
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
0712461976
Imechapishwa Agosti 4, 2014, saa 5:22 asubuhi
MPIRA wa miguu ni mchezo wa mipango, huwa hauna
njia ya mkato ili kufikia kilele cha mafanikio.
Mataifa yote yaliyofanikiwa na yanayoendelea
kufanikiwa katika mchezo wa soka ni kutokana na uwekezaji mkubwa na mipango
thabiti hasa katika soka la vijana.
Nchi kama Ujerumani, imelitengeneza soka lake kwa
zaidi ya miaka 10 mpaka kufikia mafanikio ya kutwaa ubingwa wa kombe la dunia
majira ya kiangazi mwaka huu nchini Brazil.
Ujerumani imetengeneza mfumo sahihi wa soka la
vijana, kila timu inayoshiriki ligi kuu nchini humo, Bundesliga ina timu bora
ya vijana wa umri toafuti, walimu wenye taaluma za juu na akademi za uhakika.
Vijana wengi wanazalishwa kwa ajili ya kutumika
katika timu za wakubwa kwa baadaye. Timu zina malengo ya muda mrefu.
Hali hii inasababisha urahisi kuunda timu ya Taifa
ya vijana ya Ujerumani, na ndio maana juzi juzi tu wamelitishia soka la dunia
baada ya timu ya Taifa ya chini ya miaka 19 kutwaa ubingwa wa kombe la Ulaya
kwa vijana.
Kaka zao wametoka kutwaa kombe la dunia kwa
mipango sahihi, madogo nao wanafuata nyayo zao. Hakika mpira ni mpango na sio
njia ya mkato ‘shortcut’.
Hata ukifuatilia Hispania, wametawala kwa muda
mrefu katika soka la dunia kwasababu ya uwezaji mkubwa walioufanya katika soka
la ndani. Pia Uholanzi wana Historia ya kuwa na mipango mizito katika soka la
vijana.
Nchi kama Cost Rica, Colombia, Uruguay, Korea
Kusini, Iran zimejitahidi kusogea mpaka kufika pale zilipo kutokana na
uwezezaji na mipango sahihi.
Afrika magharibu imetawala soka la Afrika kwa muda
mrefu kwasababu ya uwezezaji mkubwa walioweka pamoja na kujali soka la vijana.
Jana Tanzania imetolewa na Msumbiji katika
michuano ya kuwania kufuzu fainali za mataifa ya Afrika, mwakani nchini
Morocco.


Stars ilitoka sare ya 2-2 uwanja wa Taifa jijini
Dar es salaam wiki mbili zilizopita na jana ilifungwa mabao 2-1 katika uwanja
wa Taifa wa Zimpeto, nje kidogo ya Mji wa Maputo, hivyo kutolewa kwa wastani wa
mabao 4-3.
Baada ya mechi hiyo, nimefuatilia mijadala mingi
ya watu wa mpira. Kila mtu anasababu zake na maoni yake. Wapo wanalilaumu benchi
la ufundi chini ya kocha mkuu Mart Nooij, wengi uongozi wa TFF na wengine
wanawabebesha lawama zote wachezaji.
Walio wengi wanalaumu kuwa wachezaji wa Tanzania
kwa asilimia zote ni wabovu, sio wazalendo na hawana malengo na nchi yao.
Kiufupi! lawama zote zinaweza kuwa sahihi
kwasababu yanapotea makosa , lazima wa kulaumiwa awepo. Wachezaji wanabeba
msalaba kwasababu wao ndio wanaocheza mpira wakati wengine ni mashabiki tu.
Kimsingi, tatizo kwa soka letu lipo. Kabla ya
mechi ya jana, jumamosi timu ya taifa ya vijana chini ya miaka 17, Serengeti
Boys ilifungwa mabao 4-0 na Afika kusini ‘Amajimbos’ na kutupwa nje ya michuano
ya kufuzu fainali za vijana.
Rais wa TFF, Jamal Malinzi alishuhudia mechi hiyo
na baada ya mechi alikiri wazi kuwa tatizo la timu zetu ni maandalizi mabovu yatokanayo
na uwezo mdogo wa kiuchumi pamoja na kukosekana kwa mfumo sahihi wa soka la
vijana.
Malinzi aliongea vitu mbalimbali, lakini niliona
ana hoja kubwa katika mpango wa soka la vijana. Alisema wapo kuandaa mpango
maalumu wa kitaifa wa soka la vijana ili kupata muendelezo mzuri wa soka la
vijana na hatimaye timu ya taifa ya wakubwa.
Hakuna jinsi ya kuchomoka hapa tulipo bila Taifa
kukubali kukaa chini na kuangalia mfumo wake wa soka la vijana na hatimaye
kutafuta njia ya kuboresha zaidi.
Soka la vijana litatusaidia. Kuna haja ya kuwa na
akademi zitakazowalea wachezaji wetu kuanzia miaka 10-12, 12-14, 14-16, 16-18,
18-21 na hatimaye timu ya wakubwa.
Mchezaji mzuri wa miaka 10-12 anapofikisha miaka
14, anatakiwa kuhamia daraja la 14-16 na kuendelea kadiri miaka inavyozidi
kukatika.
Manake kama mchezaji ataendelea kubakia katika
kiwango chake, anaweza kujikuta amefika timu ya wakubwa akiwa ameshacheza timu
zaidi ya tatu za Taifa za vijana. Hii itakuwa faida kubwa.
Pia itawafanya wachezaji kujijenga kiuchezaji na
kuwa wazalendo kwa nchi. Itakuwa rahisi kupata timu ya taifa imara.
Tutalaamu , tutatukana, lakini mwisho wa siku,
viongozi na wadau wa soka, hawawezi kukwepa kurudi katika soka la vijana kama
wanataka kufika Morocco.
Mimi siamini kama tutakuja kufanikiwa bila kurudi
nyuma zaidi. Tutaendelea kutiana moyo na kuombeana dua, wakati nao maadui zetu wanaomba Mungu huyo
huyo.
Unadhani Mungu atamsaidia nani kati ya
aliyejiandaa vizuri na akamuomba na yule aliyejiandaa kwa tia maji tia maji
kama sisi?
Tutaona Mungu anawapendelea wenzetu na kuona hana
maana kwetu, kumbe wachawi wa soka letu ni sisi wenyewe. Mwisho wa siku
tutakufuru kwa madai ya Mungu kutusahau Watanzania. Mungu habariki penye
sifuri.
Asubuhi njema kwa wote!
0 comments:
Post a Comment