Wanalambalamba, Azam fc watahimili kasi ya Yanga, Simba na Mbeya City ili kutetea ubingwa wao msimu ujao?
Na Baraka Mpenja, Dar es salaam
Imechapishwa Julai 3, 2014, saa 3:00 asubuhi
MABINGWA wa ligi kuu soka Tanzania bara, Azam fc
wanatarajia kuweka kambi nje ya nchi kwa lengo la kujiimarisha zaidi kabla ya
kuanza harakati za kutetea ubingwa wao pamoja na kucheza ligi ya mabingwa
barani Afrika mwakani.
Jemedari Said, meneja wa Azam fc amesema wamepokea
mialiko kadha wa kadha, lakini wanasubiri kocha mkuu, Mcameroon, Joseph Marius Omog achague wapi
atakwenda.
“Ratiba ya kwenda nje ya nchi ipo. Kuna mialiko
kadha wa kadha. Mwalimu baada ya kufanya maandalizi ya hapa nyumbani, yeye
ndiye atachagua wapi pa kwenda. Yeye atachagua ni wapi anaona akienda timu
itafanya maandalizi mazuri na kushiriki vizuri katika michuano ya CAF na ligi
kuu”. Alisema Jemeadari.

Azam fc wameshaanza mawindo ya msimu mpya chini ya kocha Mcameroon, Joseph Marius Omog.
Jemedari aliongeza kuwa walipozungumza na mwalimu
alisema hatapeleka timu sehemu yoyote kwa ajili ya kujifurahisha bali atapeleka
timu ambapo itapata uzoefu wa ligi ya mabingwa na itakuwa ni faida pia kwa ligi
ya nyumbani.
Meneja huyo alisema kama mwalimu wao ataamua
kuipeleka timu sehemu ilipokuwa msimu uliopita na kutwaa ubingwa kwa maana ya
Afrika kusini hilo ni juu yake na kama ataamua kwenda sehemu nyingine, pia ni
maamuzi yake.
Hata hivyo kuna taarifa zisizo rasmi kuwa Azam
wanatarajia kuweka kambi nchini Kenya au Amerika, lakini uongozi haujasema
lolote zaidi ya kumsubiri Omog achague sehemu ya kuweka chimbo lake.


0 comments:
Post a Comment