
…..Tunakiwa kumaliza mechi Dar es Salaam
…...Mimi ni mshambulizi wa kati
Na Baraka Mbolembole
Imechapishwa Julai 11, 2014, saa 7:06 mchana
Timu ya Soka ya Taifa ya Tanzania, Taifa Stars
itacheza na ile ya Msumbiji, Black Mambas mwishoni mwa wiki ijayo katika uwanja
wa Taifa, Dar es Salaam.
Stars chini ya Mwalimu,Martin Nooij tayari
imeingia kambini,Tukuyu Mbeya, mwanzoni mwa wiki hii ikitokea nchini Botswana
ilipokuwa na kambi ya mafunzo ya wiki mbili.
Mchezo huo wa kwanza wa mtoano kuwania nafasi ya
kufuzu katika hatua ya makundi kuwania tiketi ya kucheza michuano ya Mataifa
Afrika, AFCON 2015, nchini Morocco unataraji kuwa mgumu kwa kila upande.
Msumbiji iliifunga Stars katika mchezo wa mwisho
wa hatua ya makundi kuwania nafasi ya kufuzu kwa fainali za Afrika mwaka 2008
nchini Ghana.
Stars
ililazwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza wa mashindano katika uwanja wa Taifa,
septemba, 2007, bao maridadi la mpira wa kichwa lililofungwa na aliyekuwa
nahodha wa Msumbiji, Tico Tico.
Miaka miwili iliyopita timu hizo zilikutana katika
michezo ya mtoano kuwania kufuzu kwa fainali zilizofanyika nchini Afrika
Kusini,2013 na Stars iliondolewa kwa changamoto ya mikwaju ya penalti.
“ Mechi ya wiki ijayo itakuwa ngumu, naamini
Msumbiji nao watakuja wakiwa wamejipanga kuhakikisha hatupati ushindi katika
uwanja wa nyumbani” anasema mshambulizi, Mbwana Samatta ambaye alipoteza mkwaju
wa mwisho wa penalti na kuitupa nje Stars.

Msumbiji walilazimisha sare ya bao
1-1 katika uwanja wa Taifa,wiki mbili baadaye, Stars iliyokuwa chini ya Kim
Poulsen ilipata matokeo kama hayo kabla ya kuchapwa katika mipigo ya penalti.
Samatta, mfungaji bora wa kombe la Shirikisho
barani Afrika 2013 akiwa na klabu yake ya TPMazembe ya DRC, amekuwa na uzoefu
wa kutosha sasa kuhusiana na michezo ya kimataifa ya mtoano bila shaka
mshambulizi huyu anaweza kuisaidia zaidi Tanzania katika mchezo ujao kutokana
na mafanikio ambayo tayari yameonekana wakati akiwa katika uwakilishi wa klabu
yake.
“ Muhimu siyo kutazama mchezaji mmoja mmoja au
timu inacheza kwa kiwango gani, ndiyo wakati mwingine mashabiki wanakuwa
wakifurahia mpira tunaocheza, lakini kitu muhimu zaidi ni kufunga mabao ya
kutosha” anasema, Samatta wakati alipofanya mahojiano na mtandao huu.
Kila mtu anafahamu kuwa mchezo huo utakuwa mgumu,
lakini umefikia wakati ambao Stars inatakiwa kufuzu kwa michuano CAN, katika
miaka minne iliyopita timu imeshindwa kufikia lengo hilo katika michuano mitatu
tofauti, kuna kitu chochote kimepatikana kutoka kwa wachezaji? Wachezaji wamejifunza
nini kutoka katika michuano iliyopita?
“ Kuna kitu
kimeongezeka kwa timu na kwa mchezaji mmoja mmoja, hivi sasa wachezaji wa Taifa
Stars wanajiamini sana wanapokuwa mchezoni, pasi ni nzuri na unakutana hata
katika eneo letu la ulinzi wachezaji wanakuwa na utulivu, wanapasiana bila hofu yoyote".

"Tunacheza
vizuri nyumbani na huwa tunafanya hivyo katika michezo ya ugenini” anasema
mshambulizi huyu namba moja wa TP Mazembe. Na kuongeza ;” Kinachotakiwa ni ‘Kutwist’
vichwa vya wachezaji ili waelewe
majukumu yao na kuifahamu vizuri timu pinzani, hili ni jukumu ambalo linatakiwa
kufanywa na waandishi wa habari pia. Inasaidia kuwafanya wachezaji waelewe
mchezo ulio mbele yao”
Tanzania ilitolewa na Msumbiji miaka miwili
iliyopita katika michuano kama hii, ili kufuzu kwa fainali za Morocco,Stars
inalazimika kuitoa kwanza ,Black Mambas ili kuungana na timu za Zambia, Niger
na Cape Verde kuwania tiketi mbili za kundi hilo ambazo zinaweza kupatikana,
lakini kwa kulipa kisasi cha timu hiyo ya Kusini mwa Afrika
“ Kwanza ni lazima tumalize mechi Dar es
Salaam,hatutakiwi kufanya kama wakati ule tuliposhindwa kupata ushindi katika
uwanja wa nyumbani” anasema Samatta ambaye amekuwa akipangwa katika nafasi ya
mshambulizi wa pembeni au mshambulizi wa pili katika timu ya Taifa.

Samatta amefunga
mabao sita katika michezo17 inayotambulika na FIFA kuanzia mwaka 2011 alipoitwa
kwa mara ya kwanza na kocha Jan Poulsen.
Poulsen alimuingiza kikosini akiwa na miaka 18 na
haraka akamuamini kama mshambulizi wa kwanza katika kikosi chake. Alifunga mabao
manne ndani ya mwaka mmoja aliofanya kazi na Jan lakini tangu timu hiyo
ikinolewa na Kim Poulsen, Samatta amekuwa ‘butu’ katika ufungaji japokuwa
amekuwa mfungaji wa kutegemewa sana katika klabu yake ya TP Mazembe.
“ Nachoweza
kusema nimekuwa makini na mtulivu, na wakati mwingine huwa nasema ni bahati
kutoka kwa Mungu. Mimi ni ‘ mwanajeshi wa mbele’ mshambulizi wa kwanza kabisa,
hivyo ndivyo ninavyotumika katika klabu yangu na nimekuwa nifunga mabao ya
kutosha kutokana na kupangwa katika nafasi hiyo nayoipenda. Mchezaji huwezi
kujichagulia nafasi ya kucheza katika timu, mahitaji ya Mwalimu ndiyo jambo la
msingi"
" Napenda kucheza katika nafasi yoyote nayopangwa Stars kutokana na mfumo
wa kocha anavyotaka” anasema Samatta amekuwa akipangwa nyuma ya mshambulizi,
John Bocco katika timu ya Taifa.
“ Siwezi kusema kama huwa nina furaha au laa!,
naweza kufurahia kama nikipangwa katika wingi ya kushoto, au mshambulizi wa
kwanza na si nyuma ya mshambuliaji wa kwanza kwa sababu nakosa nafasi ya
kuuchezea mpira”
Naweza kufurahi km nikicheza km winga ya kushoto
au streka sio nyuma ya streka.

Mechi 17 za Fifa, mabao sita inamaanisha nini kwa
mshambulizi huyu unayependwa nchini Tanzania. “ Bado sijafanya nachopenda
kufanya, lakini inatokana na ufinyu wa michezo, bado nina imani wakati upo wa
kufanya mambo makubwa kwa Taifa langu, kufunga mabao kadri inavyowezekana ili
kukaribiana idadi ya michezo”anasema mchezaji huyo anayedai anafunga mabao
mengi katika klabu yake kutokana na kuzungukwa na wachezaji wengi wa kulipwa,
kitu ambacho hakipo kwa Stars.
Samatta ametoa wito kwa mashabiki wa soka nchini
kuwapa sapoti wachezaji wao katika muda wote wa mchezo na kuwafanya wageni wao
kuingia mchecheto. Hivyo ndivyo mazingira ya uwanja yanavyokuwa katika uwanja
Stade de TP Mazembe wakati timu ngeni zinapokuwa zikitembelea katika uwanja
huo.
“ Mashabiki wana mchango mkubwa sana katika mchezo
kama huo,wanatakiwa kuinuka katika viti vyao na kuimba wimbo wa Taifa pamoja na
wachezaji. Kuishangilia timu muda wote ili kuwafanya Msumbiji wajione wapo
ugenini hasa. Waje kwa wingi uwanjani siku ya mchezo kuipa sapoti timu”
0714 08 43 08
Chanzo:shaffihdauda.com

0 comments:
Post a Comment