SASA maji yamezidi unga! unaweza kusema hivyo kutokana na Mtibwa Sugar kuhangaika kutafuta njia ya kukwepa mkasi wa kushuka daraja.
Mpaka kufikia mwishoni mwa mwaka jana Mtibwa Sugar walikuwa wanaongoza ligi na walipokwenda kucheza michuano ya kombe la Mapinduzi na kufika fainali wakifungwa na Simba kwa penalti, mambo yamekuwa magumu ligi kuu.
Wamekuwa wakifungwa mechi nyingi na kutoka sare na mara moja moja kushinda kwa mbinde.
Mpaka sasa wapo mstari mwekundu, wanashika nafasi ya 12 katika ya timu 14 za ligi kuu wakijikusanyia pointi 23 katika mechi 20 walizocheza.
Mwishoni mwa wiki iliyopita walifungwa goli 1-0 na Stand United na kabla ya mechi hiyo walifungwa 2-1 na Kagera Sugar katikati ya wiki iliyopita, mechi zote zilichezwa CCM Kambarage, Shinyanga.
Afisa habari wa klabu hiyo, Tobias Kifaru ameuambia mtandao huu kuwa sasa mambo yamekaa sawa kuelekea mechi ijayo kwa wamepewa maneno (mashairi) mazito kwa lengo la kuwaongezea morali.
Mtibwa Sugar itaikaribisha Azam fc katika mechi ya ligi kuu jumamosi ya wiki hii uwanja wa Manungu Complex.
"Tunakutana na Azam kwetu, ni mchezo mgumu, lakini morali ni kubwa kwa wachezaji. Tumekaa nao na kuwaeleza kuwa wanalo jukumu la kuinusuru timu isishuke daraja, itakuwa aibu kwao wanapoenda timu nyingine, kila mtu anawacheka kwa kuishusha timu"
"Wameonesha kuguswa na maneno mazito ya kocha na viongozi, wameahidi kupambana vikali dhidi ya Azam fc". Amesema Kifaru.


0 comments:
Post a Comment