
Wachezaji wa Simba sc wakishangilia bao la Ramadhan Singano 'Messi' jana Simba ikiitandika Gor Mahia 3-0 uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
ZAMANI mtu anayeitwa Baba katika familia alikuwa
mtu wa kuogopwa na watoto na pengine hata mke wake wa ndoa.
Kutokana na ufalme huo, akina Baba walikuwa
wanatamba na kuvimba kichwa pale wanapoogopwa na wakigundua watoto hawana uogo
kwao, walidhani hawaheshimiwe.
Baba anaporudi nyumbani kutoka matembezini, watoto
hukimbia kwenda kulala mara wasikiapo sauti yake nje.
Baadhi ya watu walidhani kuwa ukali ni njia
mojawapo ya kulea familia katika ubora, lakini walio wengi walishindwa kufikia
malengo kwasababu watoto wao walishindwa kuwa huru.
Kuwa mkali sana pale mtoto anapofeli mtihani sio
suluhisho la kumfanya afaulu. Hakuna kitu kibaya kama kufanya kitu ukiwa katika
usimamizi mkali au hofu ya kufeli.
Kama upo kwenye chumba cha mtihani na unawaza
jinsi baba atakavyokuchapa ukifeli, basi utakuwa na presha ya mtihani na
utashindwa kufanya vizuri.
Kufeli na kufaulu kupo kwa ajili ya wanafunzi,
hutakiwa kuwaza kufaulu tu wakati kufeli pia kupo.
‘Udingi’ ni tatizo kubwa sana hasa ulimwengu huu
wa utandawazi. Siku hizi U-baba bora unaopendwa na watoto ni kuwa mpole na
kujua namna ya kuzungumza nao pale wanapokosea.
Busara ikitawala katika mazungumzo yako, basi una
asilimia kubwa ya kuwavutia watoto wako na wakafanya kile unachotaka.
Hata katika mpira wa miguu, zamani makocha wengi
walikuwa wanaendekeza ‘udingi’. Kuwashauri ilikuwa ngumu na uhusiano na
wachezaji ulikuwa wa Baba na mtoto.
Mfano aliyekuwa kocha wa Brazil, Luiz Felipe
Scolari ana ‘udingi’ mwingi. Hashauriki, haambiliki na hata wachezaji wake
wanamuogopa kwasababu hajajirahisisha kwao.
Kutokana na tabia hii, Scolari amejikuta akifeli
katika soka la kisasa. Siku hizi makocha wanaofanikiwa ni wale wenye mahusiano
na wachezaji kama ‘washikaji’.

Leo atapitishwa TFF?: Emmanuel Okwi alikuwa chachu ya mabao ya Simba jana
Ikitokea tatizo wanalitatua kirafiki tu, na wakati
mwingine mchezaji anamchukulia kocha wake kama jamaa yake tu. Anakuwa na uhuru
wa kuomba kitu, kushauri kitu na hata kueleza mambo yake binafsi.
Makocha wanakuwa kama walezi na wanawapanga
wachezaji kisaikolojia. Kutokana na hili wachezaji wanajikuta ni marafiki wa
makocha wao na kazi inafanyika vizuri.


Kuna aina ya makocha huwa ni wakali kupindukia.
Hataki kuona mchezaji anakosea, lakini wanajisahau kuwa mpira wa miguu ni
mchezo wa makosa.
Mfano ni aliyekuwa kocha wa Simba, Mcroatia,
Zdravko Logarusic maarufu kama Loga. Huyu jamaa kama ulibahatika kumuona katika
mazoezi yake na hata wakati wa mechi, alikuwa hana uvumilivu, na ukali wake
uliwafanya wachezaji wawe wanyonge mno.
Mchezaji anaingia uwanjani, lakini fikira zake
zote zipo katika kukwepa makosa.
Unaweza kuona Ramadhani Singano ‘Messi’, Amiss
Tambwe yuko nafasi nzuri ya kufunga na anatakiwa kujaribu kupiga shuti, lakini
anatafuta sehemu ya kupeleka mpira kwasababu sababu anaogopa kumuudhi Loga.
Ukikosea muda huo huo unakwenda kukalia ‘benchi’
a.k.a gogo.Lakini kumbe mpira hauko hivyo, hutakiwa kuogopa kukosea, fanya
ufikiriavyo, ukikosea ni sehemu ya mchezo wa soka.
Baada ya mazingira hayo magumu kwa wachezaji wa
Simba, uongozi ukasikiliza kero zao za chini kwa chini na kuamua kuachana na
Loga aliyedaiwa kuwatukana Amri Kiemba, Shaaban Kisiga na wengineo baada ya
kufungwa mabao 3-0 na Zesco United ya Zambia katika mechi ya Tamasha la ‘Simba
Day’, Agosti 9 mwaka huu uwanja wa Taifa.
Mzambia Patrick Phiri alichukua mikoba na kwa mara
ya kwanza jana ameiongoza Simba katika mchezo wa kimataifa wa kirafiki dhidi ya
mabingwa wa Kenya, Gor Mahia ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Simba ilishinda mabao 3-0 ambapo Mkenya Paul
Kiongera alifunga mawili na Ramadhani Singano ‘Messi’ alishindilia moja.

Mafanikio?: Aliyekuwa kocha wa Simba, Logarusic aliwafunga Yanga mabao 3-1 na kutwaa kombe la Nani Mtani Jembe mwezi desemba kwa jana uwanja wa Taifa.
Wakati mashabiki wakifurahia ushindi huo, binafsi
nilikuwa nawatazama wachezaji wa Simba kwa jicho la tatu na nilibaini baadhi ya
mambo ya msingi kuongezeka kwao.
Mosi; lugha ya miili yao ‘Body language’ ilionesha
kuwa wapo huru kucheza mpira. Walikuwa wapesi na kufanya kila wanachotaka
tofauti na kipindi cha Loga.
Wachezaji kama ‘Messi’, Kiongera, Uhuru Seleman,
Shaaban Kisiga walionekana kuonana vizuri na mawasiliano yao yalikuwa
mazuri. Hawakuonekana kuwa na hofu ya
kukosea, walicheza kwa kujiamini, kwa uhuru na ilisaidia sana kuifanya Simba
iwe na makali kipindi cha pili.
Kipindi cha Loga wachezaji hawakuwa na uhuru, hofu
ilitanda na walishindwa kutumia tafsiri za akili zao katika kuucheza mpira.
Muda wote waliwaza maelekezo ya mwalimu.
Katika mpira maelekezo ya kocha ndio hutumika
kucheza mpira,lakini kuna mazingira inakulazimu kutumia akili yako. Na ndicho
kilionekana kwa wachezaji wa Simba.
Pili; ladha ya mpira wa Simba ilionekana. Kwa
kawaida Watanzania wengi wanapenda sana kuona mpira wa pasi ‘passing football’.
Na huo ndio utamaduni wa Simba kwa muda mrefu.
Kocha mkuu wa Simba sc, Patrick Phiri
Simba wana utamaduni wa kuweka mpira chini na
kupiga pasi fupi fupi, lakini kwa muda mrefu mpira wa aina hiyo ulipotea.
Lakini kurejea kwa Phiri kumeonekana kuwa chachu ya kurudi kwa mpira huu.
Wachezaji hasa kipindi cha pili walicheza vizuri
kuanzia katikati na walionana kwa pasi zilizosisimua mashabiki wa Simba.
Tatu; wachezaji wanaonekana kumridhia Phiri. Kocha
huyu ni kipenzi cha mashabiki na viongozi wa Simba. Historia yake ni kubwa
Msimbazi. Mara baada ya kurudi tena kwa mara ya tatu, wachezaji walionekana
kumkubali na wengine kuonesha furaha yao kwa kujaribu kumueleza kero walizokuwa
nazo.
Phiri ni mtu mzima, lakini hana ‘udingi’. Anapenda
sana kuzungumza na wachezaji na siku zote huwafanya kuwa marafiki zake. Hana
ukali usiokuwa na sababu. Ni mwalimu anayependa zaidi kuelekeza kuliko kufoka.
Huwa anayakubali makosa na ana amini ni sehemu ya
mchezo. Na ndio maana wachezaji wanapasiana kwa uhuru, wanacheza kwa kuonesha
vipaji binafsi na kucheza kitimu. Simba walionekana kuwa na ushirikiano mzuri
kuanzia nyuma mpaka mbele.
Viungo walicheza vizuri na kuipandisha timu na
hatimaye kutengeneza nafasi za kufunga.
Unaweza kusema Gor Mahia hawana ukali kwa sasa, lakini
nadhani ilikuwa muhimu kuangalia namna Simba walivyocheza vizuri.
Nne; mashabiki wa Simba wameonekana kujenga imani katika
timu yao. Kama una kumbukumbu nzuri, msimu uliopita, hususani mechi za mwishoni
katika mzunguko wa pili, mapato ya mlangoni kwa Simba yalipungua mno.
Kuna wakati mapato ya jumla yalikuwa milioni 20
tu. Haikuwa kawaida kwa timu kubwa kama Simba, lakini ililazimika kuwa hivi
kutokana na mashabiki wengi kuisusa timu ya Loga.
Wachezaji walionekana kucheza chini ya kiwango na
ilitafsiriwa kama ni kumgomea Loga. Dhahiri, kocha huyu hakupendwa. Mashabiki
hawakwenda uwanjani kwa wingi, wakati wa Yanga waliendelea kumiminika.
Lakini kama ulikuwepo jana uwanjani, mashabiki
walifurika kwa wingi ukizingatia ni mechi ya kirafiki. Walionekana kuwa na
imani kubwa na Phiri na walishangilia kwa muda wote wa mechi na kuwakera wenzao
wa upande wa pili.
Nadhani nguvu na uumoja umerejea simba na hii itawasaidia
kufanya vizuri uwanjani. Cha msingi, wana Simba wote wanatakiwa kumuamini kocha
na wachezaji wake. Wampe muda ili afanye kazi yake.
Phiri ni Simba, Phiri ni kocha sahihi kwa Simba
kwasababu ni mwenyeji Msimbazi na anaijua Simba vizuri mno. Simba ni kama
nyumbani kwake, na ndio maana unaona timu inarudi kwa muda mfupi baada ya
kushika hatamu. Sijui nini kitatokea baadaye, lakini kwa kiwango cha jana ‘Well
done’ Simba Sports Club.
Jumapili njema!
0 comments:
Post a Comment