Tanzania. Mkataba wa haki za Matangazo ya Televisheni
walioingia Azam TV na bodi ya ligi kuu (TPLB) unakufanya ujifunze kirahisi kuwa
kuna rushwa ilitembea, huhitaji kwenda shule ili kufanya uchunguzi kugundau
kuwa rushwa ilitembea wakati wa mchakato wa kusainiwa kwa mkataba ule.
Katika hali ya kawaida, haiwezekani kwamba klabu zote zipate
gawio sawa kutokana na haki za matangazo ya televisheni (Milioni 100 kutoka
Azam TV).
Huu mgogoro unaondelea Hispania baina ya chama cha soka, chama
cha wachezaji, bodi ya ligi na serikali unatufumbua macho sisi tuliopo dunia ya
mbali ili walau tuweze kujifunza. Ingawa si kwa kufuata kila kitu kwasababu
wenzetu wameendelea sana, lakini ni muhimu kupata maarifa machache ambayo
tunaweza kuyatumia katika mazingira ya kwetu kwa lengo la kupata tija katika
soka letu.
Cha kwanza, kwa muundo wa bodi ya ligi kuu ya kwetu
inayohusisha ligi kuu na ligi daraja la kwanza, timu zote za ligi kuu na ligi daraja
la kwanza zinatakiwa kunufaika na haki za matangazo ya Televisheni kwasababu mkataba unasainiwa kati ya bodi ya ligi na
Televisheni (Azam TV) ambayo inaundwa na timu za ligi kuu na ligi daraja la
kwanza.
Haiwezekani kila mapato yanayopatikana katika bodi
yasizihusu klabu za ligi daraja la kwanza, yaani sawasawa na wewe una watoto wa
kuwazaa nyumbani kwako na watoto wa mjomba au Shangazi, unapika chakula, lakini
ikifika wakati wa kupakua msosi unawaambia watoto wa Shangazi au mjomba kwamba ‘chakula
hiki hakiwahusu’.
Watoto wote wanaishi kwenye familia moja (timu za ligi kuu
na daraja la kwanza), ingawa watoto wako wa kuwazaa wanaweza kunufaika zaidi,
lakini lazima watoto wengine wanufaike pia kwa kiasi fulani.
Kitu walichotufumbua macho Hispania ni kwamba; mikataba yote
wanayoingia Bodi ya ligi kuu, klabu za ligi daraja la kwanza zihusishwe wakati
wanakwenda kufanya mazungumzo ya haki za matangazo ya Televisheni kwasababu nao
ni sehemu ya wanachama wa bodi.
Lazima zihusishwe kwa maana ya maamuzi ya pamoja katika haki
za matangazo. Kwa mfano Azam TV kwa kutotambua wanaweza kutumia fedha nyingi kuingia mkataba wa ligi kuu na ligi daraja la
kwanza, kumbe wao wana haki ya kukubaliana kwa pamoja kwasababu wanafikia
makubaliano na bodi ya ligi na sio klabu moja moja. Kama wangekuwa wanakubaliana
na timu moja moja, wangeweza kuchagua Simba, Yanga na Azam.
Kwa vile wanakubaliana na bodi ambayo inajumuisha klabu za
ligi kuu na ligi daraja la kwanza, Azam TV wao wanatakiwa kuja na fedha ya
pamoja, halafu bodi wao ndio wanakaa chini kutengeneza gawio la pesa kwa klabu
za ligi kuu na daraja la kwanza.
Kwasababu klabu za ligi kuu mechi zao zinaoneshwa nyingi
wanaweza kupata asilimia 90 na klabu za ligi daraja la kwanza zipate asilimia
10 kwa kuwa mechi zao zinaoneshwa
chache.
Kingine cha kujifunza ni nguvu ya wachezaji katika mikataba,
kwa mfano chama cha wachezaji cha soka la Hispania kinagoma kucheza kwasababu
wanaona vipengele vilivyomo katika mkataba vikisainiwa bila chombo chao kuhusishwa
kitawaathiri wao moja kwa moja katika mazingira makuu mawili,
Kwanza ule mkataba ukisainiwa, mapato yao kwa maana ya
mishahara na bonasi vitapungua kutokana na klabu kushuka kimapato.
Pili; mfumo huu haujengi mazingira mazuri kwa hawa ambao
tunasema hawana kitu (timu za segunda division). Utaratibu mpya hauji kuwafanya
wapate zaidi bali unakuja kuwadidimiza. kwahiyo wao kama chama cha wachezaji
wameungana na chama cha soka kugoma kwasababu kwenye huo mkataba hakuna mazingira ya wao
kama wahusika wakuu kunufaika.
Ukija kwetu Bongo ukilinganisha na haya yanayofanyika
Hispania, kumbe hata hii mikataba wanayoingia bodi ya ligi, wachezaji nao wanatakiwa
kuwa na chama chao kinachoweza kuungana kugomea vipengele vya mikataba vinavyowanyonya
wao.
Chama cha wachezaji kinatakiwa kuwa na wanasheria, wataalamu
ambao wanaingia kwenye vikao na kuwasilisha maslahi ya wachezaji. Haimaanishi Jonas Mkude kuwa mchezaji wa Simba, basi Simba
wana mamlaka yote ya kufanya chochote, lazima kuwepo mipaka, uhusiano wa klabu
na mchezaji upo uwanjani kwa kufunga magoli na kucheza dakika 90, lakini
linapokuja suala la maslahi pamoja na biashara linaangalia kwa jicho lingine,
wachezaji wanatakiwa kuwa na watu wanaowasimamia.
Mchezaji lazima naye apate stahiki yake katika mikataba inayosainiwa,
ukiangalia wachezaji wa ulaya kama Cristiano Ronaldo, klabu yake ya Real Madrid
ina mkataba na kampuni ya Adidas kwa ajili ya kuwavalisha jezi wachezaji,
kwasababu Ronaldo anachezea timu ambayo ina mkataba na Adidas basi analazimika
kuvaa jezi ya Adidas, lakini mchezaji halazimishwi kuvaa kiatu cha Adidas
kwasababu mguu ni wake mwenyewe.
Ndio maana Ronaldo anavaa kiatu cha Nike kwasababu ana
mkataba nao binafsi kama mchezaji. Akiwa katika mazingira ya nje ya klabu
anavaa nguo za Nike, akiwa anafanya mkutano na waandishi wa habari unaomuhusu
yeye na mambo yake anavaa nguo ya Nike, lakini akiwa anafanya kwa kuiwakilisha
klabu, anavaa nguo za klabu ambazo ni Adidas.
Hii maana yake ni kwamba, wachezaji wana nguvu, wana nafasi kubwa kwa kila kinachofanywa na klabu
au chombo chochote kinachosimamia mpira na kuingiza pato kwa kumuhusisha yeye.
Ndio maana wacheza nchini Hispania wanaamua kugoma kwasababu
ule mkataba unawaathiri moja kwa moja na wanaona wakiingia mkataba huo mpya
mapato yao yatashuka kwasababu klabu badala ya kupata kwa mfano milioni 100
sasa itapata milioni 70.
Kama klabu itashusha kimapato, maana yake itarudi huku chini
kukata baadhi ya gharama za uendeshaji ikiwemo kupunguza mishahara kutokana na
chanzo mojawapo cha mapato kupungua (haki za matangazo ya Televisheni).
Wachezaji wa Kibongo wajitambue kwa kuangalia wachezaji wa
Hispania walivyoanzisha mgomo wakitetea maslahi yao bila kujali kama muswada
ule una faida au hapana. Wao wanatumia wataalamu wao ambao wapo kwenye chama
chao, wanatetea maslahi yao, wanawaeleza kuwa humu ndani ya mkataba kuna
vipengele ambavyo keshokutwa vitawaathiri ninyi moja kwa moja, wao kama wawakilishi wa chama hawakubaliani na
vipengele hivyo na wamewataka wachezaji kutumia nguvu yao kugoma.
Kibongobongo, tunapoelekea kusaini mikataba mipya, lazima tukubali
kutumia wataalamu wenye uelewa wa kujadiliana kuhusu haki za matangazo ya
Televisheni ili watetee maslahi ya klabu
pamoja na wachezaji.
Klabu ziwe na chombo chao chenye watu wenye uelewe, ambao
wanakwenda kutetea maslahi ya klabu. Pia wawepo viongozi wa klabu wanaotetea
maslahi ya wachezaji.
Kilichopo Bongo, ‘Third Part” kwa maana ya makampuni
wanapata urahisi kwasababu viongozi wengi wa mpira hawaendi kutetea maslahi ya
klabu wala wachezaji, wapo kwa ajili ya
kutetea maslahi yao na ndio maana unakuta madhamini anakuja anasaini mkataba
rahisi kwasababu wanaokwenda kufanya mazungumzo ya mkataba hawana taaluma
yoyote, wanarubuniwa kirahisi kwa kupewa hela (rushwa) ili waweze kukubali matakwa ya makampuni ya
udhamini na kuridhia kusaini mikataba
ambayo wadau na wataalamu wa soka wanaona ni ‘Bomu’.
Nawatakia siku njema!
0 comments:
Post a Comment