Mdau wa soka, Mtemi Ramadhani amelaumu maandalizi ya zima moto kwa timu za taifa za vijana
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 3, 2014, saa 6:02 mchana
KUKOSEKANA kwa wafadhili na wadhamini katika soka
la vijana, maandalizi duni ni miongoni kwa sababu za timu za taifa kuboronga katika
michuano ya kimataifa.
Mchezaji wa zamani na mdau wa soka nchini, Mtemi
Ramadhani jana alikuwa shuhuda wa mechi baina ya timu ya vijana ya Tanzania
chini ya miaka 17, Serengeti Boys na Afrika kusini ambapo wenyeji waliibuka na
ushindi mnono wa mabao 4-0.
Mtemi baada ya mechi hiyo alisema: “Mchezo haukuwa
mbaya sana wala mzuri sana. Hali ya uchezaji: wachezaji walianza vizuri, lakini
sasa hapa pana baridi kali, baadaye vijana walikuja wamechoka sana, kwahiyo wenzetu
wakacheza sana na kutufunga mabao 4-0 na tunamshukuru mungu wametunga hayo, kwakweli
wangetufunga hata mabao 7 au 8”.
Kutokana na matokeo hayo mabaya, mtandao huu
ukataka kujua wapi kuna makosa katika soka la vijana. Mtemi akafunguka:

“Kwanza timu zetu hizi tuzilee kwa muda mrefu,na
kama unavyoelewa timu yetu hii ya vijana haina wafadhili wala wadhamini,
nafikiri kama tungepata watu hawa, timu ingefanya mazoezi ya muda mrefu, vijana
wakawa pamoja kwa muda mrefu, nafikiri jambo hili lingetusaidia nchi kutoka
hapa tulipo”.
‘Lakini hii kusema labda tunacheza baada ya maandalizi ya wiki
moja au mbili, haitusaidii. Vijana wanakosa uzoefu. Hata ukiangalia vijana wetu
hawa , hii ni mechi ya pili tu, kiukweli wanatakiwa wapate uzoefu, wapate
wafadhili, wacheze mechi nyingi za kimataifa za kirafiki. Afrika kusini wapo
mbali, wapo juu kimchezo, unaweza kuona tofauti yao na sisi”
Tayari tatizo lipo, Mtemi akiwa mdau wa soka
nchini alitoa wito: “Ombi langu, wadhamini
wajitokeze kudhamini timu za vijana, sio timu kubwa tu. Vijana wapate uzoefu,
wakae kambini muda mrefu na wacheze mechi mbalimbali za kirafiki za kimataifa”
Serengeti Boys inawasubiri kaka zao wa Taifa Stars
ili warudi pamoja nchini.
Stars inashuka dimbani jioni ya leo kukipiga na
timu ya taifa ya Msumbuji ‘Black Mambas’ katika mchezo wa marudiano, kuwania
kupangwa hatua ya makundi ya kusaka tiketi ya kushiriki fainali za mataifa ya
Afrika, mwakani nchini Morocco.
Mechi ya kwanza jijini Dar es salaam, Taifa Stars
ilitoka sare ya mabao 2-2 na ili kusonga mbele inahitaji ushindi wa aina yoyote
au sare ya kuanzia mabao 3-3.
0 comments:
Post a Comment