
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
WEKUNDU wa Msimbazi wanatarajia kucheza mechi ya
kimataifa ya kirafiki dhidi ya mabingwa wa ligi kuu nchini Kenya, Gor Mahia
siku ya jumamosi katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam.
Geofrey Nyange ‘Kaburu’, makamu wa Rais wa Simba
sc, amewaambia waandishi wa habari leo jijini Dar es salaam kuwa kikosi cha Gor
Mahia kitawasili kesho uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Mwalimu Julius Nyerere
jijini Dar es salaam kikitokea Nairobi kwa kutumia ndege ya shirika la Kenya.
Kaburu aliongeza kuwa nacho kikosi cha Simba
kitawasili siku hiyo hiyo kikitokea Zanzibar kilipoweka kambi ya kujiwinda na
ligi kuu.
Licha ya kukipiga na Simba, Gor Mahia imeomba
kucheza mechi mbili, hivyo siku ya jumapili watakuwa na mechi nyingine ya
kirariki wakati kikosi cha Patrick Phiri kitarejea Zanzibar kuendelea kumalizia
program zake za maandalizi kabla ya ligi kuanza septemba 20 mwaka huu.
Awali Simba walipanga kuchuana na Mtibwa Sugar,
lakini kocha Phiri akapendekeza kutafutiwa mechi ngumu ya kimataifa ili
kuangalia namna kikosi chake kilivyoimarika.
Mechi ya jumamosi itakuwa fursa nzuri kwa
mashabiki wa Simba kuwaona wachezaji wao akiwemo mshambuliaji hatari aliyerejea
Msimbazi, Mganda Emmanuel Anord Okwi ambaye atavalia jezi yake namba 25
aliyokuwa anaitumia kabla ya kutimkia Etoile Du Sahel ya Tunisia.
Kaburu alisema viingilio katika mechi hiyo ni
shilingi elfu 5 (5,000) kwa viti vya kijana, viti vya rangi ya chungwa ni
shilingi 10,000, VIP C na B itakuwa shilingi 2,000 wakati VIP A itakuwa
shilingi elfu 30,000.
Tiketi kwa ajili ya mchezo huo zitaanza kuuzwa
siku ya mechi kuanzia majira ya saa 4:00 asubuhi.
Simba wataanza kampeni za kusaka ubingwa wa ligi
kuu bara septemba 21 katika uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam dhidi ya
Coastal Union.
0 comments:
Post a Comment