
Kocha mkuu wa Yanga sc, Marcio Maximo (kushoto) akimuelekeza jambo mshambuliaji wa klabu hiyo, Jerryson John Tegete (kulia)
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Agosti 3, 2014, saa 2:10 usiku
YANGA SC inatarajia kuanika hadharani wachezaji
watakaoitumikia klabu hiyo msimu ujao wa ligi kuu soka Tanzania bara na
michuano ya kombe la shirikisho na wale watakaoachwa Agosti 17 mwaka huu.
Afisa habari wa Yanga sc, Baraka Kizuguto
amekaririwa na baadhi ya vyombo vya habari jioni ya leo akisema kuwa zoezi la
usajili linaendelea vizuri ambapo viongozi wa kamati ya usajili wanashirikiana
kwa karibu zaidi na benchi la ufundi chini ya kocha mkuu, Mbrazil, Marcio Maximo.
“Mwalimu anaendelea kufanyia kazi ripoti yake
pamoja na kutaja wachezaji anaowahitaji. Siku itapofika ambayo ni Agosti 17,
mwalimu ataweka kila kitu hadharani,” alisema Kizuguto.
Baada ya Maximo kuwasajili wachezaji wawili kutoka
Brazil, kiungo mshambuliaji Andrey Coutinho na mshambuliaji Gleison Santos
Santana ‘Jaja’, Yanga imefikisha wachezaji sita wa kigeni.
Kwa mujibu wa sheria inayotumika kwa wachezaji wa
kigeni kwa sasa, kila klabu ya ligi kuu inatakiwa kuwa na wachezaji wa kigeni wasiozidi
watano, hivyo Yanga inatakiwa kumuacha mmoja.
Kumekuwa na mjadala mzito wa nani anaichwa
hususani kwa Waganda wawili, Khamis Kiiza na Emmanuel Okwi, lakini Kizuguto
alisema kila kitu ni Agosti 17 mwaka huu.
“Kuna Mbuyu Twite, Khamis Kiiza, Haruna Niyonzima
na Emmanuel Okwi, wote hatima yao itajulikana Agosti 17, hapo itajulikana nani
atabaki Yanga na nani ataondoka,” aliongoza Kizuguto.
0 comments:
Post a Comment