'Yanga inahofia kufanyiwa fitina na wapinzani wao nchini Tunisia.'
IKIWA ni sawa na ilivyokuwa katika mechi ya pili dhidi ya FC Platinum nchini Zimbabwe, Yanga wameamua kusafiri na chakula pamoja na maji yao kwenda nchini Tunisia kuivaa Etoile Sportive du Sahel (ESS).
Yanga, mabingwa mara 25 wa Tanzania Bara, watarudiana na mabingwa hao wa zamani wa Kombe la Shirikisho na Klabu Bingwa barani Afrika katika mechi ya hatua ya 16 bora ya michuano ya Kombe la Shirikisho mwaka huu nchini Tunisia Jumamosi.
Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Yanga, Jery Muro, ameuambia mtandao huu jijini hapa leo kuwa kikosi chao kinaondoka leo usiku kwa ndege ya kibiashara ambamo wataweka pia chakula, maji na vyombo vya kulia watakapokuwa Tunisia.
"Kwa kifupi, hatutatumia kitu chochote cha wapinzani wetu tutakapokuwa nchini Tunisia. Makamu Mwenyekiti wetu, Clement Sanga, tayarui yuko Tunisia akiandaa mahali ambapo timu itafikia na watu watakaoipokea timu uwanja wa ndege," amesema Muro.
TELELA KUWAKOSA ESS
Aidha, kiungo fundi Salum Telela, ataikosa mechi ya Jumamosi kutokana na majeraha. Kiungo huyo aliumia baada ya kukwatuliwa na mshambuliaji wa City, Themi Felix katika mechi ambayo walishinda 3-1 Uwanja wa Taifa jijini hapa wiki juzi.
Yanga inayonolewa na Mdachi Hans van der Pluijm, inahitaji ushindi au sare ya mabao 2-2 au kushinda katika matuta baada ya sare ya 1-1 ili ifuzu katika hatua inayofuata.
0 comments:
Post a Comment