‘Azam FC ilitwaa ubingwa wa VPL msimu wa 2013/14 bila kupoteza mechi hata moja ukiwa ni msimu wake wa saba Ligi Kuu.’
AZAM FC imekuwa klabu ya mfano kwa maendeleo ya soka la Tanzania kutokana na uwekezaji wake wa mabilioni ya shilingi katika mchezo huo.
Mara kadhaa Rais wa Tanzania, Jakaya Kikwete, amekuwa akiitolea mfano anapozungumzia ustawi wa michezo, hususani mpira wa miguu unaoongoza kwa kuwa na wapenzi wengi nchini na ulimwenguni kwa ujumla.
Wamiliki wa klabu hiyo wamewekeza kikamilifu katika soka kwa kujenga miundombinu ya kisasa vikiwamo viwanja, hosteli za wachezaji na vifaa vingine rafiki kwa maendeleo ya soka.
Hata hivyo, nia njema ya familia ya Said Salum Bakhresa (SSB) katika kuhakikisha klabu hiyo inakuwa mfano wa kuigwa nchini na kimataifa katika ustawi wa soka, inaonekana kutaka kuharibiwa na watu ambao binafsi ninaona wanataka kuirudisha kulekule ambako klabu kongwe nchini, Simba na Yanga zilijikwaa.
Kwa miaka mingi Simba na Yanga zimekuwa zikibadilishana kutwaa taji la Ligi Kuu Tanzania. Tangu ligi hiyo ianzishwe 1965, Yanga imetwaa taji mara 25 wakati watani wao wa hadi, Simba wametwaa mara 18.
Licha ya kutwaa ubingwa wa Bara mara nyingi zaidi, timu hizo kongwe zaidi nchini zimekuwa hazifanywi vyema katika michuano ya kimataifa, jambo ambalo limekuwa likizua hofu kwamba huenda zinatwaa ubingwa wa Bara kwa njia sizizo halali.
Msimu wa 2013/14 Azam FC ilifanikiwa kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) kwa kuzipiku klabu hizo kongwe, lakini imeshindwa kufanya vyema katika michuano ya kimataifa ikishiriki Kombe la Shirikisho mara mbili na Klabu Bingwa Afrika mara moja.
Sababu ya kuchemsha kwa Wanalambalamba katika anga za kimataifa haihitaji uende Chuo Kikuu kuielewa. Bado haijaiva kupambana katika michuano ya kimataifa kutokana na uchanga wake kisoka. Ikumbukwe kuwa Azam ilipanda VPL 2007. Imepataje mafanikio haya makubwa ya kutwaa taji la Ligi Kuu ndani ya miaka saba tangu kupanda kwake?
Wanaofuatilia kwa kina VPL, watakubaliana na mimi kwamba udhaifu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) katika kupanga ratiba ya ligi ni miongoni mwa sababu kuntu zinazosababisha kuibuka kwa minong'ono ya baadhi ya wadau wa soka kuhusu upatikanaji wa mabingwa wa ligi hiyo.
Mathalani, wakati Azam FC inatwaa ubingwa wa VPL msimu wa 2013/14 bila kupoteza hata mechi moja, ratiba ya ligi hiyo ilikuwa na mchango mkubwa kwa klabu hiyo kufanya vyema.
Kikosi cha Wanalambalamba kiliuanza msimu huo kwa kucheza mechi tatu mfululizo ugenini dhidi ya Mtibwa Sugar (Turiani), Rhino Rangers (Tabora) na Kagera Sugar (Kagera).
Hadi mzunguko wa kwanza unamalizika Novemba 9, 2013, Azam ilikuwa imebakisha mechi tatu za nje ya jiji la Dar es Salaam (mzunguko wa pili) dhidi ya Mgambo Shooting (Tanga), Ruvu Shooting (Pwani) na Mbeya City (Mbeya). Kwa nini TFF ilipanga ratiba ya aina hiyo?
Msimu uliomalizika juzi Azam na Yanga ndizo timu zilizoiwakilisha Tanzania Bara katika michuano ya kimataifa. Azam iling'olewa katika hatua ya kwanza dhidi ya El-Merrikh ya Sudan, lakini inashangaza kuona timu hiyo ya Chamazi ilikuwa na mechi nyingi za kiporo.
Azam pia imekuwa na migogoro kadhaa ya ndani ya klabu, ambayo wakati mwingine imekuwa ikiathiri timu, lakini ni mara chache kuona, kusikia au kusoma katika chombo cha habari nchini kikiambia ukweli Azam FC kuhusu mambo yasiyofaa katika ustawi wa mpira wa miguu.
Mwaka jana, ni tahariri moja pekee katika magazeti ya Tanzania iliyoikosoa Azam FC. Tahariri hiyo iliandikwa katika gazeti la NIPASHE ikiponda kitendo cha uongozi wa Azam FC kusafiri kwa basi kwenda Uganda kucheza mechi za kirafiki nchini humo ilhali ilikuwa na muda mfupi kujiandaa kwa mechi ngumu dhidi ya Yanga.
Ninakumbuka uongozi wa Azam FC ulifanyia kazi suala hilo na kuamua kuisafirisha timu kwa ndege badala ya basi kutoka Uganda kurejea Dar es Salaam na kupata sare ya mabao 2-2 dhidi ya Yanga katika mechi hiyo iliyochezwa kwenye Uwanja wa Taifa Desemba 28.
Si kila kitu kinachofanywa na Azam FC ni sahihi. Kutokana na ukweli huo, ninafikiri ipo haja kwa klabu hii changa kuambiwa ukweli pale inapokosea ili irudi katika misingi sahihi ya uendeshaji wa soka.
Miongoni mwa wadau wachache wa soka niliowahi kuwasikia wakiikosoa Azam FC, ni nyota wa zamani wa Yanga, Sunday Manara, ambaye aliwahi kukosoa utaratibu wa klabu hiyo kusajili wachezaji wanaoachwa na Simba na Yanga.
"Azam itashindwa kufikia malengo yake, kama ikiendelea kusajili 'mitumba' ya Simba na Yanga. Wawekeze katika kituo chao cha soka kwa kuibua na kulea vijana wenye vipaji," alisema Manara.
Kama Manara ameweza kuikosoa Azam FC, kwa nini isiwe TFF? Kwa nini visiwe vyombo vya habari vya Tanzania?
IMEANDIKWA NA SANULA ATHANAS, MWANDISHI WA MICHEZO MWANDAMIZI WA GAZETI LA NIPASHE.
CHANZO: NIPASHE

0 comments:
Post a Comment