Kocha wa Mbeya City fc, Juma Mwambusi (kushoto)
BAADA ya kuwafunga Simba 2-0 jana uwanja wa Sokoine, kocha Juma Mwambusi wa Mbeya City amesema mechi ya Simba dhidi ya Kagera Sugar iliyochezwa Kambarage Mnyama akishinda 2-1 aliitumia kuisoma Simba na kuandaa mkakati madhubuti uliompa pointi tatu.
Mwambusi amevuna pointi 6 msimu huu kutoka kwa Simba kwani mechi ya kwanza januari 28 mwaka huu Mbeya City ilishinda 2-1 uwanja wa Taifa.
Msimu ulioita, timu hizi zilitoka 2-2 uwanja wa Taifa kabla ya kutoka 1-1 uwanja wa Sokoine.
Mwambusi anasema: "Kabla ya mchezo na Simba niliwaambia wachezaji wangu umuhimu wa kupata pointi tatu nyumbani, tulipoteza mechi na Yanga katika mazingira tofauti kwa hali ya hewa na mambo mengine, nikawaambia kikubwa tuko nafasi ambayo si nzuri katika msimamo wa ligi, tunahitaji kutoka nafasi za chini. Niliwaambia mechi ya kwanza kupata pointi tatu nyumbani ni kuanzia ya Simba, wametekeleza nilichowaagiza, nawapongeza sana"
"Nasema hata nafasi ya tatu au nne naweza kupata kwasababu timu bado hazijaachana sana, kama nilivyosema mwanzo wa ligi kwamba msimu huu utakuwa mgumu kwasababu tulishapiga bunduki na watu wakajua tuko wapi, kila mechi kwetu ni ngumu, lakini nikasema angalau tumelize tano bora"
"Nilishawaona Simba walipocheza na Kagera Sugar, nilijua nini tunaweza tukafanya na kikatusaidia, niliweka wachezaji wengi katikati na tulitawala na tulimuweka Nonga (Paul) peke yake mbele, tukipanga mashambulizi kutoka nyuma tunajua kule mbele kuna mtu mzuri,
nilishawaona Simba nikaingia na mpango B (Plan B) na tumeweza kuchukua pointi tatu".


0 comments:
Post a Comment