Viongozi wa Azam FC, kutoka kushoto waliokaa ni Idrissa Nassoro (Katibu Mkuu), Saad Kawemba (CEO) na aliyesimama ni Said Mohamed (Mwenyekiti)
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
'Yanga SC na Azam FC ndizo zinakimbizana kuwania ubingwa wa Ligi Kuu ya Bara msimu huu.'
USHINDI mnono wa mabao 8-0 ambao Yanga SC uliupata jana dhidi ya Coastal Union FC, umezua balaa kwa mabingwa watetezi Azam FC baada ya viongozi wa klabu hiyo ya Chamazi jijini hapa kurushiana maneno makali kutokana na timu yao kuambulia sare katika mechi iliyopita.
Yanga SC, mabingwa mara 24 wa Tanzania Bara, waliwachambanga bila huruma kwa kuwachapa kipigo cha mbwa mwizi cha mabao 8-0 mabingwa wa 1988 wa Tanzania Bara, Coastal Union FC Uwanja wa Taifa jana wakati wapinzani wao katika mbio za ubingwa msimu huu, Azam FC wakilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Mbeya City FC Uwanja wa Azam jijiji hapa jana pia.
Kwa matokeo hayo, Yanga SC imepanua wigo wa pointi kati yake na mabingwa hao watetezi kutoka pointi nne kabla ya mechi ya jana hadi pointi sita baada ya mechi, ingawa Azam FC wana mechi moja mkononi.
Baada ya mechi ya Azamn FC dhidi ya City kumalizika, viongozi wawili wa wanalambalamba; Jemedari Said, meneja wa timu na Saad Kawemba, Ofisa Mtendaji Mkuu (CEO) wa klabu, walianza kutupiana maneno makali, tena hadharani, yaani kweupe.
Katika mahojiano na mtandao huu leo mchana, Jemedari amesema kilichotokea kati yake na bosi wake ni sehemu ya changamoto za kazi na kimemalizwa kimpira maana kilikuwa tukio la kisoka.
"Kulitokea kupishana lugha, si unajua tena tulikuwa tumepata matokeo ambayo hayakuwa mazuri. Siwezi kueleza alichoniambia hadi tukafikia hatua hiyo kwa sababu ni masuala ya ndani ya klabu," amesema Jemedari.
Alipotafutwa na mtandao huu kuelezea kilichotokea hadi wakafikia hatua ya kutoleana lugha chafu mbele za watu, Kawemba, mkurugenzi wa zamani wa mashindano wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), amesema Jemedari alichanganywa na matokeo ya mechi mbili za jana (Yanga dhidi ya Coastal na Azam FC dhidi ya City).
"Nilimwambia afanye jambo fulani kwa ajili ya maandalizi ya timu kwenda Morogoro leo, lakini akajibu tofauti na nilivyotarajia," Kawemab amesema na kuongeza:
"Huenda matokeo ya jana yaliwaumiza watuy fulani kuzidi watu wengine. Ninafikiri alihitaji muda zaidi baada ya matokeo hayo kabla hajatumwa kufanya kazi ya klabu ndiyo maana alivyojibu ovyo, nikatoa kwa mtu mwingine jukumu nililokuwa nimepanga kumpa.
"Kilichotokea kitajadiliwa na uongozi ndani ya vikao vyetu. Ripoti ya mechi itawasilishwa kwa uongozi, hivyo kila kitu kitajadiliwa huko.
"Timu inaondoka leo kwenda Morogoro kujiandaa kwa mechi dhgidi ya Mtibwa. Tumeambulia sare katika mechi iliyopita, si mbaya ingawa wenzetu wamefanikiwa kupata ushindi baada ya kutuombea njaa. Nasi tutapambana kuupa ushindi huku tukiwaombea njaa," amesema zaidi Kawemba.


0 comments:
Post a Comment