
Na
Oswald Ngonyani
Mwezi Mei mwaka 2012, Didier Drogba, aliiihama klabu
yake aliyoichezea kwa mahaba makubwa klabu ya Chelsea baada ya kuichezea kwa
muda wa miaka minane.
Ulikuwa uamuzi ulioonekana kuwasononesha mashabiki
wengi wa ‘The Blues’ na hata baadhi yao kujikuta wakikumbwa na fadhaiko, tena
fadhaiko kuu ndani ya mioyo yao.
Nakumbuka
wakati akiihama Chelsea, alitajwa kuwa mchezaji bora zaidi wakati wa mechi ya
fainali ya kuwania kombe la klabu bingwa barani Ulaya (UEFA) ambapo Chelsea,
iliibuka na ushindi dhidi ya Klabu ngumu ya Bayern Munich ya nchini Ujerumani.
Katika
mchezo huo wa fainali mwanamume huyu aliyezaliwa miaka 36 iliyopita huko
Abidjan nchini Ivory Coast alifunga penalti ya mwisho na kuipa Chelsea ushindi
wake wa kwanza katika fainali hizo.


Baada
ya kandarasi yake na Chelsea kumalizika, mchezaji huyo mwenye sifa ya kutumia
nguvu zaidi dimbani aliamua kujiunga na klabu ya Shanghai Shenhua inayoshiriki
katika mechi za ligi kuu nchini Uchina.
Ripoti
zinasema kuwa Drogba alijiunga na klabu hiyo baada ya kusaini mkataba wa pauni
elfu mia mbili kwa wiki na tayari aliifanyia makubwa klabu hiyo kwa kuifungia
magoli mara kwa mara katika kila mchezo aliokuwa amepangwa.
Umaarufu
aliouonyesha Drogba, wakati wa fainali ya kombe la klabu bingwa barani Ulaya
mjini Munich, Ujerumani, ulimpa heshima zaidi na wanazi wengi wa The Blues
duniani kote.
Heshima
kama hiyo aliipata pia barani Afrika baada ya kuiwezesha timu yake ya Taifa ya
Ivory Coast kutinga mpaka katika hatua ya fainali ya AFCON 2012 lakini kwa
bahati mabaya hawakuchukua ubingwa mbele ya wenyeji Zambia.
NYAKATI ZENYE MACHUNGU
ZAIDI ZA DROGBA KATIKA TIMU YAKE YA TAIFA
Drogba
ambaye jina lake halisi ni Tébily Didier Yves Drogba alikiongoza kikosi hicho
cha Ivory Coast kufikia fainali ya mashindano hayo kwa mara ya pili yaani mwaka
2012.
Kama
ilivyokuwa katika fainali ya mashindano hayo nchini Misri, miaka nane
iliyopita, fainali hiyo iliamuliwa kwa njia ya penalti. Katika mechi hiyo,
Zambia ambayo haikutarajiwa na wengi kushinda, ilivunja ndoto ya Drogba ya
kushinda kombe hilo na timu yake ya taifa.
Kwa
Drogba hilo lilikuwa pigo kubwa mno na kamwe hatakuja kulisahau asilani. Katika
nyakati zake zote za Unahodha wa Timu ya Taifa hajapata bahati ya kutwaa
ubingwa huo, katika awamu tofauti alionekana kujidhatiti sana kwa dhati ya moyo
wake lakini alishindwa kabisa kukidhi haja ya uhitaji wake.

KUHUSU UFALME WAKE PALE
DARAJANI
Wakati
alipokuwa akiichezea Chelsea hususan katika misimu ya mwaka 2004 mpaka mwaka
2012 Drogba alifunga zaidi ya magoli 150 na kucheza takriban mechi 350. Alishinda
kombe la ligi kuu ya Premier mara tatu, kombe la FA mara nne na kombe la ligi
mara mbili.
Mwezi
Oktoba mwaka 2012 mashabiki wa Chelsea walipiga kura ambapo aliibuka kuwa
mchezaji bora zaidi kuwahi kusajiliwa na klabu hiyo tangu ilipoanzishwa.

Drogba
aliwahi kushinda taji la BBC la mchezaji bora barani Afrika mwaka wa 2009 na licha
ya kukumbwa na maswaibu katika maisha yake, Drogba hakupoteza muda na nafasi
aliyopata alijikakamua na kuwa mmoja wa wachezaji bora zaidi kutoka Afrika.
Kujituma
kwake ndani ya dimba kumemfanya aheshimike zaidi katika mawanda ya soka la
England lakini pia katika mawanda ya soka la Afrika na duniani kwa ujumla.
ALIVYOPOKELEWA KWA MIKONO
MIWILI STAMFORD BRIDGE NA MWALIMU WAKE KIPENZI JOSE MOURINHO
Pamoja
na maisha ya soka kumuendea vema sana nchini China, Ujio wa Kocha wake wa
zamani, Kipenzi chake Jose Mourinho pale darajani ulimfanya arudi tena kucheza
Ligi kuu ya England EPL huku akipewa nafasi zaidi na Kocha wake huyo, nafasi
ambayo mpaka sasa ameonekana kuitendea haki na hata kuwaridhsisha mashabiki
wake.
Ukongwe
wa umri wake ulionekana kuwatisha mashabiki wengi wa Chelsea, lakini Jose
Mourinho alionekana kuona mbali zaidi na kuwataka mashabiki hao kutokuwa na
hofu kuhusu Drogba.

Hata
yeye Drogba alionekana kuridhishwa sana na uamuzi wake wa kurudi katika klabu
yake ya zamani, klabu aliyoitumikia kwa mahaba makubwa kuliko.
Nakumbuka mara baada ya kusaini mkataba wake
wa mwaka mmoja wa kuitumikia klabu hiyo alizungumza maneno machache yaliyokuwa
na maana kubwa sanaa:
“Yalikuwa
maamuzi rahisi nisingeweza kupoteza nafasi ya kufanya kazi tena na Jose. Kila
mtu anajua mahusiano mazuri niliyokuwa nayo na klabu hii, na mara zote nimekuwa
nikijisikia kama nyumbani”.
“Hamu
yangu bado ni ile ile na naangalia mbele kuisaidia timu hii. Namefurahia sana
ukurasa huu mwingine wa maisha yangu ya soka”.
Naye Mourinho aliwaondoa hofu mashabiki wa
klabu hiyo akisisitiza kuwa Muivorycost huyo bado ni mshambuliaji bora katika
ulimwengu wa soka.
“Amekuja
kwa sababu ni miongoni mwa washambuliaji bora Ulaya. Namjua sana na najua kuja
kwake kutamfanya ayafanye yale makubwa aliyowahi kuyafanya klabuni miaka ya
nyuma”, Alisema Mourinho.

Drogba ambaye katika fainali za sasa za AFCON
2015 hakuwepo katika kikosi cha Taifa cha Ivory Coast baada ya kustaafu aliiangalia
timu yake kupitia Televisheni ambapo Tembo hao wanaoongozwa na mchezaji bora wa
Afrika, kiungo Yaya Toure walifanikiwa kuutwaa ubingwa wa AFCON, ubingwa ambao
walikuwa wameumisi sana.
Atakumbukwa kutokana na uwezo wake ndani ya
dimba, uwezo ambao kwa kiasi kikubwa uliiwezesha timu yake ya Taifa kucheza
fainali ya AFCON katika awamu mbili tofauti lakini pia uwezo wake huo kwa kiasi
kikubwa ulichagiza timu yake ya Chelsea kufanya vema katika mashindano ya ndani
na nje ya England.
Naomba kutamatisha.
Unapenda
kuwa Mkufunzi wa mchezo wa soka? Nunua sasa Kitabu cha ‘SIRI YA SOKA’ Uweze
kuwa na uelewa zaidi katika mchezo huo, Wasiliana na Mwandishi wa Makala haya
kwa simu namba 0767 57 32 87 ili kuweza
kujipatia nakala ya Kitabu hicho.
0 comments:
Post a Comment