
Na Bertha Lumala, Dar es Salaam
Mabingwa mara 19 wa Tanzania Bara, Simba SC wameshindwa kusafiri kwenda usukumani mjini Shinyanga kuwafuata Stand United FC kwa ajili ya mechi yao ya mwishoni mwa wiki.
Simba SC itakuwa na kibarua kigumu itakapowavaa wapigadebe hao katika mechi ya mzunguko wa pili ya Ligi Kuu Tanzania Bara itakayochezwa Uwanja wa CCM Kambarage mjini Shinyanga Jumapili.
Msemaji wa Simba SC, Humprey Nyasio ameuambia mtandao huu muda mfupi uliopita kuwa kikosi chao kimeshindwa kwenda Kanda ya Ziwa leo kutokana na mipango ya benchi lao la ufundi.
"Ilikuwa tusafiri kwenda Shinyanga leo, lakini imeshindikana kutokana na mipango ya Kocha Mkuu (Goran Kopunovic). Ameongeza programu moja ya mazoezi, hivyo timu imefanya mazoezi kwa siku mbili leo," amesema Nyasio.
"Kesho tutasafiri kuwafuata wapinzani wetu, habari njema kwetu ni kwamba hatuna majeruhi na wachezaji wote wapo kambini," amesema zaidi ofisa huyo.
Simba SC ililazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Stand United FC katika mechi ya mzunguko wa kwanza iliyochezwa Uwanja wa Taifa jijini hapa Oktoba 4 mwaka jana.
Stand United FC inayoshiriki kwa mara ya kwanza Ligi Kuu msimu huu, iliifunga mabao 4-1 Mgambo Shooting katika mechi iliyopita Uwanja wa CCM Kambarage huku Simba SC ikishinda 2-0 dhidi ya Polisi Moro mjini Morogoro Jumapili.
Simba SC yenye pointi 20 baada ya kucheza mechi 14, inakamata nafasi ya nne katika msimamo wa ligi hiyo yenye timu 14 wakati Stand yenye pointi 15 baada ya mechi 15, iko nafasi ya 12.

0 comments:
Post a Comment