
Na Baraka Mpenja
Imechapishwa Agosti 2, 2014, saa 12:33 jioni
TIMU ya Taifa ya Tanzania ya vijana chini ya miaka
17, Serengeti Boys imebugizwa mabao 4-0 dhidi ya timu ya Taifa ya vijana wa
umri huo ya Afrika kusini maarufu kama Amajimbos katika mchezo wa kuwania
kufuzu fainali za vijana za mataifa ya Afrika.
Mechi hiyo rahisi kwa Afrika kusini imepigwa jioni
ya leo katika uwanja wa Dobsonville uliopo Soweto na kushuhudia wenyeji
wakitoka na furaha.
Taarifa kutoka nchini Afrika kusini zineeleza kuwa
vijana wa Serengeti walizidiwa kila idara na wangepigwa hata mabao 7 kwasababu
Amajimbos walikosa nafasi nyingi za wazi.
Serengeti ambao hawakuandaliwa tangu siku nyingi, wiki mbili zilizopita walitoka suluhu ya bila
kufunga katika mchezo wa kwanza uliopigwa uwanja wa Azam Complex, Chamazi nje
kidogo ya jiji la Dar es salaam.
Licha ya suluhu hiyo, kwa kiasi kikubwa Amajimbos
walitawala mchezo huo na kuonekana kuwa vizuri kiufundi na kimbinu.
Mechi ya marudiano mjini Soweto imekuwa nyepesi
kwa wenyeji na sasa Serengeti imetolewa
kwa wastani wa mabao 4-0.
Kaka zao Taifa stars wanashuka dimbani kesho
kwenye uwanja wa Taifa wa Zimpeto uliopo nje kidogo ya jiji la Maputo dhidi ya
wenyeji Msumbiji, kuwania kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kucheza
fainali za mataifa ya Afrika mwakani nchini Morocco.
Mechi ya kwanza iliyopigwa wiki mbili zilizopita
ndani ya uwanja wa Taifa jijini Dar es salaam, Taifa Stars ilitoka sare ya
mabao 2-2 na sasa inahitaji ushindi au sare ya kuanzia mabao 3-3 ili kusonga
mbele.
0 comments:
Post a Comment