Wakili Dkt. Daniel Ndumbaro
SHIRIKISHO la soka Tanzania limetuma taarifa kwa
vyombo vya habari jioni ya leo kuwa kamati ya rufani ya nidhamu ya Shirikisho
hilo imekutana leo (Aprili 12 mwaka huu) kujadili rufani ya Wakili Dkt. Damas Daniel
Ndumbaro aliyefungiwa miaka saba na TFF kujihusisha na shughuli za soka.
Katika kikao hicho imeelezwa kuwa TFF
iliwakilishwa na wakili wake Emmanuel Muga wakati Dkt. Ndumbaro hakufika wala
kuwakilishwa na wakili wake, hivyo kamati chini ya mwenyekiti wake Revocatus
Kuuli imeazimia kutuma wito tena kwa Ndumabaro.
Mtandao huu umemtafuta wakili maarufu Dkt.
Ndumbaro kutaka kujua kwanini hakufika mbele ya kamati.
Ndumbaro amekanusha kuwa hana taarifa yoyote ya
wito kutoka TFF kuhusiana na kikao cha kamati ya nidhamu.
Aidha Ndumbaro ameongeza kuwa hata alipomuuliza
katibu muhtasi wake (secretary) naye amesema hajaletewa taarifa yoyote wito
kutoka TFF.
“Lakini nina imani na mwenyekiti wa kamati ya rufaa
ya nidhamu ambaye ni muadilifu kwa maana ya kwamba ametoa fursa ya kutuma wito
mwingine kwake”. Amesema Ndumbaro na kuongeza, “Hii inaonekana wazi kuwa TFF
ilipanga suala liamuriwe kwa upande mmoja , wakili wa TFF alikuwepo, lakini
upande wa Utetezi wangu haukupewa taarifa yoyote juu ya kikao”.
TAARIFA ILIYOTUMWA KWA VYOMBO VYA HABARI JIONI YA
LEO HII HAPA;
Kamati ya Rufaa ya Nidhamu - TFF imekutana leo
tarehe 12/04/2015 kujadili rufaa No. 1/2014 ya DR. DAMAS
NDUMBARO dhidi ya TFF.
TFF iliwakilishwa na Wakili Msomi Emmanuel Muga na
Dr. Ndumbaro hakufika wala hakuwakilishwa na wakili wake.
Kufuatia kutofika kwa Dr. Ndumbaro, Kamati, kwa
Azimio moja, iliamuru TFF itoe wito mpya na mpaka tarehe 14/04/2015 uwe
umemfikia Dr. Ndumbaro, ukimfahamisha tarehe ya kikao kijacho cha kusikiliza
rufaa yake.
Imetolewa na Mwenyekiti,
REVOCATUS KUULI
MWENYEKITI WA KAMATI
12/04/2015.


0 comments:
Post a Comment