'JKT Ruvu Stars ilishinda 2-1 dhidi ya Stand United FC katika mechi ya mzunguko wa kwanza wa ligi ya Bara msimu huu iliyochezwa Uwanja wa Azam jijini Dar es Salaam Januari 10 mwaka huu.'
KATIKA kuhakikisha haitelemki daraja, Stand United FC imetamba kuendeleza kilio kwa kocha mzawa Felix Minziro kwa kukichapa kikosi chake cha JKT Ruvu Stars katika mechi pekee ya leo ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezzwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga.
Stand wameshinda mechi zote mbili zilizopita nyumbani dhidi ya Mtibwa Sugar FC na Polisi Moro FC na leo Mkurugenzi wa Ufundi wa timu hiyo pekee katika ligi ya Bara kutoka Shinyanga msimu huu, Muhibu Kanu, amesema wameweka lengo la kushinda mechi zote za nyumbani zilizobaki kabla ya kumalizika kwa msimu huu Mei 9.
"Tuna kikosi kizuri kwa sasa ambacho kinaweza kufanya lolote kwa muda wowote. Tunasubiri muda ufike ili tuchukue pointi tatu kutoka kwa maafande wa JKT Ruvu. Tunatambua mechi itakuwa ngumu kutokana na matokeo ya wapinzani wetu katika mechji zilizopita," amesema Kanu.
JKT Ruvu Stars imekuwa na matokeo mabovu katika mechi za karibuni ikipoteza mechi zote mbili zilizopita dhidi ya Ruvu Shooting na Coastal Union. Pia ilifungwa na Yanga SC na kutoka suluhu dhidi ya Ndanda FC katika mechi nyingine za karibuni.
Kikosi cha Minziro kinajivuania uwapo wa mshambuliaji wake hatyari msimu huu, Samwuel Kamuntu mwenye mabao saba, lakini Stand nao wana mshambuliaji hatari kutoka Nigeria, Abasirim Chidiebere ambaye tayari ameshaziona nyavu mara nane, hivyo kuifanya mechi hiyo Na. 156 kuwa ngumu kutabiri mshindi kwa timu hizo ambazo bado ziko hatarini kuporomoka daraja.
Stand United FC inayonolewa na kocha mkuu Mganda Mathias Lule, iko nafasi ya nane katika msimamo wa ligi ikiwa na pointi 27 baada ya mechi 21 wakati JKT Ruvu iko nafasi ya tatu kutoka mkiani ikiwa na pointi 24 baada ya mechi 22.


0 comments:
Post a Comment