Na
Baraka Mbolembole, Dar es Salaam,
Unamkumbuka,
Ruud Voller?. Hata kwa kutazama video zake za miaka ya nyuma. Voller alifunga
bao la ushindi katika mchezo wa fainali za kombe la dunia, mwaka 1990 wakati
Ujerumani ilipoishinda Argentina kwa mabao 2-1.
Enzi
za uchezaji wake mashabiki wa soka nchini Ujerumani walimpachika jina la '
bingwa wa magoli yasiyovutia duniani'. Magoli ya Voller yalikuwa hayasisimui
kama magoli yanayofungwa na akina Cristiano Ronaldo, Zlatan Ibrahimovic,
Neymar, Leonel Messi.
Kilichovutia
katika moyo wa Voller ni kuhakikisha anafunga mabao kadri inavyowezekana na
kuisaidia timu yake kushinda mataji. Jina halitafutika kamwe kwa kile
alichoifanyi nchi yake, rekodi yake ya mabao katika ligi ya Bundesliga bado
inasomeka na sifa yake ni ileile hadi sasa, ' bingwa wa mabao yasiyovutia
duniani'.
Ulimuona mshambulizi, Geilson Santos ‘ Jaja’
katika mchezo wa jana wakati timu yake ya Yanga ilipofanikiwa kupata ushindi ‘
mwembamba’ wa bao 1-0 dhidi ya Thika United ya Kenya katika mchezo wa kimataifa
wa kirafiki?. Je ni mchezaji wa aina gani? Ataisaidia Yanga? Kuna baadhi ya
mashabiki walionekana kumzomea mshambulizi huyo kutoka Brazil wakati mchezo
ukiendelea, lakini dakika 15 baada ya kuanza kipindi cha pili mchezaji huyo
akawanyamazisha kwa bao la ‘ kujituma’ akiwahi katika nafasi ambayo krosi ya
Saimon Msuva ilikuwa ikikatiza.
MCHEZAJI MVUMILIVU
Jaja ni mzito, mwili wake wenyewe ni mzito lakini
goli lake limekumbusha kitu muhimu kuwa uzito wake haupo hadi katika kujipanga
na kutumbukiza mpira nyavuni. Akili yake ina uharaka na mchezaji ambaye
anafikia maamuzi ya kujaribu kufunga hata kama sehemu aliyopo ni ngumu. Hakuwa
na lolote katika kipindi chote cha kwanza lakini aliwafanya viungowanne
wachezesha timu kuwa huru. Alijitahidi kuituliza mipira na kupiga pasi kwa
wenzake, kitu kingine alionyesha namna anavyoweza kutumia uzito wake kuwabana
walinzi wa timu pinzani.
Haijalishi kama bao lake ni la kuvutia ama sivyo,
lakini kilicho bora ni kwamba alifunga bao akicheza kama mshambulizi huru kwa
dakika 87 na kutimiza jukumu hilo ipasavyo. Mwalimu Maximo alimvumilia mchezaji
huyo licha ya kukutana na changamoto za kuzomewa katika kipindi cha kwanza. Na
jambo hilo lilimfanya mchezaji huyo kuendelea kucheza kwa kujiamini. Mchezaji
pia alionyesha uvumilivu kutokana na kile alichokishuhudia katika baadhi ya
majukwaa. Maximo ameanza vizuri.
JAJA KUFUNGA KATIKA UWANJA WA TAIFA KATIKA MCHEZO
WAKE WA KWANZA.
Ni kitu kizuri kwa mchezaji mpya kufunga mbele ya mashabiki wa klabu
yako katika mchezo wa kwanza ndani ya uwanja wa nyumbani. Wakati kocha wake
akifurahia na kufanikiwa kwa mbinu zake, Jaja amefanikiwa kufanya vizuri licha
ya kwamba si kwa kiwango cha juu. Ingekuwa si vizuri kushindwa kufunga wakati
nyuma yake alichezeshwa Msuva, Haruna Niyonzima akicheza kama kiungo mchezesha
timu akitokea katikati ya uwanja, Hassan Dilunga akichezesha timu akitokea
upande wa kulia na Countinho akifanya hivyo akitokea upande wa kushoto.
Viungo hao
wanne wote ni wachezesha timu wazuri hivyo hakukuwa na sababu ya Jaja kucheza
dakika 87 bila kufunga. Ametoa zawadi nzuri kwa mashabiki wa timu yake. Mabao
mawili katika michezo minne, bila shaka ataendelea kufunga zaidi katika ligi
kuu. Jaja si Voller ila anaweza kufunga zaidi mabao kama ilivyokuwa kwa kina
Ambani Boniface na Maurus Sunguti, Yanga haijawahi kuwa na mshambulizi wa
kuvutia ila daima wametoa wafungaji bora wa ligi kuu Bara mara kibao, sijui kwa
Jaja ila ataendelea kuwafunga magoli yasiyovutia na atajiwekea sifa yake kama
Ambani kama amtamuheshimu.
0714 08 43 08

0 comments:
Post a Comment