
Yanga na Simba ndio timu zinazobeba taswira ya soka la Tanzania
Na Oswald Ngonyani
KATIKA vitu ambavyo nchi ya Tanzania imebarikiwa
ni pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wapenda michezo hususan mchezo wa soka.
Lakini pamoja na kuwa na idadi kubwa ya wanazi na
mashabiki wa mchezo huo kwa bahati mbaya sana watanzania walio wengi wanaonekana
kuihususudu zaidi soka ya nje kuliko soka yetu watanzania.
Pengine kunaweza kukawa na sababu lukuki za
watanzania wengi kuwa na utamaduni huu lakini miongoni mwa sababu ambazo zipo
wazi zaidi ni Ubora wa Ligi za wenzetu, Ligi ambazo kwazo zipo imara kutoka
ngazi ya Uongozi wa juu mpaka kwa Uongozi wa timu husika.
Mbali na suala la uongozi, pia uwezo wa hali ya
juu unaooneshwa na wachezaji na vilabu husika ni sababu nyingineyo ambayo kwa
kiasi kikubwa imewafanya wadau na wanazi wengi wa soka la bongo kuwa wafuasi
wakubwa wa soka ya Ulaya, soka ambayo kila leo inazidi kujiongezea idadi ya
mashabiki.
Wakati fulani nilikuwa ninawaza kuhusu hawa
wachezaji tulio nao sasa, Je ni kweli kabisa uwezo wao ni wa chini sana hata
washindwe kuleta ubora katika ligi zetu mbalimbali hasa Ligi Kuu ya Vodacom?
Je ni kweli Viongozi tulio nao ndiyo haswa sababu
ya soka letu watanzania kuzidi kurudi nyuma badala ya kusonga mbele kama ilivyo
kwa wenzetu kule Ulaya na kwingineko?
Je, Uongozi wetu wenye dhamana ya mpira wa miguu
nchini (TFF) ni kweli ndiyo chanzo cha madudu haya yanayoonekana kutokea kila
leo katika soka la bongo?
Azam fc inaaminika kuwa klabu yenye mtazamo mpya katika sola la Tanzania
Pengine kila mwanafamilia ya mchezo wa soka
atakuwa na jawabu lake kuhusu maswali haya niliyouliza. Mimi naweza
nikasema mfumo mbovu wa kiutendaji ndani ya Ligi ndiyo sababu ya madudu haya
yanayojitokeza kila leo, lakini mwingine anaweza akasema mambo mengine ambayo
pia yanaweza yakawa sababu ya soka letu kuzidi kuwa na uswahili mwingi.
Kwa siku za karibuni Ligi yetu imeonekana
kuboreshwa sana na wadhamini wake, na wengi walidhani kuwa baada ya maboresho
hayo pengine ustahimilivu na ubora wa Ligi yetu vingezidi kujipambanua lakini
kwa bahati mbaya ni kama tunazidi kudorora.
Kasi ya wachezaji wetu kwenda kufanya majaribio
(trials) ughaibuni wala haipo tena. Wanandinga wetu wameonekana kutokuwa na
mipango thabiti kuhusu kutafuta maslahi yao hata nje ya mipaka.
Wapo wapo tu, wala hawaeleweki. Leo hii ukiwauliza
wachezaji wengi wa soka la bongo kuhusu malengo yao kwa siku za baadaye kuhusu
Uanasoka wao, wengi watakujibu majibu ambayo yanawiana.
Kucheza Simba, Yanga au Azam ndizo ndoto za
wachezaji wetu hawa, na wale ambao tayari wapo katika vikosi hivi vya timu
kubwa na zinazolipa vizuri, wamekwishabweteka na wala hawaiwazii kesho yao
kunako mustakabali wa kutengeneza pesa kupitia vipaji vyao.

Mbeya City fc ni timu yenye mtazamo wa kisasa ingawa bado ni changa
Wakati mwingine sioni sababu sana ya kuwashangaa
mashabiki wa mchezo wa kandanda hapa nchini kuamua kujikita zaidi katika soka
la Ughaibuni, pengine wamekwishaona kariba ya wachezaji wetu wengi, wachezaji
ambao soka yao ni ile ile, wala haileti hamasa kuitazama.
Wachezaji wetu wanacheza mchezo unaofanana karibu
kila kitu. Katika michezo kumi ambayo utafuatilia kwa umakini hutaweza kugundua
vipaji vya ziada walivyonavyo wachezaji wetu hawa.
Mtibwa Sugar ni moja ya timu zilizokaa muda mrefu katika ligi ya Tanzania bara
Asilimia kubwa ya wachezaji tulio nao wanacheza
mpira wa “Mam’bomba” yaani aina ya mpira wa kubutua butua, mpira ambao hata mtu
asiyekuwa na’idea’ ya mchezo wa soka anaweza akafanya hivyo.
Yaani kuucheza mpira katika minajili ya ‘bora
liende’.
Ni jambo linalotia hasira sana lakini hakuna namna
nyingine kwani haya yote yanayotokea katika soka la sasa yapo kwa sababu ya
vile mfumo wetu ulivyo.
Wachezaji wetu hawajipi nafasi ya kuwafuatilia
wachezaji wenzao wanaocheza soka la kulipwa kule Ulaya.
Wachezaji ambao wanaupa heshima kubwa mpira, hii
ni kutokana na ukweli kuwa kupitia soka wanaweza kuyaendesha maisha yao tena
kwa mafanikio makubwa.
Wanafanya vema pale wanapopata nafasi ya
kusajiliwa timu fulani lakini pia pale wanapopata nafasi dimbani. Si watu wa
kubweteka kama ilivyo kwa wachezaji wetu.
Ndio maana wachezaji kama Cristiano Ronaldo na
Lionel Messi siku zote wanaonekana kuwa bora na hata kuukwaa uchezaji bora wa
dunia mara kwa mara hii inatokana na heshima wanayoitoa katika mchezo huu.
Hawana dharau, wala hawawezi kubweteka kwa sababu
ya mafanikio waliyo nayo sasa.Wanaendelea kujibidiisha tena na tena kwa lengo
la kukidhi haja ya uhitaji kwa mashabiki wao kitu ambacho wachezaji wa
Kitanzania wamekishindwa.
Soka la bongo michosho mitupu. Soka la bongo
linakinaisha na kwa kiasi kikubwa linakera tena linakera sana. Viongozi
wanaongoza soka pasipo kufuata misingi stahiki ya kiuongozi.
Wachezaji nao hali kadhalika, wala hawaoneshi
kuiheshimu kazi yao hiyo. Wapo wapo tu wala hawana tofauti na watu
wengine.Viongozi wa timu nao wana hulka zilezile, hulka za kutojitambua za
kuongoza timu katika minajili ya bora liende.
Kwa staili hii ni lazima tutapunguza mashabiki na
hata kuwapa mwanya wakuwa wafuasi wakubwa wa soka ya nje, vinginevyo ni lazima
Viongozi husika wafanye kazi ya ziada ili kuifanya Ligi yetu kuwa bora zaidi,
lakini pia wachezaji wetu wanatakiwa kuwatendea haki mashabiki wao tofauti na
ilivyo sasa.
MIMI YANGU MACHO
(0767 57 32 87)
0 comments:
Post a Comment